Tutapigania damu yetu kwa gharama yoyote - Semina

Na Bakari Mwakangwale

Damu ya Muislamu ni takatifu haiwezi kumwaga burebure tu.

Haki ya Muislamu ya uhai itapiganiwa kwa gharama yoyote

Hayo yamesemwa na akinamama wa Kiislamu toka Shinyanga walio jijini kuhudhuria semina ya khitma ya mashahidi wa Mwembechai.

"Tunachukua fursa hii kuungana na Waislamu wenzetu popote pale walipo, ambao wanagushwa na mauaji ya Mwembechai", ameeleza msemaji wa akina mama mmoja.

Wakizungumza katika semina inayoendelea katika Msikiti wa Mwenge, wamesema wanalaani mauaji yaliyofanywa na polisi kwa Waislamu halikadhalika kudhalilishwa kwa akinamama.

Nao wawakilishi toka Korogwe, walieleza kuwa umoja wao ulianzishwa Februari 28, 1998 na kuzinduliwa na Mhe. Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi Julai 25, mwaka huo huo ukiwa na madhumuni ya kushikamana kwa pamoja katika kamba ya Mwenyezi Mungu kutofanikiwa ili kukuza Uislamu.

"Kwa mshikamano huo tunategemea kupata maendeleo katika nyanja za elimu, afya na kijamii", alieleza mmoja wa wawakilishi hao.

Wawakilishi hao walieleza mafanikio yao kuwa ni kuunganisha kina mama wa mji wa Korogwe na vitongoji vyake vyote, (Manundu, Old Korogwe, Kwa Samangube, Mgombezi na Majengo) walieleza mafanikio mengine ni kufuturisha taasisi mbalimbali katika mwezi wa Ramadhani kama vile Magereza, shule ya sekondari wasichana Korogwe, Chuo cha Uuguzi (PHN) na chuo cha Waalimu (TTC).

Aidha walieleza matarajio yao kuwa ni kupanua wigo wao hadi vijijini, kupata mawasiliano na vyombo vingine vya kidini pamoja na kuhamasisha Waislamu wote kupeleka masuala yao ya malalamiko katika kitengo cha suluhu walichoanzisha.

Walieleza matatizo waliyo nayo ni kusumbuliwa na BAKWATA: "Tumelazimika mara nyingi kuswali swala za Idd za pamoja tukiwa tumesimamiwa na mitutu ya bunduki na polisi kwa fitina za taasisi kama hiyo", alieleza.

Pia walitoa maombi kushirikiana ili semina kama hizo zifanyike wilayani kwao (Korogwe) ili watu wao wahamasishike.

Kwa mujbu wa mmoja wa wasimamizi wa semina hiyo Bi. Fatma Musa, alieleza kuwa semina hiyo imehudhuriwa na kina mama kutoka sehemu mbalimbali alizitaja kuwa ni Bukoba, Mbeya, Iringa, Morogoro, Korogwe, Songea, Shinyanga na kwingineko.

Pia alieleza kuwa semina hiyo inatarajia kumalizika Februari 12.

AN-NUUR mpaka linakwenda mitamboni ni wawakilishi wa Korogwe na Shinyanga tu ndio waliowakilisha ripoti zao.

"Tunatarajia kupata ripoti zaidi kutoka kwa wawakilishi wengine toka mikoani", alisema Bi Fatma Musa.


Tume yatuhumiwa kwa kupunguza muda wa kampeni

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeituhumu hatua ya Tume ya Uchaguzi kupunguza muda wa kampeni na kueleza muda huo hautoshi, kwani kuna ongezeko kubwa la wapiga kura mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Akwilombe alisema katika makao makuu ya chama hicho Buguruni Jijini mapema wiki hii kuwa Watanzania wengi sasa hivi wameingia katika siasa ambapo kuna ongezeko la wapiga kura takriban milioni nne mpaka tano, hivyo ingefaa muda huo uongezwe badala ya kupunguzwa.

Pia alieleza kuwa ongezeko lingine linatokana na vijana waliokuwa na umri kati ya miaka kuanzia 15 na 17 mwaka huo (1995), alieleza kuwa hawa mwaka huu lazima wapige kura.

"Kwa vigezo hivi kutakuwa na mabadiliko hawezi kupatikana Rais kwa kura milioni tatu, lazima atakwenda kwa kura milioni tano au saba", alisema Naibu Katibu huyo.

Mapema hivi karibuni Tume ya Uchaguzi imetangaza kupunguza muda wa kampeni na Mwenyekiti wake Jaji Lewis Makame, bila sababu maalum.

Naibu Katibu huyo wa CUF ameeleza kuwa wameshangazwa na hatua hiyo kwani wameshapeleka malalamiko kwamba siku zilizopangwa awali hazitoshi, pia walieleza hili katika mjadala na washauri wa mambo ya uchaguzi waliokuja hivi karibuni.

"Walikuja washauri wa mambo ya uchaguzi wiki mbili zilizopita, moja ya madai ilikuwa muda wa kujiandikisha uongezwe, badala yake wamepunguza muda", alisema Bw. Akwilombe.

Aidha, alieleza kuwa washauri hao waliafiki suala hili kwani katika nchi kama hii yenye mawasiliano duni haiwezekani kuwa na muda mfupi wa uchaguzi.

Alieleza kuwa wao hawana imani na Tume ya Uchaguzi na kuhoji kuwa tume inafanya kazi na nani? "Tume inafanya kazi na nani wateja wao ni vyama vya siasa, mawasiliano na sisi ni madogo".

Bw. Akwilombe alieleza kuwa Tume haina uwezo wa kuendesha uchaguzi: "kwani hata ukiangalia mwaka 1995 kesi nyingi zilikuwa ni makosa ya Tume, Tume inavuruga Demokrasia, inaleta vurugu katika nchi", alisisitiza Bw. Akwilombe.

Katika taarifa yake iliyotangazwa katika baadhi ya vyombo vya habari, Tume hiyo imeeleza kuwa, badala ya kuanza kampeni za uchaguzi Mkuu Agosti 14, mwaka huu, kama ilivyokuwa awali, sasa zitaanza Agosti 19.

Kwa mujibu wa taarifa hizo uandikishaji utakuwa kati ya Agosti 8 na agosti 28 mwaka huu, badala ya Agosti Mosi hadi 21 kwa ratiba ya awali.


'Simameni imara kuipiga vita dhulma'



Na Abu Zubeir, Dodoma

WAISLAMU wametakiwa waache kuishabikia dhulma inayotendeka dhidi yao, badala yake waungane.

Uislamu kuiondoa. Aidha wale wenye mawazo kuwa zipo taasisi au vikundi fulani vyenye uwezo wa kupambana na dhulma ni mawazo potofu kwani suala la kuondoa uovu ni jukumu la kila Muislamu.

Sheikh Ahmed Said aliyasema hayo hivi karibuni pindi alipokuwa akitoa khotuba yake ya sala ya Ijumaa Masjid Manyema mjini Dodoma.

Sheikh Said alisema kuwa kuishabikia au kuikubali dhulma ni kule kukaa kimya bila kutoa hisia kwa kuwaambia wale wanaodhulumu.

Sheikh Saidi amewataka Waislamu wajione kama ndugu moja, kutoa ushirikiano wa kila hali na mali na kuonesha hisia kwa matatizo yanayowapata ndugu zao, yachukuliwe kama ni yao wote.

Wakati huo huo, Waislamu kadhaa kutoka eneo la Ujiji Mkoani Kigoma wako njiani kuelekea Dar es Salaam kuungana na Waislamu wengine nchini kuhudhuria kumbukumbu ya mauaji ya Waislamu Mwembechai yaliyofanyka Februari, 1998.

Akitoa taarifa hizo miongoni mwa wajumbe hao ambao walitegemewa kuwasili Dar es Salaam Alhamsi Februari 10, mwaka huu, Bwana Sissango ambaye ni mvuvi maarufu wa mjini Kigoma, alisimama mjini Dodoma wakati akitafuta usafiri wa mabasi kuelekea Dar es Salaam.

Alisema kuwa wenzake wametangulia kwa gari moshi kuelekea Dar es Salaam. "Mimi nimeamua kusimama kidogo kwa ajili ya kuwaona jamaa zangu ambao ni wagonjwa", alimaliza kusema.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook