Eid Mubarak!
Ramadhani inakwisha, Eidi kukaribisha,
Ndugu kuwafuturisha, asubuhi na mchana,
Funga tunahitimisha, mafunzo kushikamana,
Karibu! Karibu sana! Karibu mapochopocho.
Tuwalishe maskini, wale ambacho hawana,
Wali ama biriani, na vinywaji kujichana,
Iwaondoke huzuni, wamtaje Sub-hana,
Karibu! Karibu sana! Karibu mapochopocho.
Tuwavishe masikini, wapendeze kujiona,
Watoto wa majirani, nguo wapate kushona,
Wafurahi mitaani, wacheke sio kununa,
Karibu! Karibu sana! Karibu mapochopocho.
Nguo ziwe za hijabu, atakazo Maulana,
Si vya utu kuharibu, visiketi vya kuchana,
Zikavuka taratibu, mwili vikaja kubana,
Karibu! Karibu sana! Karibu mapochopocho.
Ewe Eid Mubaraka, kwa mabibi na mabwana,
Akina dada na kaka, sote tukikumbukana,
Pongezi kuburudika, udugu kualikana,
Karibu! Karibu sana! Karibu mapochopocho.
Tuzipige takbira, mema tukaombeana,
Masikini mafukara, wote na kupongezana,
U-akbaru kabira, Allahu Mola Rabana,
Karibu! Karibu sana! Karibu mapochopocho.
Allahu Akbaru, Kabira wa Sub-hana,
Waswadaqa wa adahu, Chechnya wajahidina,
Washindishe washukuru, wanalia faizina
Karibu! Karibu sana! Karibu mapochopocho.
Na Al-Habib Al-Marddad,
Dar es Salaam.
Refaa!?
Kweli Rais Mkapa, usemavyo hutanii,
Madai tuliyokupa, katu hushughulikii,
Hayafai yakutupa, kwa Taifa na jamii,
Sawa sawa refarii, sie sio wananchi!
Wacha zifugwe nguruwe, kila pembe zitalii,
Mabucha tuongezewe, kwa zako zote bidii,
Makusudi wauziwe, wanetu hatuzuwii,
Sawa sawa refarii, sie sio wananchi!
Nguruwe ana thamani, sio sisi nchi hii,
Tumevishwa uhaini, vipigo haki tutii,
Makwetu Misikitini, twapigwa hutusikii,
Sawa sawa refarii, sie sio wananchi!
Waitika Vatikani, sisi hutuzingatii,
Yupo balozi nchini, vipi OIC,
Kupinga hatukuoni, kulikoni refarii,
Sawa sawa refarii, sie sio wananchi!
Ndiyo mana twauawa, sheria hufatilii,
Ukasema sawasawa, mauaji huchukii,
Na filimbi wachukuwa, wapuliza “pii pii”,
Sawa sawa refarii, sie sio wananchi!
Si kujenga wavuruga, tahadhari refarii,
Watu kuuwa kumwaga, damu hatukuridhii,
“Piga shaba” “yule piga”, ni haki hukumu
hii,
Sawa sawa refarii, sie sio wananchi!
Dikupa dikupatile Dikilema,
Dar es Salaam.
Nikichane?
Nilinunua kikadi, cha kijani rangi yake,
Lengo na langu kusudi, heshima nitambulike,
Vipi niitwe gaidi, udini wanipachike,
Jee, hiki kikadi, nichane nisikichane?
Haki zangu nikihoji, zile za kitabu chake,
Wanatumwa wanyongaji, na kunipiga mateke,
Katikati kwenye jiji, risasi nishambulike,
Jee, hiki kikadi, nichane nisikichane?
Kila nikifurukuta, mzalendo nisikike,
Hapo shutuma napata, eti nina peke peke,
Kwamba vurugu naleta, napigwa nihadhirike,
Jee, hiki kikadi, nichane nisikichane?
Ni kama vile kejeli, najibiwa kwa makeke,
Eti kipigo halali, kimya nisihuzunike,
Walouwa kikatili, si vyema wahukumike,
Jee, hiki kikadi, nichane nisikichane?
Vipi nilipie kodi, huku bado niteseke,
Kebehi zinavyozidi, nijikombe nipendeke,
Waziwazi makusudi, nidumu nidhalilike,
Jee, hiki kikadi, nichane nisikichane?
Awe mmoja kwanini, peke akubalike,
Mimi niitwe muhuni, bure nidharaulike,
Kikadi cha kazi gani, nikitunze kitunzike,
Jee, hiki kikadi, nichane nisikichane?
Ee jama mwanisikia, semeni nishaurike,
Mwenye hoja kuchangia, malenga nisiumbuke,
Kiko nimeshachukia, nikichane kichanike,
Jee, hiki kikadi, nichane nisikichane?
Idd Kikong’ona,
Morogoro.
Kwakheri Ramadhani
Namshukuru Manani, kwa zake nyingi rehema,
Kauleta Ramadhani, mwezi ulio na huruma,
Atujalie imani, tushikamane daima,
Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.
Karibu tena mwakani, kwaheri wende salama,
Yale tuloyatamani, tuyashike hima hima,
Yatufae duniani, na kesho huko kiama,
Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.
Tuyashike kwa yakini, yale tuliyoyasoma,
Athari iwe moyoni, mwili usende mrama,
Tutaingia motoni, na huku tunalalama,
Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.
Tuidumishe amani, maisha yawe salama,
Wabara na visiwani, sote ndugu Islama,
Tutende ya ihsani, tuyaache ya dhahama,
Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.
Swaumu ya Ramadhani, walifunga toka zama,
Wa huko Uarabuni, pia bandari salama,
Ikafika vijijini, hadi mjini Kigoma,
Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.
Kukesha Misikitini, kwa safu wamesimama,
Wakiomba Yamanani, atupe istikama,
Tujeingia peponi, waume kwa wanamama,
Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.
Tufate ya Ramadhani, maadili yalo mema,
Uislamu ndio dini, ubishi tuweke nyuma,
Tukiacha ya Qur’ani, tutaila michongoma,
Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.
Beti nane kituoni, kalamu imesimama,
Namuomba Rahamani, atupe zake karama,
Tuisimamishe dini, iende bila kukwama,
Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.
(Safarini Moshi kwa muda)
N.D. Abdulwahabu Y. Lesindilo,
Vivaha S.C. Ltd,
S.L.P. 1241,
(K.T.C) Chekereni,
MOSHI.
--
![]()
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |