MAKALA

Hasara za kuwabagua raia

Na S. Hussein

MIONGONI mwa rasilimali muhimu mno ambazo Taifa lolote hutegemea ni watu. Hawa ndio wanaounda na kulijenga Taifa.

Hata hivyo, watu hawa wanatofauti za aina nyingi, kuu kati ya hizo ni jinsia, rangi, dini na kabila. Iwapo Taifa husika halitaweka misingi bora ya Utaifa, tofauti hizi huweza kuleta madhara makubwa.

Mbali ya kuweza kusababisha machafuko katika jamii kama ilivyotokea Rwanda, Burundi, Yugoslavia, Bosnia na Afrika Kusini, suala la ubaguzi lina hasara kubwa kwa jamii kimaendeleo kwani sehemu fulani ya jamii hukosa fursa ya kutoa mchango katika sekta mbalimali.

Kwa mfano hapa Tanzania kitendo cha kuwabagua Waislamu kielimu, kimeitia hasara jamii yetu kwani idadi kubwa ya wananchi hawa wamekosa nyenzo muhimu ya maendeleo. Mbali na wao wenyewe kushindwa kujikwamua kwa sababu ya elimu duni, pia hatujuia ni wangapi miongoni mwa wananchi hao walionyimwa elimu ambao wangeweza kuchangia vipaji vyao katika taaluma na kulipatia Taifa wataalamu wa masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na wahandisi, madaktari na wachumi.

Watu hawa wangeweza kuwa wajenzi bora wa Taifa letu lakini vipaji vyao vimeuawa kwa makusudi na kuishia mitaani ambapo serikali sasa inahangaika kwa nguvu na gharama kubwa kulidhibiti kundi hilo athirika ili kupunguza uhalifu.

Vile vile, kiutawala, hatujui Waislamu walionyimwa madaraka wangetoa mchango gani katika maendeleo ya Taifa letu. Leo hii mtu ana haki kusema kuwa watu wa dini fulani waliorundikana madarakani ndio walioliangusha Taifa letu hadi kuwa moja ya mataifa ya mwisho katika jedwali la maendeleo duniani.

Tunahisi mchango wa Waislamu ungekuwa mkubwa kwa kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye twaweza kusema alisakiziwa nchi iliyokuwa mufilisi wa kila kitu isipokuwa madeni tu.

Kwa hali hiyo, kama tungegawana madaraka kwa uwiano mzuri, huenda nchi yetu isingeanguka kiasi cha kuwafanya watu wa kawaida wahoji kuwa hao wanaong'ang'ania madaraka wamesoma kweli au wamekaa madarasa mengi?

Baya zaidi ya yote hayo, ni serikali kuzuia jitihada za wananchi walioathirika kujikwamua kiuchumi na kielimu. Kitendo ambacho kinawshangaza hata wahisani ambao wanatuona kweli sisi ni masikini jeuri.

Jitihada hizo za wananchi kwa msaada wa wafadhili zingesaidia nchi kupunguza idadi ya watu wasio na elimu au uwezo wa kiuchumi ambao ni mzigo mzito kwa jamii na taifa.

Waislamu wanataka kujiunga na OIC, shirika ambalo litasaidia jamii kwa ujumla kwa kujenga mahospitali, mashule, vyuo vya fani mbalimbali pamoja na kuanzisha miradi ya maendeleo. Mambo yote haya yatanufaisha Tanzania na Watanzania.

Hapana shaka hospitali zitakazojengwa zitatoa huduma kwa wananchi wote. Tunao ushahidi wa zahanati za Waislamu zinavyotoa msaada mkubwa wa kitabibu kwa wananchi wa dini na imani zote na halikadhalika hospitali za Wakristo zinavyohudumia watu wote.

Aidha, shule na vyuo vya elimu hata kama vitamilikiwa na Waislamu bado watakaonufaika ni wazalendo wa nchi hii hata ikiwa ni Waislamu watupu. Kuna vijana waliosoma katika shule za Kiislamu ambao hivi sasa wanatoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa.

Hivi, viongozi wetu wa nchi huwa wana maana gani wanapoitangazia dunia kuwa nchi yetu ni masikini sana kiasi kwamba watoto wengi hawapati hata elimu ya msingi wakati wao wenyewe wanachangia kuwakwamisha wananchi wasiweze kuondokana na tatizo hilo.

Au wanapozungumzia watoto wasiokwenda shule huwa hawawahesabu watoto wa Kiislamu?

Kadri tunavyozidi kupoteza muda ndivyo tunavyozidi kulidumaza taifa letu kwani idadi ya watu wasio na elimu inazidi kuongezeka na ni vigumu kupata maendeleo ya haraka ya kitaifa iwapo nchi ina umati mkubwa wa wasio na elimu.

Faida nyingine ya OIC ni ajira watakazopata vijana wetu kutokana na miradi ya maendeleo. Leo vijana ambao wengi wao ni Waislamu wanakamatwa na kutupwa magerezani kwa kosa la uzururaji wakati kazi zenyewe hakuna. Na serikali yenyewe inatamka bayana kuwa ajira hakuna. Sasa vipi waikatae hisani ya kuongezewa vyanzo vya ajira. Au Waislamu hawastahili kupata ajira na kuishi maisha bora kama raia wengine?

Wakati umefika kuachana na sera za Vaticano za kubagua raia wa dini nyingine. Twafahamu kuwa kinachozuia OIC ni kuwa wenzetu walikwishasajili Taifa hili katika buku la 'Baba Mtakatifu' hivyo kuiruhusu OIC ni kuusaliti Ukatoliki. Tuachane na udini huo, tulinusuru Taifa letu.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook