Mauaji ya Mwembechai ni ya kidini.
Mapambano kati ya polisi
na Waislamu:
Waliokufa sasa ni wawili
IDADI ya watu waliouawa kufuatia mapigano kati ya polisi na waumini wa dini ya Kiislamu katika msikiti wa Mwembe Chai jijini, imefikia wawili baada ya mtu mmoja aliyekuwa amelazwa hospitalini Muhimbili, kufariki dunia jana usiku.
Habari kutoka wodi namba tisa Kibasila ambako majeruhi wamelazwa zinasema mtu huyo ambaye jina lake halijafahamika mara moja alifariki jana usiku mara baada ya kufikishwa wodini hapo.
Wengine waliolazwa katika wodi hiyo ni pamoja na mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Kiislamu ya Al-Haramaini iliyopo Mtaa wa Lindi Ilala, Chuki Kipambano (17) ambaye alijeruhiwa kwa risasi mgongoni na kifuani.
Katika wodi hiyo pia kuna mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Mtiani (32) mkazi wa mtaa wa Sikukuu Kariakoo jijini.
Bw. Mtiani ambaye pamoja na kujeruhiwa kwa risasi kwenye mguu wa kushoto, alikuwa akiendelea kuhubiri kitandani kwake. Hata hivyo, baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wadi hiyo, walikuwa wakimbeza Bw. Mtiani kwa kumwita 'mtangaza dini'.
Habari zaidi kutoka Hospitalini hapo, zilisema kwamba jina la mtu aliyeuawa juzi na polisi limetambulika kuwa ni Saleh Issa (30) mkazi wa Tandale Jijini.
Katika tukio jingine Mwandishi Wetu Tumaini Mwaijenge anaripoti kuwa jeshi la Magereza limelazimika kuimarisha ulinzi wa magereza yake matatu yaliyopo jijini kufuatia tishio lililotolewa na Waislamu wenye msimamo mkali wa kutaka kuwatoa viongozi wao waliokamatwa kutokana na kashfa za kidini.
Gazeti hili lilishuhudia askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia ghasia Magerezani (KMKGM), kikivinjari katika gereza la Keko, wilayani Temeke na askari wengine wakiwa kwenye Gereza Kuu la Ukonga na lile la Segerea.
"Hakikisheni hakuna mtu yeyote anayesogelea gereza bila ya kazi maalum. Jukumu la ulinzi liko mikononi mwenu", alisikika Kamishna Mkuu wa Jeshi hilo, Bw. Onel Malisa akiwaambia askari hao alipokuwa katika ukaguzi wa usalama wa magereza hayo, usiku wa kumkia jana.
Katika ziara hiyo ya Bw. Malisa, alikuwepo pia Mkuu mpya wa Magereza wa mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Ahmed Shangiri ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa chuo cha Magereza cha Ukonga.
Tukio jingine lililovuta hisia za askari katika gereza la Keko ni kuona watuhumiwa hao wa kike, wakiingia gerezani hapo bila kuwa na nguo za ndani walipopekuliwa.
Walipoulizwa ni kwa vipi wote hawajavaa nguo zao za ndani, walidai kuwa walilazimika kuzivua kutokana na kuwashwa na mabomu ya machozi yaliyovurumishwa na polisi katika jitihada za kuwatawanya kutoka katika msikiti huo wa Mwembe Chai.
Naye Nelly Mtema anaripoti, kwamba Bw. Christopher Mtikila anayejiita Mchungaji wa Taasisi ya Liberty Desk amepinga kitendo cha polisi kuwashambulia na kuwaua waumini wa Kiislamu wa Msikiti wa Mwembechai jijini na kusema kuwa kitendo hicho kinakiuka uhuru wa kuabudu.
"Kuwa na uhuru wa kuabudu, lazima kila kundi
liwe na uvumilivu katika kuvumilia maneno ya wenzake na tulikubaliana hivyo
pale Karimjee sasa nguvu ya dola imetoka wapi?" alihoji Mchungaji Mtikila.
Ni dhahiri kuwa mauaji ya Waislamu yamefanywa na serikali isiyo na dini lakini ikawa inatii kanisa.
Nukuu
nyingine inayoonyesha kuwa mauaji yale ni ya kidini, kwa vile kanisa limeishinikiza
serikali na kuwa mtandao mzima wa serikali una harufu ya kanisa zaidi kuliko
taifa ni pale serikali na chama tawala kinyume na ubinadamu, Waziri mkuu
ameripotiwa akisema Serikali sasa imeamua kwa dhati kupambana na watu wanaokashfu
dini" (majira). CCM nayo imewapongeza polisi na kuelekeza J.W.T.Z. litumike
kupambana na vurugu za kidini. (Mtanzania Na 706 la Ijumaa Februari
20/1998 linatuelimisha zaidi.)
KUFUATIA VURUGU ZA MWEMBECHAI
JWTZ ruksa kutumia risasi kuzima ghasia zote za kidini
Na Mwandishi wetu
VIKOSI vya ulinzi na usalama vimeelekezwa kutumia risasi za moto kuzima ghasia za kidini iwapo kufanya hivyo, itakuwa ndiyo njia pekee ya kulinda amani ya walio wengi, imefahamika.
Habari zilizopatikana serikalini, zimeeleza kuwa hayo, yalikuwa maazimio ya mkutano wa kamati ya Ulinzi na usalama pamoja na Kamati Kuu ya CCM iliyokutana mjini dodoma na kujadili matukio yaliyosababishwa na Waislamu wenye imani kali wa Msikiti wa Mwembe Chai, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM amesema kuwa hiyo imekuja kufuatia wasiwasi wa serikali kwamba lipo kundi la vijana wa Kitanzania waliopewa mafunzo rasmi ya kuleta na kuendeleza ghasia za kidini.
Alisema pia kuwa serikali ina wasiwasi kwamba vurugu zilizotokea katika msikiti wa Mwembe Chai zinachochewa na mataifa ya nje na zinaweza kukua iwapo serikali haitachukua hatua madhubuti.
"Risasi za moto zitatumika tu. Kwa sababu hekima iko wapi kama utaona vurugu hizo zinaweza kusababisha vifo vya watu 200, ukaacha kumpiga mmoja kusalimisha wengi?" alidadisi kiongozi huyo aliyetaka jina lake lisiandikwe gazetini.
Hata hivyo, alisema kuwa risasi hizo hazitawalenga watu wote, bali wale viongozi watakaoonekana kuwa mbele katika vurugu hizo.
Kiongozi huyo, alisema kuwa yeye binafsi anapingana na kauli ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Gewe aliyoitoa hivi karibuni kwamba polisi waliwapiga risasi kwa bahati mbaya wale waliofariki.
Alieleza kuwa polisi hawakuwa na njia yoyote ya kufanya isipokuwa kuwapiga risasi za moto viongozi wa vurugu hizo kwa sababu bila hivyo vurugu hizo zisingekoma. Alisema hata misahafu inasema kuwa ukimpiga mchungaji kondoo watatawanyika.
Aidha, kiongozi huyo alisema kuwa nchi nne
za Mashariki ya Kati zinashukiwa kuhusika katika ghasia na mihadhara ya
dini ambayo imesababisha maafa na uharibifu katika eneo la Mwembe Chai.
Majira
la Jumamosi Aprili 4, 1998, inasema:
...CCM yaunga mkono polisi
Na Rachel Lugoe
KAMATI Kuu ya Chama cha Mapunduzi (CCM) imeipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kufunga kwa muda Msikiti wa Mwembe Chai jijini na kuweka ulinzi mkali wa Polisi na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika eneo hilo.
Tamko la kamati hiyo kuhusu tukio la Mwembechai la Machi 29, mwaka huu, iliyotolewa jijini jana na Idara ya Uenezi ya chama hicho, limesema hatua kama hizo pia zichukuliwe kwa misikiti mingine yote inayoeneza vurugu na uchochezi nchini.
Uamuzi wa kuunga mkono hatua za Serikali ulitolewa
baada ya kikao cha Kamati hiyo iliyokaa Aprili mosi mwaka huu kilichoongozwa
na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Benjamin Mkapa ambapo pamoja na mambo
mengine, vurugu za Msikiti wa Mwembechai zilijadiliwa.
Kuhusu
CCM kuelekeza kutumia JWTZ, gazeti la Rai Na. 225, Alhamisi Februari 19-Februari
24/1998 linaripoti hivi:
BAADA YA POLISI, FFU KUPATA
TAABU MWEMBECHAI
Jeshi sasa kupambana na wanaofanya
vurugu
MAFUNZO maalum ya kukabiliana na vurugu nchini, yameanza ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na habari za uhakika zinaeleza kuwa mafunzo hayo yanafuatia vurugu zilizozuka katika msikiti wa Mwembe chai Alhamisi iliyopita.
Habari za kuaminika kutoka Chama cha Mapinduzi CCM na serikalini, zimethibitisha kuwa uamuzi wa kulitaka jeshi kuanza kujiandaa kupambana na ghasia za namna hiyo ulifikiwa katika vikao vya wiki iliyopita vya CCM vilivyofanyika Dodoma.
Vikao hivyo ni vya Kamati Kuu pamoja na Kamati ya Ulinzi na Uslama ya chama hicho. Vikao hivyo vyote vilifanyika chini ya mwenyekiti wa kamati hizo mbili, Rais Benjamin Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.
Habari hizi baadae zilikanushwa vikai na serikali.
Habari hizi za kukanusha kutumia jeshi nazo zimeripotiwa na magazeti kadhaa. Kujikanganya kwa serikali na chama kunatia mashaka makubwa juu ya kauli ya kuitegemea.'
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |