Maoni Yetu


Watanzania tuinusuru nchi

MAKABURU wa Afrika Kusini waliweka siasa yao ya ubaguzi wa rangi na ili kuidumisha ikawa ni lazima waongeze ukandamizaji juu ya ukandamizaji.

Wakawafunga Waafrika, kuwatesa na kuwaua ovyo. Hayo yote yalifanyika kwa sababu makaburu hawakuwa na njia nyingine kuihami siasa yao iliyokuwa ikipingwa na wananchi walio wengi.

Hata hivyo ilifika mahali Makaburu wakatanabahi kwamba udhalimu juu ya udhalimu hauleti ufumbuzi wala propaganda za kuwaita wapigania haki kwamba ni wahaini hazina tija.

Walitulizana na busara zao wakaangalia maslahi ya nchi. Sasa wao na Waafrika wanaishi kwa salama na amani.

Wahutu na Watutsi hawakujifunza; halikadhalika Wakristo na Waislamu wa Lebanon hawakujifunza.

Matokeo yake tunayajua, si jambo la kuhitaji utafiti au simulizi zaidi. Yaelekea Wakatoliki na Waanglikana huko Ireland ndio kwanza wanaanza kuzinduka baada ya Darsa iliyowagharimu roho nyingi za watu na mali.

Ukizungumzia madhila ya Watanzania waliofanyiwa na wakoloni, zaidi ya asilimia hamsini (50%) ya Watanzania hawakuelewi, wanachoelewa zaidi ni athari za "operesheni vijiji vya ujamaa. Azimio la Arusha, Siasa ni Kilimo, operesheni wahujumu uchumi, utaifishaji wa majumba, vita vya Kagera, maduka ya kaya", na kadhalika.

Haya ukiwauliza wanaweza kueleza hasara zake na faida zake kama zilikuwepo. Habari za wakoloni hawawezi kuzielewa; kwa sababu hawakushuhudia madhila yale lakini pia hao wakoloni wenyewe leo hawapo.

Aidha, wananchi leo hawaelewi kitu ila kwamba wao wamenyimwa elimu na matokeo yake wamekuwa wazamiaji, vibaka na wapaa samaki Feri. Hunyimwa vyeo na madaraka japo wamesoma na ndio maana hawaonekani. Si kwenye serikali wala mashirika ya umma!

Hawaelewi kitu zaidi kwamba wao ni watu wa kudhulumiwa na kuvamiwa na kupigwa Misikitini. Kwao, Misikiti yao hunajisiwa na polisi, dada na mama zao kudhalilishwa! Wanaowaua hupongezwa.

Wananchi hawa uonevu wa mkoloni hawauelewi kwani ama walikuwa hawajazaliwa au walikuwa watoto.

Katika kipindi cha mwaka 1963/64, historia ilishuhudia Masheikh wakifungwa, kutishwa na kufukuzwa nchini. Mwaka 1968 Jumuiya za Waislamu zikavunjwa na kuundwa jumuiya ambalo si lao na wasilolitaka. Umoja wa Waislamu ukasambaratishwa na mahusiano yao na Waislamu wenzao wa nje yakafungiwa milango. Huku Maaskofu na wafadhili wao kutoka nje wakifunguliwa milango zaidi.

Watu ambao hawakushuhudia udhalimu ule waweza kusema kuwa si mambo yaliyo na uthibitisho wa kisayansi.

Lakini miaka thelathini baadaye yale yale yamejirudia kuwatoa wasiwasi wale waliokuwa hawakuyashuhudia ya mwaka 1963/64 na 1968.

Mwaka 1993 Masheikh walifungwa na kudhalilishwa bila ya sababu yoyote ya msingi, wengine wamewekwa rumande kukosa matibabu na hawakudumu tena baada ya wenye kauli kukinai kuwaweka rumande. Misikiti ilipigwa mabomu na watu kujeruhiwa nani ya Msikiti.

Huko nyuma Waislamu na Wakristo walikuwa wanasilimishana na kubatizana. Leo ni suala la polisi na Mahakama kumkamata na kumhukumu mtu anaposhitakiwa na Jamhuri kwa kusema Yesu si Mungu.

Kwa mara kwanza Waislamu wanauliwa hadharani kwa kulengwa shabaha. Na waliopatia "target" wanapongezwa huku sheria ikikandamizwa wauaji wasifikishwe mahakamani.

Hatujui wanaodai ushahidi na utafiti wa kisayansi wanakusudia sayansi gani. Au neno hili ni tata lenye tafsiri nyingi kutokana na hisia za mtu!

Hofu yetu ni kuwa miaka 30 ijayo yapi yatatokea yatakayowathibitishia watoto na wajukuu wetu kwamba hayo yalitokea mwaka 1998! Lakini kwa hakika mwenye busara zake asiyeongozwa na jazba, chuki zisizo za misingi wala ile za sera za Kanisa kuwaona wengine kuwa watu wasiofaa, ndivyo anavyoeleza Padri Crane katika Sivalon kwamba:

"Tatizo la Afrika ni kwamba watu wasiofaa wamewekwa katika nafasi za utawala. Tutaweza vipi kuweka watu wanaostahili katika nafasi hizi? Lazima tujitahidi kadiri ya uwezo wetu kupata wasomi Wakatoliki ambao watashika nafasi muhimu kwenye ngazi zote za kijamii. Wakatoliki wetu Walei wajitahidi kushika nafasi hizi. Tutaweza kuwaingiza kwenye nafasi hizi za uongozi kwa njia ya kujenga vikundi vidogo vidogo vya wasomi Wakatoliki..." (uk. 23).

Hali hii ni ya kutisha. Tuna kizazi hapa hakijui kitu ila ni kizazi chenye kudhulumiwa.

Tumefika mahali ama mambo hayo yaishe au tuseme wazi hasa tumekusudia ipi iwe hatma ya nchi hii.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook