KUMBUKUMBU ZA MWEMBECHAI
 
 

Wakati Serikali ikiendelea kuwanyima dhamana, matibabu:
Waislamu waanza kufariki gerezani


AN-NUUR Na. 150 Muharam 1419, Mei 22-28, 1998

BWANA Mohammed Omar ameongeza idadi ya Waislamu waliofia mikononi mwa serikali, kufuatia uvamizi wa polisi katika Msikiti wa Mwembechai, hapo Februari 12, 13 na 29 mwaka huu.

Bw. Mohammed alifariki dunia Jumapili ya Mei 17, 1998 majira ya saa nane usiku katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Kifo hicho cha kusikitisha cha Bw. Mohammed kilitanguliwa na kuugua kwa muda mrefu baada ya kunyimwa dhamana na kukosa matibabu. Yeye alikuwa miongoni mwa Waislamu wengi walio mahabusu katika gereza la Segerea kwa zaidi ya miezi mitatu akituhumiwa kuhusika na vurugu za Mwembechai zilizosababisha magari ya serikali na ofisi za CCM kuchomwa moto.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia yake, maradhi yaliyomsababishia kifo chake ni pamoja na kubanwa na mbavu, kuvimba tumbo na moyo.

Aidha, kwa mujibu wa msemaji huyo, marehemu kabla ya kupelekwa mahabusu, polisi walimpiga ovyo mwilini wakati walipomvamia na kumkamata akiwa kazini kwake maeneo ya Friends Corner, Manzese, hapo Februari 13, mwaka huu, hali iliyomsababisha kupatwa na maumivu makali sehemu nyingi za mwili wake.

Alisema afya ya marehemu ilianza kubadilika siku chache baada ya kuingizwa gerezani. Pamoja na jitihada za kumtetea na kumuombea dhamana ili akapatiwe matibabu ya uhakika, utetezi huo uliishia kupuuzwa.

Wakili anayewatetea watuhumiwa hao alidai mahakamani Kisutu kuwa wateja wake walikuwa wakipewa Asprin bila kujali maradhi wanayoumwa.

Kwa hali hiyo, kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo hali ya marehemu gerezani hapo ilivyozidi kuwa mbaya kiasi cha kushindwa kufika mahakamani. Ilipofika Ijumaa ya Mei 15, mwaka huu, hali ya marehemu ilikuwa ni ya kukatisha tamaa kuweza kupona tena. Ndipo alipopelekwa hospitali ya Muhimbili ambapo siku mbili baadae alirejea kwa Mola wake. "Ilikuwa kana kwamba alipelekwa akakatie roho Muhimbili", alisikika mmoja wa ndugu wa marehemu.

Marehemu ambaye alikuwa ni mkazi wa Kimara-Matangini, jijini Dar es Salaam, alizaliwa mnamo mwaka wa 1948 huko Kidugalo, wilayani Morogoro.

Marehemu ambaye amezikwa Jumanne Mei 19, 1998, katika makaburi ya Kwa Hengo, hapo hapo Kimara, ameacha mjane na watoto wanane. Allah (s.w.) amghufirie makosa yake. Amin.

Wakati Mohamed Omar amekufa Waislamu wengine walioko ndani bado ni mahututi kwani kutokana na kunyimwa dhamana hawapati matibabu yanayostahiki.

Miongoni mwao wana maradhi ya moyo, vidonda vya tumbo na kadhalika, lakini wote hawa hupewa Aspirin.

Aidha yupo yule mwanafunzi ambaye amepigwa risasi mgongoni na sasa yupo taaban. Ndugu zake na Waislamu wanashindwa kumpatia matibabu yanayostahiki hata nje ya nchi kwani naye yupo Muhimbili kama "mfungwa" hana dhamana.

Kufuatia kifo cha Muhamed wito umetolewa kwa Waislamu kusoma khitma katika Misikiti yao na kufanya swala ya ghaibu. Aidha, Waislamu wamehimizwa kuweka Itiqaf ili kumlilia Mola wao kutokana na hii hali inayozidi kuwa mbaya.

Wito huo umetolewa na Waislamu waliohudhuria mazishi ya muhanga huyo. Waislamu kutoka sehemu mbalimbali mikoani walioongea na AN-NUUR kwa njia ya simu wameeleza kusikitishwa kwao na kutokupata japo fursa ya kuwazika wale wanaokufa katika kadhia hii.

Hata hivyo, wamesema wataungana na Waislamu wenzao wa Dar es Salaam kusoma Khitma, swala ya jeneza ya ghaib na Qunut.



 
 

Mihadhara ya kidini na mauaji ya Mwembechai:
Serikali, Kanisa Katoliki lawamani


AN-NUUR Na. 150 Muharam 1419, Mei 22-28, 1998

SERIKALI ya CCM imelaumiwa kwa kuitikia malalamiko ya viongozi wa Kanisa Katoliki dhidi ya kinachodaiwa kuwa mihadhara ya kashfa inayoendeshwa na wahadhiri wa Kiislamu nchini.

Madai hayo yamo katika Waraka wenye kurasa 53 aliotumiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Muislamu mmoja mwenye jina la Abu Aziz wa Dar es Salaam.

Katika Waraka huo wa Mei 15, 1998 ambao umeandikwa katika lugha ya Kiingereza na nakala zake kutumwa ofisi ya Rais na Taasisi mbalimbali pamoja na ofisi za Kibalozi zilizopo nchini, kuna lawama pia zilizoelekezwa kwa viongozi wa Kanisa Katoliki kwa kuishinikiza serikali kuchukua hatua dhidi ya mahubiri ya Waislamu yasiyokubali Uungu wa Yesu.

Waraka huo unadai kuwa ingawa Kanisa Katoliki limekuwa likiishinikiza Serikali toka mwaka 1993 kuchukua hatua dhidi ya mihadhara ya Waislamu, serikali ya CCM iliongeza nguvu na kasi ya kuwakamata wahadhiri wa Kiislamu baada ya mwezi Januari, 1998.

Waraka unaeleza kuwa kasi hiyo ya kamatakamata ilijitokeza baada ya Padri Camillus Lwambano Paroko wa Kanisa Katoliki Mburahati kuilamumu serikali kwa kutotekeleza ahadi zake za kuchukua hatua dhidi ya Waislamu wanaoendesha mihadhara ya kashfa.

"Ni maoni yangu kuwa kuitikia kwa serikali kuliegemea upande mmoja kutokana na ukweli kwamba mwaka 1993 Rais Mwinyi aliwakutanisha viongozi wa Kanisa Katoliki na Masheikh ambapo viongozi wa Kanisa walishindwa kuthibitisha kile walichokiita kuwa ni kashfa", umeeleza Waraka huo.

Aidha, waraka huo ambao umeandikwa katika utaalamu wa kisheria na kujenga hoja zake nyingi katika misingi hiyo, umelaumu serikali kwa kuvunja katiba ya nchi katika kuruhusu askari kutumia nguvu kuliko ilivyohitajika katika kukabili kilichoitwa vurugu za Mwembechai.

Mwandishi wa Waraka huo, Abu Aziz ameshutumu mauaji yaliyofanywa na polisi Mwembechai kuwa ni ya kiuonevu na kwamba wahusika wote wanastahiki kuchukuliwa hatua za kisheria.

Waraka pia umelaumu baadhi ya vyombo vya habari kwa kushabikia hatua zilizochukuliwa na serikali katika tukio la Mwembechai na jinsi vyombo hivyo vilivyoshikilia kuwapachika watuhumiwa jina la "siasa kali", wakati hawakabiliwi na kosa la kuwa na hicho kinachoitwa siasa kali.

Waraka umebainisha kuwa madhumuni yake makubwa ni kuzungumzia juu ya ukweli wa mambo na dhulma iliyofanywa dhidi ya Waislamu kwa kuwanyima haki yao ya kidini waliyopewa na Mola inatambuliwa na katiba ya nchi.

Waraka huo umemaliza kwa kueleza kuwa ufumbuzi unaohitajika katika tatizo la muhadhara na kuuliwa kwa Waislamu Mwembechai ni kuundwa kwa Tume huru itakayojumuisha wajumbe toka taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini.

Nakala za Waraka huo zimepelekwa kwa:

Ofisi ya Rais, Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Waziri wa Mambo ya Sheria na Katiba, Mkurugenzi wa Mashitaka na Mabolozi.

Sehemu nyingine zilizofikishiwa waraka huu ni vyombo vya habari, jumuiya ya Wanasheria (Tanganyika Law Society), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake (Tanzania Women Laywers Association), Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo ya Jamii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Idara ya Taaluma ya sayansi ya jamii na siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,

Aidha, waraka huo pia umesambazwa kwa Baraza Kuu la Jumuiya ya Shia Ithnasheri ya Tanzania, AL-MALLID, KHIDMAT, Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiislamu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kanisa Katoliki Tanzania, Kanisa la Kilutheri Tanzania, Vyama vya siasa na Mfuko wa Mwalimu Nyerere.


Suala la Mwembechai:
KK aitahadharisha Serikali


AN-NUUR Na. 150 Muharam 1419, Mei 22-28, 1998

MBUNGE wa Kigamboni (CCM) Mhe. Alhaj Kitwana Kondo ameitahadharisha serikali kwamba mambo inayowafanyia Waislamu, inawafanya wajenge dhana kwamba serikali haiwataki.

Amesema ni jambo la kushangaza kwamba Waislamu wamewekwa ndani zaidi ya miezi mitatu bila ya dhamana na sasa wanakufa mmoja mmoja.

Akiongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Mei 21, mwaka huu, Alhaj Kitwana Kondo alielezea jinsi Waislamu wanavyoteseka magerezani ambapo hata pale walipotaka kujigharamia wenyewe dawa walikataliwa.

Akitoa mfano alisema Bw. Daud aliyekamatwa kwa tuhuma za kuvisaidia vikundi vya mihadhara pamoja na yeye kuwa ni mgonjwa, alipoona hali ya gereza ni mbaya na wafungwa wengi wanateseka kwa magonjwa bila ya dawa aliomba mahakamani aruhusiwe kutoa msaada wa dawa, lakini akakataliwa. Kwa sababu gani mtu akataliwe kuwanunulia wafungwa dawa; "Nia nini?" alihoji Alhaji Kondo.

Dhana inayojengeka miongoni mwa Waislamu ni kwamba serikali inataka Waislamu wale wafe mmoja mmoja jela, na lau dhamiri ya serikali si hiyo basi, Alhaj Kitwana Kondo alisihi iwape dhamana Waislamu hao.

Akizungumzia suala la mihadhara inayoitwa ya kashfa, Alhaj Kondo alisema kwamba serikali inafanya makosa kuwakamata watu wanaosema Yesu sio Mungu kwani hivyo ndivyo kitabu chao kinavyosema.

Alisema japo hiyo kashfa yenyewe mpaka leo haijaanishwa lakini kama serikali itang'ang'ania kuwaona kwamba ni wakosa Waislamu wanaosema Yesi si Mungu, basi itabidi ipige marufuku Qur'an na Uislamu wenyewe.

Alisisitiza kwamba hakuna mgogoro wowote baina ya Waislamu na Wakristo. Na ndio maana pamoja na yote yaliyotokea Mwembechai hakuna Kanisa lililodhuriwa. Alhaj Kitwana Kondo alisema mgogoro au fitna ipo baina ya serikali na Waislamu.

Katika nukta hiyo, Alhaj Kondo alihoji; hata kama ipo kashfa ni vipi serikali isimame kushitaki wakati yenyewe haina dini. Au kama imeona kashfa ni mbaya vipi imshitaki anayesema Yesu si Mungu lakini isimshitaki aliyewakashifu Waislamu katika gazeti la Sunday Observer kuhusu vazi la buibui.

Aidha, Alhaj Kondo alihoji ni vipi aliyeandika kwenye baiskeli yake "Yesu si Mungu" akamatwe, lakini walioandika Yesu ni Mungu katika magari yao wasikamatwe.

Kuhuusu kukamatwa kwa Bw. Daud anayedaiwa kuvisaidia vikundi vya mihadhara, Alhaj Kitwana Kondo ameishangaa serikali ni vipi mtu anakamatwa kwa kuisaidia jumuiya ambayo haijapigwa marufuku.

Alisema si kosa kuisaidia taasisi ambayo haijapigwa marufuku. Na taasisi za mihadhara anazodaiwa kuzisaidia hazijapigwa marufuku. Vipi Bw. Daud akamatwe na kuwekwa ndani mwezi wa pili sasa dhamana kukataliwa!

"Serikari haifanyi vyema kuwazuia wafanyabiashara kusaidia taasisi ambazo hazijapigwa marufuku", alisema Mhe. Kitwana Kondo. Kuhusu kauli ya serikali kwamba itazifungia baadhi ya taasisi, Mhe. Kitwana Kondo amesema serikali isiwe na mtindo wa kutaka kuzifungia jumuiya za kidini kwa vile zinaikosoa.

Akizunguma kwa uchungu Mhe. Kondo alilaani kitendo cha polisi kuingia Msikitini na zaidi kitendo cha wanawake wa Kiislamu kudhalilishwa huko gerezani walipokuwa rumande.

Alisema mpaka leo serikali haijafanya lolote kuhusu madhila hayo waliyofanyiwa Waislamu. Bali mambo yanazidi ambapo waliomo ndani wanakufa mmoja mmoja na dhamana hawapewi. Mhe. Kitwana Kondo alitahadharisha kwamba fitna iliyopo baina ya serikali na Waislamu yaweza kuzua baa pale aliposema kuwa madogo ndio huvunja mfupa.
 

Hatimaye Mzee Katambo, Chata waachiwa

Na Mwandishi Wetu

WAZEE wawili waliowekwa rumande kwa miezi kadhaa wameungana na familia zao baada ya AN-NUUR kufichua kupuuzwa agizo la Rais kulikofanywa na baadhi ya wahusika.

Kwa takriban miezi mitano, Mzee Chata Abdallah na Mzee Katambo walisota mahabusu hatimaye wameachiliwa huru ikidaiwa kwamba hawana shitaka la kujibu.

Mzee Chata Abdallah ambaye ni Imamu wa Msikiti wa Mtambani aliachiwa huru mchana wa Ijumaa, Julai 3, Mzee Mussa Katambo aliachiwa Julai 6.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, mwendesha mashitaka wa Polisi alidai mbele ya Hakimu Ligema kuwa washitakiwa hao wamefutiwa shitaka na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) baada ya kuona hawana kesi ya kujibu.

Kukamatwa kwa wazee hao kulifuatia hatua za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Luteni Makamba kuitikia kilio cha Paroko Lwambano wa Kanisa Katoliki Mburahati kuhusiana na suala la mihadhara.

Wakiwa rumande pamoja na watuhumiwa wengine wa kadhia ya Mwembechai, taarifa zinafaamisha kwamba Rais alitoa agizo ambalo lilitaka wahusika wawaachie huru wazee wote, wanawake na wanafunzi.

Hata hivyo pamoja na kuwepo kwa agizo la Rais, wazee hao waliendelea kusota rumande katika gereza la Segerea huku wakipata mateso na madhalilisho ya kila namna.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake Mwananyamala kwa Msisiri, Mzee Chata alisema kwamba, alikamatwa nyumbani kwake Februari 10, 1998 saa 5 asubuhi na askari watatu walivalia kiraia.

Alipelekwa kituo cha polisi Oysterbay kisha kituo kikuu (Central) ambapo kote alidaiwa kufanya mhadhara bila kibali na kuwakaribisha watu wa mhadhara katika msikiti anaoungoza, walilala kituo cha polisi ambapo kesho yake walipelekwa mahakamani na kisha kurundikwa Keko.

Huko amesema walikuwa wakivuliwa nguo bila kujali umri wao kwa madai ya kupelekuliwa. Pamoja na kuvuliwa nguo mara kwa mara amesema walikuwa wakipigwa sana virungu na kupewa adhabu mbalimbali.

Akitoa mfano, alisema yeye pamoja na kuvimba na kuumwa miguu alikuwa akilazimishwa kuchuchumaa wakati hawezi. Alisema ilibidi akinge kifua awaambie askari hao bora wampige risasi.

Alisema pamoja na watuhumiwa kuugua maradhi mbalimbali kama upele, vifua, tumbo na magonjwa mengine, lakini wote walikuwa wakipewa Panadol, Aspro na Asprin.

Mzee Chata Abdallah alizaliwa mwaka 1922 huko Rutare, Ujiji mkoani Kigoma. Alisoma Madrasa (ya juu) mwaka 1929 hadi 1938 huko Tabora.

Muda wote amekuwa ni mwanachama hai wa TANU na CCM. Amewahi kuwa mjumbe wa Halmashauri ya TANU ya Wilaya ya Igunga na mkoa wa Tabora.

Amekuwa Diwani kati ya mwaka 1968 hadi 1976 akawa Katibu Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni.

Hivi sasa ni Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mtambani, wilayani Kinondoni.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook