Kulinda utakatifu wa damu na heshima yenu:
Kila aliye muumini awe Diamond J'pili


Na Mwandishi Wetu'
 

"NAKUAMURUNI asiswali mtu Aswir, ila awe amefika kwenye ardhi ya Banu Qurayzah", Mtume aliwaamuru maswahaba wake mara tu baada ya vita vya Ahzab. Kwa uzito huo huo, isimkute mtu Aswr ila yupo Diamond Jubilee Jumapili.

Huo ni wito wa Kamati ya Maandalizi ya Khitma ya mashahidi wa Mwembechai kwa waumini.

Leo halikadhalika, imeelezwa haki ya uhai wa Muislamu na heshima yao, ni ya kupiganiwa.

Waumini wa dini ya Kiislamu kwa mara nyingine tena wanatazamiwa kumiminika kwa maelfu katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini kuwaombea dua Waislamu waliouawa na polisi Mwembechai Februari 13, 1998.

Shughuli hiyo itakayofanyika Jumapili ambayo ni tarehe mnasaba na tukio hilo, itawakusanya pamoja waumini wa dini ya Kiislamu Jijini na mikoa mingine.

Kwa mujibu wa Kamati ya Maandalizi, shughuli hiyo itaanza saa 10 alasiri ya siku hiyo ambapo Waislamu wametakiwa kuswalia Misikiti ya jirani tayari kuelekea ukumbini.

Hadi sasa waumini kutoka Shinyanga, Bukoba, Songea, Dodoma na Iringa wamekwishawasili Jijini kuungana na wenzao kwa ajili ya shughuli hiyo.

Misikiti mbalimbali wiki hii imekuwa ikizungumzia dua hiyo na waumini kutakiwa kuhudhuria kwa wingi.

Matangazo yaliyobandikwa katika kuta sehemu tofauti za Jiji yanaonesha dua hiyo itaambatana na utoaji wa nasaha munasibu na tukio.

Gazeti hili limefahamishwa kuwa wanafunzi Waislamu wa shule za sekondari jijini watakuwa miongoni mwa umma utakaofurika siku hiyo na kutoa ujumbe maalum juu ya Chuki Athumani.

Aidha, vijana wa Kiislamu wa maeneo mbalimbali ya jiji watajumuika pamoja na Masheikh na Maimamu katika dua hiyo inayotazamiwa kuwa ya kihistoria.

Shughuli hiyo pia itahudhuriwa na maafisa Waislamu na watu wengine maarufu Jijini.

Mauaji yaliyofanywa na polisi Msikiti wa Mwembechai Februari 12 na 13, mwaka 1998 ni moja ya matukio makubwa ya kukumbukwa katika historia ya Taifa letu.

Katika mazingira ya kutatanisha jeshi la polisi lilivamia Msikiti wa Mwembechai likilenga kuwakamta viongozi na baadhi ya waumini waliodaiwa kuendesha mihadhara ya kashfa dhidi ya Wakristo.

Katika operesheni hiyo polisi waliwajeruhi waumini kadhaa kabla ya kumpora kiongozi waliyemtaka na kumsweka rumande.

Hali hiyo ilizua shutuma na mtafaruku miongoni mwa waumini wakati huo huo polisi waliokuwa wameuzingira msikiti wakiingia ndani huku wakifyatua hewa ya sumu iliyowaacha taabani mamia ya waumini, hiyo ilikuwa usiku wa Alhamisi Februari 12, mwaka huo.

Katika hali iliyoonekana kudhamiriwa polisi walirudi tena siku ya pili Ijumaa Februari 13, 1998 kuwazunguka waumini wa Msikiti huo baada ya swala ya ijumaa na baadaye kuanza kuwafyatulia risasi waumin hao.

Katika pigapiga hiyo waumini zaidi ya wanne waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kabla ya kusombwa na kurundikwa rumande.

Tokea wakati huo waumini wa dini ya Kiislamu wamekuwa wakiilalamikia serikali juu ya unyama huo wakiitaka serikali iunde Tume kuchunguza kadhia nzima na kuwafikisha mahakamani wauaji.

Hata hivyo, serikali haijachukua hatua yoyote mbali ya kuwashitaki waathirika tangu wakati huo.

Katika hali ya kushtukiza mnamo mwezi Desemba mwaka jana, Rais Benjamin Mkapa akigusia suala hilo katika Waraka mrefu kwenda kwa "Halmashauri Kuu", alidai halina uhusiano wowote na dini, hivyo tume ya kuchunguza mauaji haihitajiki.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook