KUMBUKUMBU ZA MWEMBECHAI
 
 

Kupotosha ukweli

SIO vigumu ndugu msomaji kuona athari ya Ukristu katika mtandao wa serikali na uendeshaji wake. Lakini inadai haina dini.

Nukta nyingine inayoonesha mauaji yale ni ya kuanza Crusade Tanzania, ni pale serikali inapotafuta mchawi wakati mwanga ni yenyewe. Baada ya kuua serikali ilikuwa inataka kuhalalisha mauawaji kwa kuihusisha mihadhara ya Dini ya Kiislamu na watu mbalimbali ili tendo lake la kuuwa lionekane lina uhalali kwa kuwa kutumiwa ni uchochezi na ni usaliti na uhaini. Serikali kwanza ilizisingizia balozi za nje. Kama vyombo vya habari vilivyoripoti, Majira ya Alhamisi Februari 19/1998 linaripoti hivi:
 


Vurugu za kidini nchini:
Serikali yazituhumu balozi za nje kuchochea

Na Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya kuzuka kwa ghasia za kidini jijini, serikali imesema imezituhumu baadhi ya balozi za nje zilizopo jijini kushiriki katika kuchochea vurugu za kidini nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Ali Ameir Mohamed alisema serikali imepata habari kuwa kuna baadhi ya balozi zinahusika moja kwa moja na vurugu hizo lakini akakataa kuzitaja ni balozi zipi.

Waziri Ameir alisema kuna baadhi ya vikundi vya kidini ambavyo vimepewa usajili na ambavyo vimekuwa vikitumiwa na balozi hizo kuchochea vurugu za kidini.

"Serikali ina habari kuwa wako vijana fulani ambao wamepewa mafunzo rasmi kuendeleza fujo nchini kwa kutumia kisingizio cha dini," alisema Bw. Ameir bila kufafanua kuwa mafunzo hayo yanatolewa na nani.

Waziri Ameir alisema serikali inaendelea na uchunguzi kuhusu uhusiano wa baadhi ya vijana walioshiriki katika vurugu za kidini na baadhi ya balozi zilizopo nchini.

"Tunafahamu kuwa wapo vijana ambao wamehusika na fujo... tunajua uhusiano wao na balozi hizo, lakini ni mapema mno kusema na tunaendelea kuchungua hadi tuukute mzizi wake," alisema Waziri huyo.

Wakati wa mkutano huo, Waziri Ameir pia alisema kuwa vurugu zilizotokea Mwembe Chai hivi karibuni zilikuwa na mkono wa baadhi ya vyama vya siasa.

"Tunaiona harufu ya mkono wa kisiasa lakini hata hivyo tunafanya uchunguzi zaidi," alisema Bw. Ameir huku akitoa mfano wa kuwepo kwa baadhi ya vijana kutoka Unguja na Pemba miongoni mwa watu waliofikishwa mahakamani kuhusiana na vurugu hizo.
 

Serikali haina uhakika na madai yake.

Serikali iliposhindwa kuthibitisha hili, iliwageukia wafanya biashara kama ilivyoripotiwa na Majira Na 1509 Alhamisi 19/1998:
 


Wanaochochea vurugu Mwembechai ni wafanyabiashara - Dk. Omar


MAKAMU wa Rais, Dk. Omar Ali Juma amewaonya wafanyabiashara wanaochochea vurugu za Mwembechai kutotumia fedha zao kununua shari na badala yake wazitumie kuleta maendeleo.

Akizungumza jana katika swala ya Idd el Hajj iliyofanyika kitaifa katika msikiti wa Simba mbili uliopo Tandika wilaya ya Temeke, Dk. Omar alisema vurugu za Mwembechai zinachochewa na wafanyabiashara ambao wanajulikana.

"Nawaonya wafanyabiashara wazitumie fedha zao kuleta maendeleo ya dini na jamii, badala ya fedha zao kuzitumia katika kuleta uchochezi," alionya Dk. Omar. Hata hivyo hakuwataja majina wafanyabiashara hao.

Alisema kuwa japokuwa Rais wa sasa, Benjamini Mkapa ni mkristo, lakini amekuwa akipenda dini zote na roho inamuuma sana kutokana na hizo fujo za Mwembechai.
 

Hili lilipoonekana halikidhi haja wabunge na mawaziri wakahusishwa kama ilivyoripotiwa na Majira na 1549 Jumanne Machi 31/1998.
 


VURUGU ZA MWEMBE CHAI
Mawaziri wawili wachochea


MAWAZIRI wawili wa Serikali ya Rais Benjamini Mkapa na wabunge wawili wa chama cha Mapinduzi (CCM) wametajwa kuwa kiini cha vurugu za kidini katika Msikiti wa Mwembe Chai ulioko jijini.

Viongozi hao ambao licha ya kuwa walezi wa vikundi vinavyoendeleza vurugu hizo wamekuwa wakipeleka mipango ya serikali ya kupambana nao hata kabla maamuzi kamili hayajafikiwa, Majira imegundua.

Afisa mmoja mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, aliyezungumza na Majira kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, jana aliiambia Majira kuwa mara kadha maamuzi kuhusu ufumbuzi wa mgogoro huo yamefikiwa lakini utekelezaji wake unakwamishwa na wakuu hao.

Alisema kukwamishwa kunatokana na baadhi ya viongozi hao kuwa karibu mno na vikundi vya Kiislamu ambavyo baadhi yake ni vile vinavyosababisha vurugu katika Msikiti wa Mwembe Chai.

"Tumegundua kuwa ndani ya vurugu hizi kuna viongozi wa serikali na wanasiasa ambao wamekuwa kikwazo kufikia maamuzi ya pamoja na baadhi yao wanatoa hata siri za serikali kwa vikundi hivyo," alisema.

Alisema kuwa mawaziri hao (majina tunayahifadhi), wamekuwa mstari wa mbele kuvikingia kifua vikundi hivyo na kwamba licha ya kuwa na mafao binafsi kiuchumi, pia wameegemea vikundi hivyo kwa maslahi ya kisiasa.

Afisa huyo alisema wabunge hao (majina yao pia tunahifadhi), mmoja kutoka kanda ya Mashariki na mwingine Kanda ya Magharibi wamekuwa ni daraja kati ya wafadhili kutoka nchi za Kiarabu na Afrika magharibi.

Alisema kuwa kila wanapokutana kutaka kuchukua hatua, maamuzi yao huvifikia vikundi hivyo kabla ya hatua kuchukuliwa. "Huu ni ushahidi wa baadhi yetu kuhusika...hakuna siri". alisema,

Alisema vurugu za Mwembe chai ni tatizo dogo ambalo kama watendaji serikalini wangekuwa na kauli moja, lakini imeshindikana kutokana na kusalitiana kwa watendaji wao kwa wao.

Afisa huyo pia alisema baadhi ya wasomi katika Vyuo vya Elimu ya Juu nchini wamo katika vurugu hizo na alimtaja Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa anapata misaada kutoka nchi moja ya Afrika Magharibi kwa ajili hiyo.
 

Baada ya kusema uwongo wote huo serikali ikatangaza kufuta vikundi vya Dini kama ilivyoripotiwa na Majira Na 1579 Alhamisi Aprili 30, 1998.
 


MIHADHARA YA KASHFA ZA KIDINI
Serikali kufuta vikundi 22

Na Faustine Rwambail

VIKUNDI 22 vya kidini nchini vimo katika hatari ya kufutiwa usajili kufuataia uchunguzi wa polisi kubaini kuwa vinajihusisha na mahubiri ya kashfa na chuki, Majira imegundua.

Katika orodha ya vikundi hivyo, 14 ni vya Kikristo na vinane vya Kiislamu na ripoti rasmi ya vikundi hivyo imewasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Benard Mchomvu.
 

Kama uongo uliotangulia hautoshi hatimae wakazua lingine kuwa ghasia za Mwembe Chai zimeandaliwa kama Majira linavyoripoti Na 1515 la Jumatano February 25, 1998:
 


'Ghasia za Mwembe Chai ziliandaliwa'

Na Faustine Rwambali

SERIKALI imeombwa kufanya uchunguzi wa kina ili kujua chanzo cha vurugu zilizotokea kwenye msikiti wa Mwembe Chai jijini hivi karibuni kwa vile madai kuwa zilitokana na mihadhara au kukamatwa kwa kiongozi wa msikiti huo si ya kweli.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Ali Malapa alipokuwa akitoa maoni yake kuhusiana na vurugu hizo ambazo zilisababisha vifo vya watu wawili, uharibifu wa mali na majeruhi kadhaa.

Maoni ya Mzee Malapa yanalingana kwa kiasi fulani na maoni ya serikali yaliyotolewa na Waziri wa mambo ya Ndani, Bw. Ali Ameir alizituhumu balozi za nje kuhusika na uchochezi wa kidini akidai kuwa upo ushahidi kuwa baadhi ya balozi zinawafadhili na kutoa mafunzo ya vurugu kwa vijana wanaojihusisha na mihadhara ya kashfa za kidini.
 

Maelezo yanayopingana ya serikali ni ushahidi wa kubabaika kwa serikali na kutafuta uhalali wa mauaji ambayo katika kutii amri ya kanisa kwa gharama yeyote ile serikali iliwabeza wabunge wake walipotaka mauaji ya polisi kwa ujumla wake yachunguzwe. Kwa kuwa hoja hii ilitolewa wakati wa maujaji ya mwembe chai, basi suala zima lilibebeshwa sura ya Mwembe Chai na kupuuzwa ingawa ni kweli kulikuwa na mauaji yaliyofanywa na polisi Arusha na Mbeya. Majira ya Jumanne March 10, 1998 inariporti hivi:-
 


Madai ya kutaka mauaji ya Polisi yachunguzwe...

Na Deus Ngowi

SPIKA wa Bunge, Bw. Pius Msekwa amekataa maombi ya wabunge 21 waliotaka aitishe kikao cha Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba ili kujadili kile kilichoelezwa kuwa ni vitendo vya kikatili vya polisi wanaotumia silaha dhidi ya raia.

Katika majibu yake aliyotoa kwa wabunge hao jana, Bw. Msekwa alisema kuwa baada ya kutafakari kwa makini na kwa kuzingatia kanuni za Bunge na mahitaji ya fedha aliamua kutolikubali ombi hilo.

"Baada ya kulitafakari ombi hilo kwa makini sana, kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za Bunge zinazohusika pamoja na mambo mengine ya kiuendeshaji hususan matumizi ya fedha, nimefikia uamuzi wa kutolikubali ombi hilo, "amesema Bw. Msekwa katika majibu hayo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook