MWENYEZI Mungu amekataza jimai nje ya ndoa, lakini katika jamii yetu ya Tanzania ngono nje ya ndoa imefanywa kuwa fasheni. Watoto wanaozaliwa wamekuwa wakikumbana na matatizo mbalimbali. Mwandishi Maulid Ahmed wa TSJ anaelezea matatizo hayo katika makala hii.
WEWE mtoto wa haramu, ondoka hapa, huna chako, hutambuliki katika familia hii, nenda kwa huyo mama yako mzinifu mkubwa, baba angekuwa hai ndie angekujali sio mimi.
Haya ni baadhi tu kati ya majibu wanayopewa watoto wanaozaliwa nje ya ndoa wakati wanapojaribu kudai haki zao kutoka ndugu zao wasio wa tumbo moja au mama zao wa kambo.
Watoto wa nje ya ndoa daima hutaraji kupatiwa mahitaji yao ya kila siku kama watoto wengine lakini badala yake hujikuta wakiambulia matusi na majibu mengine mabaya yasiyofaa.
Kijana Bakari Musa alikumbana na matatizo hayo. Ameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa ada ya shule kabla ya hapo baba yake alimfukuza mama yake na hivyo kufanya maisha kuwa magumu na kushindwa kumlipia ada.
"Imenibidi kwenda kufanya kazi za ndani (Houseboy) ili niweze kupata angalau fedha kidogo za kuendesha maisha na kumsaidia mama yangu pamoja na wadogo zangu", anasema kijana Bakari.
Kijana mwingine Somoe Juma, amepata jeraha kubwa baada ya kumwagiwa maji ya moto kwenye mgongo alipoenda kudai urithi wa baba yake kwa mama wake wa kambo.
"Sikutarajia kama ningekuwa hai mpaka leo, nilidhani ningekufa kwa kitendo cha mama yangu wa kambo alivyonifanyia", anasema Somoe.
Hiyo ni mifano midogo ya baadhi ya matatizo ambayo watoto wanaozaliwa nje ya ndoa hukumbuna nayo ingawa makosa ni ya wazazi wao.
Watoto wa nje ya ndoa (watoto wa haramu) wanatokana na wazazi kufanya uzinifu au kufanya mapenzi kabla ya kuoa au kuolewa.
Katika Uislamu, mwanamke au mwanaume haruhusiwi kufanya mapenzi ikiwa hajaolewa au kuoa (kuzini) na kufanya hivyo ni dhambi kubwa.
Kwa mujibu wa sheria za Kiislamu mtu yeyote anayezini achapwe mijeledi 100 hadharani aadhibiwe kwa kupigwa mawe.
Kwa hakika adhabu hii ni nzuri kwani inazuia uzinifu na kuzuia uzinifu ni kuzuia watoto wa nje ya ndoa na pia magonjwa mbalimbali.
Katika jamii yetu ya sasa ya Tanzania kuzaa watoto nje ya ndoa imekuwa kama kitu cha kawaida, watu wamekuwa hawajali maisha ya baadaye ya watoto wao na pia kutojali makatazo ya dini ya Kiislamu.
Bi Maftaha Abdulsalami mwenye umri wa miaka 62 anasema: " Sisi zamani tulikuwa tunaogopa kuzaa haramu, tukiona aibu na kama bahati mbaya umezaa basi mtoto hufichwa".
Nae Bi Rukia Ahmed anasema: "Watot wa siku hizi hawaogopi na hawana maadili ya Uislamu, wanaona ufahari kuzaa nje ya ndoa".
Bi Khadija Kijakazi anasema ilikuwa fahari kubwa kuolewa ukiwa Bikra.
Mzee Idd akizungumzia tabia zao enzi hizo anasema ilikuwa desturi ya wakati wao mwanaume kuijua ngoni siku ya harusi.
Mtoto yeyote huhitaji mapenzi ya wazazi wawili. Kwa kawaida mtoto wa kiume hupenda kuiga tabia ya baba na wa kike huiga ya mama, kwa kumkosa mzazi mmoja wao kunamfanya mtoto awe na upungufu fulani.
Sio hivyo tu, bali pia kumkosa mzazi mmoja kunamfanya mtoto asiwe na adabu kwani mara nyingi mzazi mmoja huogopwa zaidi hasa baba huogopewa na kwa kutokuwepo baba katika familia hiyo mtoto hufanya maovu na utundu wa hali ya juu.
Watoto kuwepo katika familia ya wazazi wote wawili inawafanya wawe na furaha, heshima na huweza kujisomea wakiwa wametulia akili zao.
Mara nyingi watoto wa nje ya ndoa huharibika kisaikolojia. Huweza kufikia kipindi fulani kuacha kufikiria mambo ya maendeleo na badala yake kufikiria jinsi ya kuepukana na karaha za watu fulani.
Bw. Epaphras Tenganamba ambae ni mwanafalsafa na ni mwandishi wa habari anasema kuwa mara nyingi mtoto wa aina hiyo huamua kuoa au kuolewa mapema iwezekanavyo ili kuondoa mawazo aliyokuwa nayo.
Wengi wao hudhani ili kuondoa mawazo kuwa hawana wazazi huamua kuoa au kuolewa mapema. Wake na waume zao huwa ndio wazazi wao katika walichobaki nacho cha maisha yao", anasema Bw. Epaphrasi.
Nae Mwanasaikolojia wa Kimarekani Nicolas Zill anasema kuwa watoto wengi wanaozaliwa nje ya ndoa wanapata matatizo na wanashindwa kuendelea kutokana na kuharibika kisaikolojia.
Zill anasema watoto wengi waliozaliwa nje ya ndoa wanaongoza kwa vitendo vya uhalifu kama wizi na utoaji mimba.
Watoto hawa huwa ni rahisi kutumika katika kufundishwa mambo ya kijeshi na watu wenye nia mbaya na baadaye kutumika katika kupigana dhidi ya serikali kama waasi.
Utumikaji wa watoto katika uasi umejidhihirisha wazi katika nchi nyingi za Kiafrika kama Liberia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Bi Irandukunda Godeberthe ambae alishuhudia vita vya Burundi anasema: "Watoto wadogo wengi chini ya umri wa miaka 17 hujiingiza katika jeshi la waasi na tena huwa wakatili sana, huua bila huruma".
Pia wengi wa watoto hawa hujikuta katika ajira ya watoto. Katika migodi hutumika kama wasaidizi kwa kuchota mchanga pia kuwapikia wachimbaji.
Kuna baadhi ya mila potofu hapa nchini zinazohalalisha wazazi kuwa na watoto wa nje ya ndoa. Mfano ni Wamasai ambao ni lazima kuzaa nje ya ndoa ambapo mtoto huyo huitwa SAITOKI.
"Kwetu Arusha ni lazima kijana wa Kimasai azae nje ya ndoa. Sababu kubwa ni kukinusuru kizazi chake kisipatwe na mikosi inayoweza kutokea katika familia kama laana inayotokana na vitu hivyo", anasema Deogratius Uvetie.
Ni makabila machache yanayokubali watoto wa nje ya ndoa tofauti na ilivyo kwa Wamasai. Hata hivyo makabila mengine huangalia maslahi tu.
Wakurya, Wamasai, Wabargaig na Wasukuma hutumia watoto wao wa kike kama chombo cha kujinufaisha kiuchumi kwa kujipatia ng'ombe.
"Sisi hatujali kama mtoto wa kike halali au haramu, mradi tu anatupatia ng'ombe ni muhimu kwetu", anasema Simon Chacha mzee wa Kikurya.
Kwa upande wa dini ya Kiislamu na Kikristo watoto hawa hawatambuliki kwani katika Uislamu watoto hawa hawapati urithi wa baba yao na Wakristo hawabatizwi.
Kwa upande mwengine sheria za nchi hazijabainisha iwapo mtoto wa nje ya ndoa anaruhusiwa au haruhusiwi kurithi. Sheria hiyo inasema kuwa mtoto huyo hataruhusiwa kurithi kama atakuwa hajaandikwa katika mirathi ya marehemu.
Kwa maana hiyo sheria za nchi zinaonesha kuwa mtoto wa nje ya ndoa hawezi kurithi ingawa haijasema kwa uwazi, kwani mtoto wa ndoa awe ameandikwa kwenye mirathi au hajaandikiwa ni lazima tu atarithi, sasa iweje kwa mtoto wa nje ya ndoa mpaka aandikwe? Hiyo inaonesha kuwa mtoto wa nje ya ndoa harithi.
Je, mzazi kwa nini uzae kiumbe ambacho hakitambuliki kidini wala kijamii? Na ambae atapata matatizo duniani?
"Mtoto wa haramu hata ukimtia kwenye chupa lazima atatoa kidole juu, ni lazima mtoto huyo atapata matatizo tu, njia ya kuepuka ni kutozini", anasema Bi Rukia Ahmed.
Kutokana na tatizo hili, hatuna budi kujenga tabia ya kuheshimu ndoa zenu na vijana kujiheshimu kwa kuacha kufanya zinaa na wasubiri mpaka wakati wa ndoa ili watoto wao wapate mapenzi na haki wanazostahiki na kuepuka matatizo haya.
Tatizo hili litaondoka iwapo tu sheria ya
dini ya Kiislamu itafuatwa kwa wale wote wanaoonekana wanazini kuadhibiwa,
watu hawatazini na jamii itakuwa yenye maadili na adabu na watoto wa nje
ya ndoa hawatakuwepo.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |