Na Dkt. Abdallah J. Saffari (Wakili)
KUTOKANA na historia hii fupi ya mgogoro baina ya Chechnya na Urusi kwa takriban karne mbili zilizopita tunaelewa wazi kuwa watu hawa wa Chechnya wanataka kujiamulia mambo yao wenyewe. Haki hii inatambuliwa na sheria zote kuu za Kimataifa.
HATA hivyo, kuna masuala kadhaa ambayo ni muhimu kuyaangalia ili kupata mafunzo ya namna ya kutatua migogoro duniani na huu wa Chechnya. Kwanza, chanzo cha mgogoro huu wa sasa ni madai ya Urusi eti Chechnya inahusika na mauaji yaliyotokana na milipuko ya mabomu mjini Moscow kiasi cha miezi mitatu iliyopi.
Serikali ya Chechnya imekanusha jambo hili hivyo ni wajibu wa Urusi kuithibitishia dunia ushahidi kuhusumadai yao. Ushahidi huo umekuwa mgumu sana kuelezwa.
Pili, kuna matukio machache muhimu katika miaka hii ya karibuni ambayo inaifanya Urusi iwe na ghadhabu kiasi cha kuvionea vitaifa vidogo kama Chechnya.
Baada ya 'zawadi ya karne' waliyoitoa kwa Wamarekani tumeona mataifa mengi ndani ya Urusi yakijitangazia uhuru, hivyo kujitenga na utawala wa Urusi. Chechnya ndiyo taifa la karibuni kabisa kufanya hivyo. Na jimbo la Dagestan nalo likaanza jitihada za kutaka kujikwamua kutoka Urusi.
Hivyo, kabla ya vita hivi vya sasa baina ya Urusi na Chechnya, Urusi ilikuwa inapambana na wapiganaji wa Dagestan. Wapiganaji wengi wa jimbo la Dagestan kama vile Chechnya, ni Waislamu. Yumkini kutokana na sababu hii, na kwa vile Chechnya na Dagestan zinapakana basi Urusi ilidai mara nyingi tu kuwa Chechnya ilikuwa inawahifadhi 'magaidi' wa Dagestan. Chechnya ilikana vile vile madai hayo ya Urusi. Kwa hiyo matukio yote haya yakapandisha maya ya Urusi. Ikawa inatafuta kisingizio tu ili kuivamia tena Chechnya kama vile ilivyotokea 1994. Sababu ikapatikana pale Moscow ilipokumbwa na milipuko ya mabomu.
Lakini pia kuna jambo la tatu la kuzingatiwa kuhusiana na vita hivi vya sasa. Nalo ni namna ambayo Urusi, taifa kubwa lenye mirathi ya silaha nyingi za maangamizi, inavyoitwanga nchi hii ndogo usiku na mchana wakitumia ndege na makombora makubwa makubwa.
Halafu wameamua kufanya vita hivi wakati wa majira ya baridi kali. Maafa ya watu, mali na wanyama hayasemeki. Pamoja na maangamizi yote hayo, Warusi wanajidai kuwa wala hawajatumia nguvu nyingi, ama sivyo tayari wengekwisha uteka mji mkuu wa Chechnya, Grozny siku nyingi tu zilizopita.
Ajabu ni kuwa, kama ni rahisi kiasi hicho, basi wanasubiri nini? Ukweli ni kwamba majeshi ya Chechnya yameukilia kulitetea taifa lao hadi tone la mwisho la damu. Na taarifa za hivi karibuni zinaonyesha majeshi ya Urusi pia yanapoteza askari wengi labda kuliko walivyotarajia mwanzo wa kampeni yao ya maangamizi ikiongozwa na Waziri Mkuu wao.
Katika kadhia hii yote ni muhimu kuona unafiki wa Umoja wa Mataifa na mataifa makuu hususan Marekani, Uingereza na Ufaransa kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Chechnya.
Dhima ya Umoja wa Mataifa katika kuzuia maangamizi duniani imedhihirisha ubaguzi ima wa rangi, dini au itikadi. Hebu tuangalie mifano michache tu kukidhi haja yetu.
Kwanza, mnamo 1984 kulitokea mapigano makali katika mji uitwao Shatila nchini Lebanon. Hapo Shatila walikuwa wanaishi wakimbizi wa Kipalestina. Israeli ilionesha nia ya kupeleka jeshi kubwa kuivamia kambi hiyo kwa madai kuwa wakimbizi hao walikuwa wakivamia Israeli na kuua raia wake. Kwa bahati nzuri Umoja wa Mataifa ulipeleka majeshi ya kulinda amani eneo hilo.
Hali hiyo ikawazuia askari wa Israeli kuivamia kambi hiyo lakini, kwa aibu kubwa, bila ya sababu zozote za maana, Umoja wa Mataifa uliamua kuondoa jeshi lake la ulinzi huku wakijua fika janga ambalo lingetokea. Na kweli, kwa unyama, na ufidhuli majeshi ya Israeli yaliteketeza kila kitu katika kambi hiyo.
Mfano wa pili ni Rwanda. Mnamo 1993 kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwa Watutsi na Wahutu walijiandaa kuteketezana katika mauaj makuu (genocide). Umoja wa Mataifa ulipata taarifa hiyo. Tena mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kuhusu majanga wakati huo alikuwa Kofi Annan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa sasa.
Kilichotokea ni mtafaruku mtupu. Kwanza Ufaransa ilipeleka askari wachache kulinda amani halafu wakaondoka. Kisha Umoja wa Mataifa ukapaleka askari wachache kulinda amani halafu wakaondoka. Kisha Umoja wa Mataifa ukapeleka askari wachache mno ambao nao waliondolewa au walishindwa kabisa kuzuia mauaji makuu kuliko yote katika historia ya nchi hiyo ya Afrika.
Ndiyo maana Kofi Annan alipata mapokezi mabaya mno wakati alipozuru Rwanda mwaka jana. La ajabu ni kuwa badala ya kuomba radhi kwa kushindwa kuzuia au kupunguza janga la mauaji yale, alitoa sababu ambazo hazikuwa za kuridhisha hata kidogo.
Mfano wa tatu ni Bosnia Hecegovina. Mnamo 1992 Serbia wakisaidiwa na Milosovic wa Jamhuri ya zamani ya Yugoslavia walilivamia taifa changa la Bosnia Hecegovina ambalo lilijitenga kutoka Yugoslavia. Wakazi wengi wa taifa hilo ni Waislamu.
Licha ya kuwa taifa hili lilikuwa likiangamizwa katikati ya 'ustaarabu' wa Ulaya ya Magharibi, hakuna aliyethubutu kuwatetea watu wa taifa hilo kwa muda mrefu. Bila ya aibu yeyote, Michael Rifkind aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Uingereza katika serikali ya John Major ya Conservatives), alidai Uingereza haikuona haja ya kuingilia vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wakati huo alijua kuwa hivyo siyo kweli kwa vile Bosnia Hecegovina lilikuwa taifa huru. Hata Margareth Thatcher, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza kabla ya John Major, alisema sababu hizo ni upuuzi mtupu.
Margareth Thatcher aliwaeleza waandishi wa habari kuwa haikuwa sahihi kuzuia silaha zisiuzwe kwa Bosnia Hecegovina eti kupunguza umwagaji damu wakati Serbia ilirithi silaha kali kutoka Yugoslavia. Alitaka serikali yake kupinga maangamizi ya Bosnia na akaikumbusha namna Uingereza ilivyookolewa na majeshi ya Marekani dhidi ya Hitler katika vita vya pili vya dunia 1939 -44. Lakini Waingereza hawakumsikiliza Margeth Thatcher.
Hatimaye vita vya Bosnia vilimalizika hususan baada ya nchi hiyo kupata silaha nzuri kujitetea dhidi ya mashambulizi ya Serbia. Na kama ambavyo daima walisema, wao hawakuhitaji majeshi ya Umoja wa Maaifa kuwatetea, walichohitaji ni kuondolewa vikwazo vya silaha ili waweze kujitetea vizuri.
Umoja wa Mataifa huo huo ulishindwa hata kutoa kauli kuilaani Iraq ilipotumiwa na Marekani kuanzisha vita vikali vya miaka saba dhidi ya Iran.
Iko mifano mingi kuonesha ubaguzi na kutojali kwa mataifa makubwa na Umoja wa Mataifa katika kuzuia au walau kujaribu kupunguza maafa na maangamizi makubwa katika maeneo ya migogoro duniani. Lakini mataifa hayo hayo na Umoja wa Mataifa huo huo, kwa uwezo na ufanisi mkubwa viliweza kuingilia maangamizi Kuwait, Kosovo, Yugoslavia na hivi karibuni tu Timor ya Mashariki.
Hatuna haja ya kuzama katika mifano ya vita katika nchi hizo tatu kwa vile inafahamika kwa wengi. Ila kwa muhtasari tu ni kuwa Wamarekani walikuwa wananunua mafuta yote kutoka Kuwait kwa bei ya 'chee' kabisa. Hivyo hawakuwa tayari kuporwa uhondo huo na Saddam Hussein alipodai mgao wa mafuta hayo hayo.
Aidha, Saddam Hussein, kama vile Noriega wa Panama, alipokuwa hana manufaa tena kwa Marekani baada ya kutumiwa kupigana na Iran kwa zaidi ya miaka saba, sasa aligeuka 'nunda'. Aliitishia Israel ambayo ni sahibu na mshirika mkuu wa Marekani katika Mashariki ya Kati.
Wamarekani wakisaidiwa na mataifa yaliyokuwa na maslahi sawa nayo, kama vile Uingereza na Ufaransa, walihakikisha Iraq inatolewa nje ya Kuwait. Na baada ya hapo wakaendelea kudundwa katika nchi yao kama popo anayepopolewa kwa manati na kundi la watoto. Kana kwamba hiyo haitoshi, hadi leo bado wameiwekea nchi hiyo vikwazo vya uchumi visivyo na mwisho.
Suala la Timor ya Mashariki nalo limedhihirisha vile Umoja wa Mataifa na washirika wake wakuu (safari hii wakisaidiwa na Austalia) walivyojitoa kuwanusuru Wakatoliki wasitekeletezwe na Waislamu wa Indonesia.
Mwisho, Kosovo. Jimbo la Kosovo ni sehemu ya Serbia ambayo lilikusudia kujitenga kutoka nchi hiyo. Raia wengi wa jimbo hilo walikuwa Waislamu wenye mnasaba na Albania. Kwa azma dhahiri ya kutaka kuwateketeza watu wa jimbo hilo, Rais wa Serbia, Milosovic, alipeleka majeshi ya maangamizi ya nchi yake katika jimbo hilo.
Kwa sauti za mbali, Umoja wa Mataifa na washirika wake wakuu wakaanza kulaani kitendo cha uvamizi wa kijeshi wa jimbo hilo. Lakini baadaye Marekani na Uingereza wakaonesha dalili za kutaka kusuluhisha mgogoro huo nje ya Umoja wa Mataifa kinyume na vile walivyofanya katika vita vya Ghuba dhidi ya Iraq.
Itakumbukwa wakati wa vita vya Iraq mataifa hayo makubwa yalitumia mwamvuli wa Umoja wa Mataifa kuikomboa Kuwait na kuiangamiza Iraq. Safari hii mataifa hayo hayakuwa na subira tena. Kwa nini? Sababu za Wamarekani na sahibu zake wakuu hususan Uingereza kuhemkwa na kutaka kuwasaidia Waislamu wa Kosovo sio huruma kama ambavyo makala katika gazeti hili la AN-NUUR yalivyofafanua vizuri kabisa. 'Huruma' ilikuwa ni geresha tu. Mataifa hayo yalipata kisingizio ha kumkomoa hasimu wao wa muda mrefu na tishio katika Ulaya kwa wakati ule. Maana baada ya kusambaratika kwa sera za Kikomunisti nchini Urusi, Taifa la Yugoslavia na baadaye Serbia, chini ya Milosovic ndilo pekee katika Ulaya lilikuwa linafuata sera za Kikomunisti (japo kwa maneno matupu!). Kwa hiyo wakati Wamarekani walipojidai kuwahasa Warusi waache kuwaangamiza Wachechen, Urusi ikatamka kuwa mbona wao Wamarekani na Waingereza walimchapa Milosovic bila aibu wala imani!
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |