Na Mwandishi Wetu
WANANCHI sehemu mbalimbali jijini na mikoani, wamepinga muswada uliopitishwa bungeni wakidai unatoa mwanya kwa siasa za udini na ukabila.
Wamesema baadhi ya watu kwa niaba ya makundi yao wamepitisha kwa nguvu muswada huo huku wakidai kuwa ni maoni ya wananchi wengi.
Aidha wametahadharisha kuwa watu wasipokuwa makini CCM itaipeleka nchi kuzimu.
"Tusipokuwa makini nchi itatoswa kuzimu", amesema Mzee Abbas bila ya kufafanua.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya jamii ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini amelamu serikali, CCM na Spika wa Bunge kutokana na namna suala hilo lilivyopelekwa.
Amesema serikali kwa upande wake imeifanyia mzaha Katiba ya nchi kwa ile hatua yake ya mwanzo ya kutoa waraka namba moja kukusanya maoni ya wananchi.
Aidha, ameituhumu CCM kwa kujali zaidi maslahi ya chama hicho ikifumbia macho hatari inayoweza kuikabili nchi kutokana na kosa la makusudi linalofanywa sasa.
Msomi huyo ametolea mfano kifungu kinachotoa ushindi kwa mgombea nafasi ya Rais kwa kufuata wingi wa kura dhidi ya wagombea wengine badala ya idadi ya asilimia 51% ya kura zote zilizopigwa.
Msomi huyo alionesha masikitiko yake wakati huu ambapo dunia inahimiza upanuzi wa demokrasia, Tanzania inaidunisha.
Alieleza kuwa kwa maoni yake marekebisho hayo yamefanywa kwa hofu ya Chama Tawala kushindwa kupata idadi ya kura za asilimia 50. Aliongeza kueleza kuwa dawa ya hofu kama hiyo ni kukubali kushirikiana kwa vyama na kuunda serikali ya mseto.
Msomi huyo alionya kwamba kifungu hicho cha sasa kitatoa mwanya kwa utawala wa kikabila, kidini na hata madhehebu.
Akitolea mfano, maoni yake hayo, alisema makabila yenye idadi kubwa ya watu nchini kama Wasukuma au madhehebu ya Kikristo kama vile Wakatoliki, wakiamua kujiandikisha kwa wingi na kufanikiwa kuwapumbaza Watanzania wasioelewa, wanaweza kuingia madarakani kwa urahisi. Hilo huenda likafungua mlango wa kila dini au kabila kufanya hivyo, ameeleza.
"Muislamu hawezi kukubali kuona Mkatoliki anachukua nchi kwa ujanja huo. Nae ataingia kikampeni nyumba kwa nyumba, na mwisho wake tutaishia kwenye vurugu za wenyewe kwa wenyewe maana hakuna atakayekubali kutawaliwa kiujanja", alimaliza.
Msomi mwingine ambaye kitaaluma ni mwanasheria amemshangaa Spika wa Bunge Mhe. Pius Msekwa kwa kushindwa kuonesha uwezo wa Bunge katika masuala ya kidola.
Bwana Damian Migeo wa Sinza jijini akizungumza na mwandishi katikati ya wiki hii amesema wanaostahiki lawama zote ni Wabunge wa CCM ambao wameonekana kutetea msimamo wa chama chao badala ya kuwakilisha matakwa ya waliowachagua.
"Kila Mbunge wa CCM aliyesimama kuzungumzia suala hilo alionekana wazi kutetea msimamo wa chama chake hata katika mambo ambayo dhahiri yanaonekana hayana maana yoyote, kwa mfano kuwemo kwa maneno ya ujamaa katika katiba ya nchi, wakati kilichopo nchini ni ubepari, amesema Bwana Damian.
Nao waumini wa Misikiti mbalimbali jijini nao wamekuwa katika mijadala mikali kuhusu suala hilo.
Mwandishi Wetu aliyezungukia Misikiti ya Ubungo Darajani, Magomeni, Mtambani na Kariakoo alikuta baadhi ya waumini wakiwa katika makundi wakijadili hatima ya nchi kufuatia kupitishwa kwa muswada huo Bungeni wiki hii.
Mzee Shaaban Kadenge wa Ubungo Darajani akihoji kauli ya Spika kuwa alikuwa akifuata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuamua kifungu gani kitumike katika suala la idadi ya Wabunge, alisema anavyoelewa yeye Spika ni mweledi wa sheria na Katiba ya nchi, pia ni mzoefu katika kuendesha vikao vya Bunge iweje ategemee ushauri wa Mwanasheria wa serikali ndani ya Bunge la chama zaidi ya kimoja.
"Hapa nimeshindwa kuelewa labda wanasheria watufahamishe hekima ya Spika katika hilo, vinginevyo hatuzuiliki kudhani kuwa Spika aliandaliwa kabla kupititisha muswada huo", alisikitika mzee huyo wakati akizungumza na waumini wenzake nje ya Msikiti mwanzoni katika ya wiki hii.
Bwana Salum ambaye ni mhadhiri wa Msikiti wa Mtambani ameonya kuwa iwapo Wazanzibari hawataiona hatari ya kumezwa nchi yao ndani ya Muungano huo badala yake "wakajikomba" kichama historia itawahukumu kwa jambo hilo.
Amesema alishangazwa na Wabunge wa CCM Zanzibar waliosimama kuupinga hadharani wito wa Mbunge mwenzao wa upinzani aliyewaomba Wazanzibari wenzie waangalie maslahi ya Zanzibar katika muswada huo.
Bwana Salim amesema Wabunge hao wako kuuza nchi yao kufikia malengo binafsi.
Naye Bwana Mvano wa Msikiti wa Magomeni amesema wale wanaopinga mawazo ya wananchi kwa kuyaita ya upinzani dhidi ya CCM hawalitakii mema Taifa.
Muumini huyo amesema ni hatari kuendelea kuudanganya uma wa Watanzania kwa kudai kuwa kilichozingatiwa katika muswada wa serikali ni maoni ya wananchi walio wengi.
"Huku ni kuvikana vilemba vya ukoka kunakolenga kudumisha utawala wa wachache", ameonya Bwana Mvano jana jioni katika moja ya vikundi vya waumini wanaoswali Msikiti huo.
Sheikh Abubakar wa Kariakoo jijini ameonesha kuhuzunishwa na jinsi mambo yanavyoendeshwa na taasisi kuu za Dola.
"Lazima wananchi sasa tusimame imara kuwaambia hao tuliowakabidhi dhamana kuwa hatutaki kuburuzwa, kwa muda miaka 40 nchi yetu imeongozwa na mawazo ya mtu, wananchi tumekaa kimya hii hali ni ya hatari", Abubakar ameliambia gazeti hili.
Naye Mwandishi Wetu kutoka Mwanza anaripoti kuwa mijadala imekuwa ikiendelea mjini humo kufuatia Bunge kupitisha muswada wa serikali juu ya katiba.
Bwana Jamal Gulet mkazi wa Kirumba amezilaumu taasisi mbalimbali kwa kulikalia kimya suala hilo.
Amesema watu wale wale wanaopiga kelele kuhusu katiba ya Zanzibar hatuwasikii wakiipigia kelele serikali ya Jamhuri ya Muungano.
"Inachofanya SMZ ni kutoa wazo Rais wa sasa asimame au la, lakini serikali ya Muungano (Bara) imeshajadili katiba na kupitisha muswada wake wenye utata," amesema Bwana huyo.
Bwana Shaaban Ndeki wa mtaa wa Igogo amewataka wananchi wote kwa kutumia njia mbalimbali kulaani hatua hiyo ya serikali inayoweza kuvuruga amani na kuisambaratisha nchi.
"Uchache wa wapinzani bungeni umetumika kuipa kibali CCM itekeleze makusudio yake na baadhi ya vigogo wa chama hicho wametumia mwanya wa kujadili muswada kwa kufanya kampeni kupitia bungeni", Ndeki amelalamika.
Muswada wa marekebisho ya 13 ya Katiba ya Muungano ulipitishwa wiki hii na kuibua mjadala mkali bungeni kati ya Wabunge wa CCM na wale wa upinzani.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na Wabunge wengi ni lile la kutangazwa Rais kwa ushindi usiozidi asilimia 50 ya wapiga kura.
Mambo mengine ni pamoja na kumpa uwezo Rais kuteua Wabunge kumi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |