MITALA ni ndoa ambayo mwanaume huwa na
zaidi ya mke mmoja. Hii ni kwa mujibu wa imani ya dini yake au mila/jadi
ya kabila lake. Ndoa hizi hazikuanza leo. Ndoa hizi zimekuwepo karne kwa
karne, toka kabla ya Nabii Issa (a.s.) na hata baada ya Nabii Muhammad
(s.a.w.).
Na Asia Mohamed
NABII Muhammad mwenyewe alikuwa na wake wengi. Pamoja na wanawake vijana alioa wanawake wajane na walioachwa na waume zao ili kuwaondoa majonzi ya kufiwa au kuachwa na waume.
Kwa mujibu wa Hadithi za Mtume, Muhammad (s.a.w.) aliwahi kumwoa bibi mmoja akiitwa Sauda, baada ya baba yake Sauda kumwomba Mtume amsitiri bintiye baada ya kukataliwa na wanaume kwa ajili ya ukali wake. Bibi huyu alikuwa mkali sana na wanaume wengi walimwogopa.
Wafalme na machifu walikuwa na desturi ya kuoa wanawake wengi kama sifa na heshima na desturi hii imeendelea mpaka leo katika nchi ambazo machifu na wafalme wanaendelea kutawala, mfano Swaziland, mfalme Mswati anaendelea mpaka leo kuoa kila mwaka.
Lakini sasa tukirudi upande wa kijamii, kwa mfano hapa kwetu Tanzania, kuna ndoa za kiserikali, kimila na kijadi.
Kwa Wakristo, ndoa ni mme/mke mmoja mpaka kifo kiwatenganishe.
Waislamu kwa mujibu wa dini yao wameruhusiwa kuoa kuanzia wake wanne (4) mpaka mmoja kwa watakaoshindwa uadilifu.
Uadilifu unaozungumziwa hapa ni haki sawa kwa wanawake unaowaoa. Kila mmoja apate sawa na mwenzake, na atakayeshindwa basi na akae na mke mmoja.
Kwa upande wa mila, ndoa hizi hufungwa kwa kufuata taratibu za kabila husika, kuanzia posa, mahari mpaka ndoa yenyewe. Hii pia huweza kuwa ya mke zaidi ya mmoja.
Kwa upande wa kiserikali mara nyingi ndoa hizi hufungwa na wahusika wenye dini tofauti. Lakini kwa sheria ya Kiislamu ndoa hii ni batili.
Kwa bahati mbaya sana, wanaume wengi, huamua kuongeza mke bila kuangalia kipato halisi cha familia.
Matokeo yake ni kujenga chuki baina ya wanawake wale na hata watoto.
Hali ikiwa mbaya mke wa kwanza huweza kudai talaka na kuacha familia isambaratike, hasa kwa watoto atakaowaacha na hivyo kukosa mapenzi na huduma muhimu.
Ndio maana inashuhudia ongezeko la watoto wa mitaani ambao baadhi yao ni matokeo ya kusambaratika kwa familia.
Hatuwezi kupingana na vitabu vitakatifu vipi vinazungumzia kuhusu suala la ndoa ila ni wajibu wa akina baba kuhakikisha kuwa, yeye na familia yake wanajitosheleza na inabakia ziada ambayo ndio itatumika kuwasaidia wanawake wengine ambao unakusudia kuongeza.
Akina mama msiwe wachoyo. Kama familia zenu zinajiweza ni vyema mkawasitiri na wenzenu ili kuwaepusha na tamaa na vishawishi kama vile kufanya uasherati na kadhalika.
Si vizuri mwanamme kutoa talaka pasi na sababu ya msingi kama kuna jambo ambalo Mwenyezi Mungu Allah (s.w.) linamchukiza ni talaka. Mume huweza kutoa talaka ikiwa mke hazai. Anasahau kuwa tatizo hilo huweza kuwa la wote. Kama unajimudu oa mwingine upate mtoto au watoto na kumbuka watoto ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu.
Mume unapokuwa muadilifu hata chuki ndani ya familia huondoka na badala yake huwepo heshima, upendo na ushirikiano.
Mume unatakiwa uwe nguzo imara ya maelewano, baina ya wake zako ili wawe kitu kimoja na hata watoto wako wawe na upendo baina yao.
Ondoa tofauti ndogo ndogo ili mke mkubwa asione mwenziwe ni kero au karaha katika nyumba.
Ni vyema akina baba wenye uwezo kimaisha na kwa mujibu wa dini zenu mnaruhusiwa kuoa wake zaidi ya mmoja, mfanye hivyo kwa uadilifu mkubwa na muwe waangalifu na wakweli kwa wake zenu.
Mfanye vile sheria inavyotaka ili kuepuka matatizo kwenye familia zenu za awali. Kwani ni heri kuwa na wanawake uliowaoa kihalali na wanaotambulika kisheria kuliko kuwa na 'nyumba ndogo' ambazo kwanza ni kinyume na sheria za dini na vile vile hazileti picha nzuri machoni mwa jamii.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |