Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC-USA
MUHESHIMIWA Rais Benjamin William Mkapa katika barua yake ya Desemba 1999 aliyoipeleka kwa Halmashauri Kuu ya Waislamu, kama majibu ya barua yao yaliyoorodhesha malalamiko ya Waislamu, pamoja na mambo mengine, amesema kwamba kubakia nyuma kwa Waislamu katika kunufaishwa na ulaji wa keki ya uhuru, kumesababishwa na sababu za kihistoria.
Katika sababu hizo za kihistoria, mojawapo ni ukosefu wa elimu ya kutosha kuwawezesha Waislamu kushika nafasi za uongozi wa kitaifa kwa uwiano wa idadi yao ili kuweza kupanga mipango ya maendeleo ya nchi na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake. Wenzetu wasiokuwa Waislamu wamezishika nafasi hizo kwa wingi kwa ajili ya elimu zao, uzoefu na umahiri wao.
Tunapozungumzia suala la dini nchini Tanzania, tunazungumzia kati ya Ukristo na Uislamu bila ya kujali madhehebu. Dini hizi mbili ndizo zenye wafuasi wengi na ndizo zenye mvutano mkubwa tangu zilipokutanishwa nchini mwetu.
Uislamu ndio uliotufikia mwanzo nchini. Waarabu walitufikia mwanzo. Shughuli yao kubwa ni kutangaza dini wala haikuwa kututawala. Hii inaonekana kwa kuwa walitosheka na visiwa vya Zanzibar na Pemba, pamoja na Ukanda wa Pwani wa Kenya na Tanganyika. Shughuli zilizowapeleka ndani zaidi ya nchi zilikuwa za kibishara ya pembe za ndovu na biashara ya watumwa ambayo waliisitawisha sana bila ya uchu wa ardhi ya kuitawala.
Katika karne iliyopita ndio tukafikiwa na wazungu. Hawa Mzee Jomo Kenyatta alisema, walikuja na Biblia katika mkono mmoja na ule wa pili wakawa na bunduki. Wakatuambia tufumbe macho tuombe. Tulipofumbua macho, ardhi yote wameichukua.
Wao waliisitawisha sana na kuidumisha biashara ya watumwa kule kwa wenzetu wa Afrika ya Magharibi. Wao walikuwa na uchu mwingi wa kufanya biashara, kueneza dini ya Kikristo, kutafuta ardhi na watu wa kuwatawala kwa ajili ya kupanua na kukuza himaya zao.
Kule Afrika ya magharibi walichukua watumwa wakawapeleka nje ya Afrika. Huku kwetu wakatufanya watumwa ndani ya nchi yetu wenyewe. Mpaka hii leo tunaendelea kuwa watumwa wao wa akili na uchumi, ingawa tunaona vibaya kukiri hivyo. Lakini ukweli siku zote unabaki pale pale.
Mvutano na chuki kati ya Uislamu na Ukristo tulipandikizwa pale ilipowawia vigumu wakoloni wamishonari wa Kikristo waliposhindwa kuueneza Ukristo katika maeneo ambayo Uislamu ulikuwa umekwisha jizatiti. Zikaanza kubuniwa mbinu za kuupiga vita Uislamu na Waislamu wenyewe ili nafasi itakayobaki wazi ijazwe na Ukristo. Mbinu hizo tangu zinaendelezwa mpaka hii leo kidhahiri na kisirisiri.
Elimu ni ufunguo wa mambo yote. Ukinyimwa elimu basi ujue umedhulumiwa kiasi ambacho mfanowe haukadiri. Sasa mpango ukawa kujenga makanisa, shule na dispensari. Ukitaka dawa au elimu ni lazima kwanza uwe Mkristo. Katika kuendesha makanisa, shule na dispensari serikali ililazimika kutoa ruzuku. Ruzuku hii ilitokana na kodi za wananchi bila kujali kuwa mlipa kodi alikuwa Mkristo au Muislamu.
Hapana shaka yoyote kuwa Waislamu walishindwa kuacha itikadi yao juu ya Mola wao kwa ajili ya mtego wa elimu na dawa. Ilikuwa lazima wategemee shule na hospitali za serikali ambazo zilikuwa chache. Wenzetu Wakristo walikuwa na hiari ya kwenda shule zozote walizozitaka. Hali kadhalika na hospitali. Ni dhahiri kuwa wengi wao walinufaika na vyote na kwa wingi kuliko Waislamu.
Serikali ilikuwa ya Wakoloni Wakristo na shule za serikali kwa hiyo zilijaa waalimu wa Kikristo na ziliendeshwa katika mitindo ya Kikristo Kikristo. Hili hii ikawawia ngumu kwa wazazi wengi wa Kiislamu kuwapeleka watoto wao humo. Hali hii ikazidi kutukandamiza kielimu Waislamu. Labda hizi ndizo sababu za kihistoria zinazolengwa na Muheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa.
Kama kweli hii ndiyo sababu inayotuletea Waislamu kuikosa keki ya uhuru, tungependa kujua katika hii miaka 40 ya uhuru ya kujitawala wenyewe, serikali yetu ilipanga mikakati gani ya kutuondoa ndugu zao kutoka hali ya unyonge wa kukosa elimu? Kama serikali yetu ilifanya hivyo mbona mpaka hii leo tunaambiwa bado hatuna elimu ya kutosha kula keki ya uhuru? Bado tunasota pale pale alipotuacha mkoloni. Lazima pana mkono wa mtu hapa unaoendesha dhulma hii.
Nilipokuwa mtoto mdogo mjini Dar es Salaam, shule za serikali kwa ajili ya watoto wa Kiafrika zilikuwa Mchikichini Primary School na Kitchwere Streets Boys' Secondary School kwa ajili ya wavulana na kwa wasichana ilikuwa shule moja tu ya Msimbazi Street Girls Primary School. Hizo ndio shule pekee watoto wa Kiislamu na Kikristo wa Dar es Salaam tuliweza kwenda kusoma.
Lakini wenzetu wa Kikristo walikuwa na shule pale Msimbazi RC Mission, pale Forodhani na kule Pugu na Kisarawe. Hali hii ilifanya watoto wa Kiislamu tuwe wengi zaidi kwa idadi katika shule za kiserikali na isitoshe wingi wetu ulisababishwa na ukweli kwamba wazazi wa mwambao wengi walikuwa ni Waislamu.
Mfumo wakati ule ulikuwa Primary School, darasa la kwanza mpaka la nne; Secondary School, darasa la tano mpaka la kumi na Senior Secondary School, darasa la kumi na moja mpaka la kumi na mbili. Senior Secondary School iliyokuwa wazi kwa watoto wa Kiislamu ilikuwa moja tu kwa nchi nzima, nayo ni ile ya Tabora peke yake. Na hata humo wengi wa wanafunzi walikuwa Wakristo.
Mchikichini kila darasa lilikuwa na mikondo mitatu na kila mkondo ulikuwa na wanafunzi 30. Pale Kitchwele darasa la 5 na 6 kila mmoja na mikondo mitatu ya wanafunzi 30 kila moja. Darasa la 7 mpaka la 10 yalikuwa na mikondo miwili miwili pia idadi ya wanafunzi ilikuwa haizidi 30 kama siyo chini yake.
Wakati huo ulikuwa huwezi kupandishwa darasa lolote mpaka upasi mtihani wa darasa. Ukifika darasa la nne kulikuwa na mtihani wa wilaya nzima ya Uzaramo kugombea nafasi zile 30 za pale Kitchwele. Darasa la sita kulikuwa na mtihani wa jimbo zima la mashariki kuwania nafasi zile 60 za pale Kitchwele, maana hiyo ndiyo ilikuwa shule ya sekondari pekee kwa jimbo zima.
Kwa kuwa nilikuwa mtoto mdogo wakati ule sikuelewa kuwa kulikuwa na mbinu na njama za kuwadhulumu elimu Waislamu. Hivi leo nikitazama nyuma na kutafakari ndio naelewa nini kilikuwa kinafanyika.
Nilianza kusoma Mchikichini 1944 nikiwa na miaka 9. Kwa siku hizo nilihesabika kuwa nilianza mapema sana maana umri wa kuanza shule ulikuwa miaka 12. Katika mikondo yote mitatu tulikuwa 90. Wanafunzi wa Kiislamu tulikuwa kati ya asilimia 60 na 75. Sababu ya kuwa wengi hivyo ilikuwa ni ya kihistoria. Wakazi wengi wa Dar es Salaam wengi ni Waislamu na Mchikichini ndiyo shule pekee iliyokuwa wazi kwa watoto wao.
Idadi yetu ilipungua baada ya mchujo wa darasa la 4 mwishoni mwa 1947. Lakini asilimia ya watoto wa Kiislamu haikubadilika kwa kuwa walipatikana wanafunzi wengine kutoka shule zingine za Uzaramoni kuingia darasa la 5 pale Kitchwele.
Maajabu yalitokea katika mchujo wa darasa la 6 mwaka 1949. Mwaka huo Headmaster alikuwa Mr. Mundy kutoka katika shule ya Kikristo kule Bukoba. Kati ya wanafunzi 90 wa Kitchwele, 30 wa Bagamoyo, 30 wa Morogoro, 30 wa Rufiji, 30 wa Kilosa na 30 wa Ulanga ambao tulikuwa tunagombea nafasi 60 za darasa la 7 pale Kitchwele ni wanafunzi 24 tu ndio tuliobahatika kupewa nafasi. Na hao ilikuwa mchanganyiko wa Waislamu na Wakristo.
Sasa jiulize mwenyewe watoto wangapi wa Kiislamu walikoseshwa nafasi ya kuendelea na masomo? Maana wao ndio idadi yao ilikuwa zaidi. Katika hao walionyimwa nafasi, mmoja wao aliyesemekana kuwa ndiye aliyekuwa wa kwanza kwa kufanya vizuri katika mtihani huo, alikuwa ni Maliki Kibwana Chanzi anayeishi mtaa wa Lindi hapo jijini.
Akaambiwa hawezi kuendelea kwa kuwa alikuwa na kimo kirefu na anaonekana kuwa ni mkubwa sana kupita wenzake. Hii siyo dhulma? Kuna anayejua huyu jamaa hii leo angekuwa nani nchini mwetu kama angepewa nafasi ile?
Tazama sasa, kwa kuwa darasa la 7 lilikuwa na nafasi 60 na zilizojazwa zilikuwa 24 tu, mpango ulifanyika pakaletwa watoto 36 kutoka Songea kuja kujaza nafasi hizo. Kati ya hao 36 wanafunzi 5 tu ndio walikuwa Waislamu, lakini 31 waliobaki wote walikuwa Wakristo.
Mara moja katika shule ya sekondari ya Jimbo la Mashariki nchini Tanganyika ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu, kumekuwa na wanafunzi wengi Wakristo kuliko Waislamu. Tutakosaje kuwa wengi wetu hawakusoma? Serikali ilikuwa ni ya wakoloni Wakristo na wakoloni Wamishonari waliokuwa wakiupiga vita Uislamu na Waislamu walikuwa na mshikamano wa kuwadhulumu Waislamu.
Naona vigumu kuamini kuwa msimamo huo haukujiendeleza mpaka hii leo. Kama sivyo kwa nini mpaka hii leo, baada ya miaka 40 ya uhuru wetu na kujitawala wenyewe bado Waislamu pamoja na mambo mengine, wanalalamika kudhulumiwa kielimu.
Sizungumzii haya yote kwa ajili ya kuleta mfarakano na chuki kati ya Waislamu na wanacchi wenzetu wasiokuwa Waislamu, bali niko katika jitihada za kuichambua serikali yetu mtazamo wa Waislamu kuhusu suala la elimu na yote mengine yale tunayoyalalamika.
Ni ukweli usiopingika kuwa serikali yetu hivi sasa imeshikwa na ndugu zetu Wakristo katika nafasi zote muhimu na kwa kuwa hatuoni mikakati wala jitihada za makusudi za kuwaondolea Waislamu matatizo yao wanayo yalalamikia, hasa katika nyanja ya elimu, ambao ndiyo ufunguo, tutakuwa na mtazamo upi mwingine?
Isitoshe ni dhahiri hata kwa kipofu asiyekuwa na elimu kuwa wapo Waislamu, tena wengi wa kutosha wenye elimu za juu, wenye ujuzi tosha, uzoefu bora na umahiri wa kubobea ambao hawakaribishwi katika meza ya keki ya uhuru kwa ajili ya itikadi zao za kiroho. Siasa kali na Mujahidina ndiyo sifa wanazopewa kwa kebehi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |