Serikali hii inawatumikia kina nani?
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington
DC - USA
TULIPOKUWA tunapigania kujikomboa kutoka kwenye minyororo ya utumwa wa kikoloni, tulikuwa katika juhudi za kuondokana na fedheha ya kutawaliwa. Tulikwishajua anayetawaliwa siku zote hupoteza thamani ya utu wake.
MTAWALIWA siku zote ni mnyonge, na mnyonge hana haki, akiipata ni kuwa mwenye nguvu, ambaye ndio mtawala wake kapenda au kazidiwa nguvu na mnyonge. Mnyonge kasema sasa basi, leo ndio mwisho wa kutawaliwa, kama kufa nife!
Watanzania kwa kuitambua hali yetu ya unyonge, ya kukosekana kwa haki zetu na fedheha ya kutawaliwa, ndipo tulipojitupa kwa hali na mali nyuma ya uongozi wa TANU na AFRO-SHIRAZ kujikomboa.
Wote walioipa msukumo TANU na AFRO-SHIRAZ hawakuwa wanachama wa TANU na AFRO-SHIRA. Wanachama wa vyama vyote vya siasa wakati huo, kama walivyo leo kwa idadi, walikuwa hawajai mkononi kama ukiwalinganisha na idadi ya wananchi wote nchini.
Hatukukataa kutawaliwa na wakoloni ili tuje tutawaliwe hii leo na CCM au kikundi kingine chochote cha wajuaji miongoni mwetu au kutoka nje ya nchi yetu.
Tunapoikabidhi serikali hii dhamana ya kuiendesha nchi yetu kwa kupitia CCM au chama chochote cha kisiasa, inapaswa wanaoipokea dhamana hiyo waelewe kuwa serikali hii ni mali ya Watanzania wote. Tangu wale waliowapigia kura, wale waliowanyima kura na pia wale ambao hawakupiga kura kabisa. Kwani haki ya kupiga kura ni ya kila mwananchi. Uanachama wa chama cha siasa si hoja.
Vile vile ni jambo la msingi kwa wale wanaoomba kura kufahamu kuwa wanapofanya hivyo, wanaomba utumishi wa umma na siyo vinginevyo. Wao ni watumishi wa umma na siyo mabwana wakubwa wa umma.
Wanapoitwa Waheshimiwa, wajue kuwa uheshimiwa ule ni wa umma walioamua kuwaweka wao katika viti vya madaraka waliyonayo kwa wakati ule. Na kwa hao wanaoteuliwa na waliowekwa na umma ni vivyo pia kwao.
La kusikitisha ni kuwa watu hao wanaokuja kuomba kazi za umma, wanakuja mikono nyuma, na kuinamisha shingo na macho kwa unyenyekevu, huku wakitoa ahadi nyingi. Kumbe ahadi zote hizo ni hewa na ulaghai.
Mara wakipata viti vya madaraka, haupiti muda kabla hawajalewa madaraka hayo. Mikono yao huwa kiunoni na kututolea macho ya ukali huku wakitunyooshea vidole kwa dharau na ufedhuli mwingi uliojaa kebehi na kiburi.
Ukitaka kuwakumbusha haki, utashutumiwa kwa uchochezi, uvunjaji wa amani na pengine uitwe mhuni au mwendawazimu. Ukichachamaa utaitiwa F.F.U, upigwe virungu na mabomu, utiwe ndani, udhalilishwe na unyimwe haki yako ya dhamana.
Kama bahati yako mbaya unaweza ukauawa kama wale wenzetu wa Mwembechai na isiwe lolote wala si chochote. Hitima yako, utasomewa risala ya uhuni.
Serikali hii ni serikali ya watu wote. Hii si serikali ya CCM wala si serikali ya Mkapa, kama wachache kwa makosa wanavyoitambua. Hii ni serikai ya umma wote mzima, kwa jumla yao Watanzania.
Unapokabidhiwa madaraka ya kutuendeshea serikali yetu, ni vyema pia ukatambua kuwa tuna hiyari ya kukuondoa madarakani kama tulivyokuwa na hiyari ya kukuweka hapo.
Si ustaarabu na pia ni utovu wa shukurani ukatumia nguvu za dola, mbinu na ulaghai uliochanganyika na wizi wa kura na udikteta kuyang'ang'ania madaraka hayo.
Tutapatwa na kichefu chefu, tutapomsikia kwa mfano mtu mzima, akisimama jukwaani mbele ya umma akatuambia tukitaka kumuenzi Mwalimu Nyerere, basi tumchague yeye maana yeye kasimama kwa tiketi ya CCM ambayo Mwalimu Nyerere aliiasisi.
Huu ni ulaghai na kutuchezea akili zetu. Hii ni dharau juu yetu. Hunabudi kujua kuwa Nyerere alikuwa binadamu. Hakuwa sera wala katiba ya nchi. Na zaidi nchi hii sio mali binafsi ya Nyerere. Mgombea atueleze atatufanyia nini na uwezo wa kutufanyia hayo anayotuahidi atautoa wapi. Na kwa nini hukutufanyia hayo katika miaka mitano aliyoongoza au muda wote wa miaka 40 ambayo chama chake kimekuwa madarakani.
Hatutaki kusikia ulaghai wa kusema kuwa tusiwachague wapinzani kwa kuwa hawana sera nzuri. Tunataka utuambie hizo sera zako nzuri zimetusaidiaje katika vita ya kuondoa maradhi, ujinga, umasikini, kukatika ovyo umeme, ukosefu wa maji na mawasiliano mabovu yanayoikabili kanda ya kusini ya nchi hii. Na kwanini mpaka sasa baada ya miaka 40 serikali ya chama chake imeshindwa kuyayaboresha.
Wala uzuri wa sera hauna maana yoyote ubakiapo katika maandishi. Tunataka viongozi watendaji sio wasoma makaratasi ya hotuba. Tunataka kujua sera nzuri wanazotusomea zimetekelezwaje katika hii miaka mitano au 40 iliyopita katika kumneemesha Mtanzania, ukiachilia mbali wale wachache waliopo madarakani na wale wanaowategemea.
Wala hatutaki kusikia serikali bado changa au ilikuwa inakusanya nguvu. Tumechoshwa na nyimbo huo, maana huo ni ulaghai dhahiri. Waliozaliwa wakati tunapata uhuru wetu hivi sasa wanapata wajukuu.
Hatutaki vile vile kusikia mchagueni huyu maana yeye ana serikali ya CCM na mpinzani hana serikali ya kukufanyieni anayowaahidi. Huu pia ni ulaghai, kwa kuwa serikali hii ya CCM pekee, hii ni serikali ya wananchi. Na tunayo madaraka na haki ya kuiambia itufanyie chochote cha kutuletea maendeleo katika jamii yetu. Na tuna uwezo na haki ya kuwapa wapinzani uongozi wa nchi yetu. Kuna ulazima gani wa kuwapa CCM hata baada ya kushindwa kwa miaka 40?
Hatutaki kuona mipango ya maendeleo inasitishwa katika maeneo ambayo wapinzani wameshinda viti vya uchaguzi, kama adhabu ya kutomchagua mgombea wa CCM. Wanaohusika na dhulma za namna hii, wachukuliwe hatua. Na chama chao kipewe adhabu ya kunyimwa kura kwa dhuluma hiyo.
Hatutaki kusikia serikali haina fedha, mpaka tuambiwe kwa nini mamilioni ya fedha yanatumiwa kukarabati Ikulu na nyumba ya Waziri Mkuu, kila mwaka na zisielekezwe kwanza kwenye maendeleo ya huduma za kijamii kwa ajili ya wananchi wa kawaida.
Tena hatutaki kuona fedha za umma au mtu binafsi zinatolewa au zinatumika kwa visingizio vya kutoa zawadi kwenye shule, hospitali, barabara na kadhalika, katika vijiji, miji na kwingineko katika siku hizi zinazoelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Zawadi zote za namna hii, zilizo nje ya mikakati ya maendeleo iliyopangwa hapo awali ni lazima ishukiwe kuwa ni rushwa na ulaghai wa kuwapumbaza wapiga kura wa sehemu zinazohusika.
Watanzania ni lazima tujitawale wenyewe. Ili tujitawale wenyewe, serikali yetu ni lazima iwe yetu wote bila kujali nani amekabidhiwa madaraka ya kuiendesha. Serikali isitawale mahakama. Na Bunge pia halina budi kushika hatamu siyo mtu moja peke yake au pamoja na kundi lake.
Bunge ndio mwakilishi mkuu wa watu wote. Bunge lazima liheshimiwe. Kuliheshimu Bunge ndio kuwaheshimu wananchi waliolichagua.
Mtu mmoja na kundi lake la kisiasa lisiwe na uwezo wa kumtisha Mbunge kwa kisingizio cha kuwa ameingia bungeni kwa tiketi yake. Ikumbukwe waliompigia kura siyo wale tu wanachama wa chama kilichompa tiketi hiyo.
Katiba ndio sheria mama. Tafsiri ya katiba isifanywe kiholela na mtu yeyote ila mahakama tu. Na tafsiri ya mahakama ndiyo ya mwisho. Isiingiliwe na mtu yeyote. National Executive wala Central Committee ya chama chochote cha siasa nchini. Siyo mahakama inasikiliza kesi ya nafaka, mtu anatoa amri ya kumwaga nafaka hiyo, pasipo uamuzi wa mahakama. Wala mahakama zetu zisionekane kuendesha kesi zinazohusu watoto wa "wakubwa" tofauti na zinavyoshughulikia za wananchi wote.
Majaji wa mahakama kuu baada ya kuwa wamechaguliwa, kusiwepo na mtu yeyote mwenye madaraka ya kuwatishia kuwafukuza kazi.
Kwa kuwa Mbunge ndio mwakilishi mkuu wa watu wote, bila kujali ameingiaje bungeni, mtu yeyote wala chama chochote, asiwe/kisiwe na uwezo wa kumtisha Mbunge au kulitisha Bunge lenyewe.
Wananchi, serikali hii ni serikali yetu wote na si serikali ya kikundi kimoja cha watu na wala si ya mtu mmoja peke yake, hata kama akituna vipi na kuunguruma vipi. Ni wajibu wetu kupata haki sawa kwa wote, saa zote na pia kwa yote na yote.
Isipowezekana hivyo na ikionekana serikali inataka kuwa ya watu fulani, basi ni lazima tuichukue serikali yetu kutoka kwa wale tuliowapa dhamana hiyo, kwa kutumia kura zetu kwa namna tunavyotaka sisi na wala isiwe kama wanavyotaka wao. Na tuhakikishe kura zetu hazichezewi na kikundi fulani cha wachache ambacho hivi sasa kinafanya kila lenye kuwezekana ili kirejee madarakani hata kwa kura moja. Tuwe tayari kwa lolote kulinda kura zetu, yaliyotufika miaka mitano au 40 iliyopita siyo ya kuhadithiwa tumeyaona wenyewe kwa macho.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |