Vita vya Chechnya:

Maofisa wa Russia wakanusha taarifa za wakuu wao


MMOJA wa makamanda wanaoongoza jeshi la Russia amesema taarifa zinazotolewa na wasemaji wa serikali ni kinyume na ukweli ulivyo katika uwanja wa mapambano nchini Chechnya.

Kamanda huyo alikuwa akikanusha taarifa kwamba vikosi vya Russia vimefanikiwa kujipenyeza katika mitaa ya Grozny na kwamba katika kipindi cha masaa 24 majeshi hayo yamefanikiwa kuua zaidi ya wapiganaji 160 wa Chechnya.

Amesema taarifa za Moscow zimeongezwa chumvi tofauti na ilivyoripotiwa kutoka uwanja wa mapambano hata hivyo kamanda huyo amedai majeshi yake yanasonga mbele kwa tahadhari kubwa kuelekea Grozny ingawa wanakumbana na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa kichechen waliojizatiti kuulinda mji huo.

" Vita ni vita huwezi kujua kwa uhakika lile litakalotokea", alisema kamanda huyo wakati akihojiwa na moja ya mashirika ya habari jana.

Mapigano makali yangali yanaendelea ambapo katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita habari kutoka uwanja wa mapambano zinafahamisha kuwa kumekuwa na majeruhi wengi pande zote huku maiti nyingi za wanajeshi wa Russia zikiwa zimezagaa kufuatia jaribio lao la kujipenyeza katika mji wa Grozny.

Mjini Ingushetia habari zinaeleza kuwa wakimbizi wa Chechnya wamefanya maandamano makubwa kuilaani Russia huku wakiitaka jumuiya ya kimataifa kuelekeza misaada ya kibinaadamu nchini humo.

Baadhi ya watu waliotoa maoni yao jana kupitia kituo cha CCN, wamelaani uvamizi wa Russia kwa kuuita ni unyama usiotakiwa kuwepo katika Millenia hii mpya ya ustaarabu.

Wakati huo huo, Mmoja wa makamanda wakuu wa Russia General Mikhael ameripotiwa kupotea baada ya mapigano makali ya milimani nje ya mji wa Grozny.

Wapiganaji wa Chechnya wamesema wamemteka Kamanda huyo na hivi sasa yuko chini ya himaya yao.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook