Mnakataa nini Waislamu wanapodai wanadhulumiwa


Na Mussa Ally, Morogoro


UISLAMU kama ulivyo, hausimami wala kutajwa baada ya jina la mtu kama ilivyo kwa Ukristo ambao husimama na kutajwa baada ya neno au jina la "Yesu" (Issa a.s.), Ubudha baada ya Sindhatha Budha, Ujmaa baada ya Karl Marx na kadhalika.
 

HALIKADHALIKA Uislamu haupo kulidhamini kabila fulani kama ilivyo Uyahudi kwa Wayahudi, Uhindi kwa Wahindi au Olapa kwa wamasai na kadhalika.

Bali Uislamu kama ulivyo na kama unavyojieleza wenyewe ni mfumo sahihi na kamili wa maisha ambao Allah (s.w.) amewawekea wanadamu kuufuata ili kufuzu katika maisha yao mafupi hapa duniani na ya milele kesho akhera.

Wala mfumo huu si mpya ulioshushwa kwa "Waarabu" karne ya saba kama maadui wa Uislamu wanavyodai , bali ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu tangu mwanzo (Nabii Adam a.s.) hadi kizazi cha mwisho.

Mfumo huu kamilifu na halisi wa maisha ndiyo pekee unaotambulika na Mwenyezi Mungu kwani yeye ndio aliouchagua kama nilivyosema kabla na hakuna mfumo mwingine wowote ule atakaoukubali au anaoukubali au alioukubali kinyume na huo. Rejea Qur'an 5:3, 3:85 na 3:67.

Baada ya darsa hilo fupi sana, hebu nirejee katika somo nililoliainisha hapo juu. Ni hivi majuzi tu Waislamu wamepokea kile kilichotafsiriwa na wengi kuwa "Decration of war" au tangazo la vita la serikali dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini.

Pamoja na mengi mengineyo Mheshimiwa Rais pia alitumia fursa hiyo ya majibu yake yasiyoridhisha kabisa kwa umma wa Kiislamu nchini kushambulia Shura ya Maimamu inayoongozwa na Sheikh Juma Mbukuzi kuwa ni kikundi kidogo cha watu kinachochochea vurugu na kuwataka Waislamu wawanyime majukwaa.

Lazima ieleweke wazi kuwa Uislamu kama nilivyotangulia kusema si dini iliyobuniwa na mtu au watu, hivyo si dini iliyobuniwa na Mbukuzi wala Shura anayoiongoza.

Anachofanya Sheikh Mbukuzi na Shura hiyo iliyochaguliwa na Waislamu kuongoza njia ni kutafsiri Qur'an katika vitendo na si vinginevyo.

Qur'an imeharamisha kudhulumu (dhulma) hivyo Waislamu wamekatazwa kabisa si tu kudhulumu bali hata kukubali kudhulumiwa au kuacha mwingine adhulumu au adhulumiwe.

Waislamu nchini wamedhulumiwa haki zao za msingi na serikali ya CCM. Na walipotoa madai yao pamoja na vielelezo stahiki kuthibitisha dhulma hiyo kwa mamlaka husika, bila ya kuona haya mamlaka yalitoa majibu yanayoashiria 'shari' kwa kundi moja la raia halali wa nchi hii.

Mbali na hapo, wale waliosimama kidete kuweka wazi dhulma hiyo na vielelezo husika walionekana maadui na mamlaka hiyo, hapo panatoa picha nyingine mpya ambayo haikufahamika kabla, picha ambayo si tu inachekesha bali pia inashangaza na kuhuzunisha umma wa wapenda amani, utulivu, mshikamano na maendeleo nchini.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook