ELIMU


Kufundisha Sayansi kwa Kiswahili tija kwa sayansi, Kiswahili na Kiingereza


Na O. Kiputiputi

LENGO la makala haya ni kujaribu kuangalia japo kwa ufupi faida itakayopatikana katika kufundisha masomo ya sayansi, hisabati na teknolojia kwa Kiswahili.

Makala inaanza kwa kuangalia historia nafasi na hadhi ya Kiswahili na Kiingereza katika mfumo wa elimu nchini kabla ya kupata uhuru hadi leo. Aidha, makala itaangalia kwa ufupi sababu za msingi zilizochangia kufanya watoa sera wang'ang'anie Kiingereza kwa zaidi ya miaka 30 sasa licha ya kelele nyingi zilizopigwa na wataalamu wa elimu na lugha juu ya madhara makubwa yaliyosababishwa na utumiaji wa Kiingereza kufundishia katika shule za sekondari.

Kisha makala itaangalia faida inayotarajiwa kupatikana hususan katika kufundisha masomo ya sayansi kwa Kiswahili. Mwisho makala itazungumzia kwa ufupi mambo ya msingi ya kuzingatia kwa waalimu na watunzi wa vitabu vya sayansi, ili kwenda sambamba na kanuni za Kimataifa.

Lugha na Elimu Tanzania

Kabla ya kupata uhuru, shule za msingi ziliendeshwa kwa kufuata matabaka. Kulikuwa na shule za Kizungu, Kiasia na Kiafrika. Licha ya mitaala tofauti, lugha tofauti zilitumika kufundishia kwenye shule hizi. Katika shule za Kiafrika, Kiswahili kilitumika kama lugha ya kufundishia shule za msingi, Kiingereza kilitumika kufundishia shule za kati (darasa la V - VII) na za sekondari. Hata hivyo, Kiswahili kilifundishwa kama somo katika shule za sekondari (Rubagumya, 1999:126).

Baada ya kupata uhuru kulitokea haja ya kubadili mfumo huu na kuanzisha mfumo mmoja wa elimu ya msingi bila ubaguzi wa rangi. Lakini sababu ya pili ambayo ndio inadhaniwa kuwa ilikuwa muhimu zaidi iliyosababisha mabadiliko ya sera ya lugha baada ya uhuru, ilitokana na Azimio la Arusha na sera ya Elimu ya Kujitegemea, ambayo ilikuwa sehemu muhimu ya falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Katika mwaka 1967 iliamuliwa Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia shule zote za msingi. Uamuzi huu ulilenga kufuta ile sera ya ubaguzi ya elimu. (Marrison, 1976: Rubagumya, 1999).

Hata hivyo Rubagumnya (1999) anaamini kuwa msukumo mkubwa ulioleta mabadiliko haya ulitokana na mtazamo mpya wa kimapinduzi na wa kizalendo wa Nyerere juu ya elimu, mtazamo ambao umejikita katika falsafa ya elimu ya kujitegemea (Nyerere, 1968), ambapo ilionekana ni vyema elimu ya msingi itolewe kwa watu wote.

Katika mtazamo huu mpya, elimu ya msingi ilichukuliwa kuwa ina lengo la kuwaandaa vijana ili kuwa raia wema kwa maisha ya vijijini, na elimu hii ilitarajiwa kujitosheleza yenyewe. Hivyo, bila shaka lugha iliyofaa kwa kufundishia ikaonekana kuwa Kiswahili na sio Kiingereza.

Kuanzia katikati ya miaka ya 70, matatizo ya kutumia lugha mbili katika mfumo wetu wa elimu (Kiswahili katika shule za msingi na Kiingereza katika shule za sekondari) yalianza kujitokeza. Kuanzia hapo hadi mwanzoni mwa miaka ya 90, kelele nyingi zilipigwa na wataalamu wa elimu na lugha kuelezea haja ya kubadili lugha ya kufundishia katika shule za sekondari kutoka Kiingereza na kuwa Kiswahili.

Orodha ya wataalamu hawa ni ndefu sana (kwa mfano, soma, Mlama na Materu, 1977; Mvungi, 1974, Mlekwa, 1977, Mochiwa, 1996, Mekacha 1998; Moshi, 1983, Kiputiputi 1989, 1998; Roy Campbell na Quorro 1987 na 1998 na Mdee 1999 n.k.).

Licha ya kelele za wataalamu hawa pamoja na ushauri uliotolewa na Tume ya Rais ya Elimu ya mwaka 1982, bado Kiingereza kinaendelea kutumika kufundishia shule za sekondari hadi leo.

Sera mpya ya lugha

Baada ya mapambano yaliyochukua zaidi ya miaka 30 juu ya lugha ipi inafaa zaidi kufundishia katika shule za sekondari, kati ya Kiswahili na Kiingereza, hatimaye Kiswahili kilishinda mapambano haya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mkutano wa Sera ya Utamaduni ulioitishwa na Wizara ya Elimu na Utamaduni huko Arusha tangu tarehe 24 - 28 Mei mwaka 1999, kati ya maazimio 10 muhimu yaliyofikiwa kwenye mkutano huo kuhusu sera ya utamaduni, azimio la pili lilihusu lugha ya Kiswahili na linasema hivi:

"Lugha ya Kiswahili ipewe hadhi ya kisheria kuwa lugha ya taifa. Aidha utekelezaji wa azma ya kutumia lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundisha shuleni na vyuoni uanze mwaka 2001 na kukamilika mwaka 2011".

Aidha, katika dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 ambayo imetoka hivi karibuni, inaeleza sifa muhimu tano ambazo inabidi zijengwe ili taifa jipya lijalo la Watanzania liwe nazo, nazo ni:

i) Maisha ya hali ya juu

ii) Amani, utulivu na mshikamano

iii) Serikali bora

iv) Jamii yenye kuelimika vizuri; na

v) Uchumi wa ushindani wenye uwezo wa kuleta ukuaji endelevu na faida kadhaa za kugawana (uk. 3).

Kuhusu jamii iliyoelimika vilivyo, dira inasisitiza kuwa:

Tanzania inafikia kuwa taifa ambalo watu wake wametopea mawazo yenye maendeleo na moyo wa ushindani. Sifa hizi zinadhaniwa zinaletwa na elimu na maarifa na ni sifa muhimu zinazowezesha taifa kutumia maarifa ili kukusanya pamoja rasilimali ya taifa hili kuwapatia watu wake mahitaji yao muhimu ya kila siku na pia kuwawezesha watu wake kuwa na sifa kubwa ya ushindani katika uchumi wa ndani na wa kimataifa. Tanzania itasisitiza kuwa ili kufikia uwezo mkubwa wa ubunifu na uvumbuzi, na elimu ya hali ya juu ya kuwezesha kupambana na changamoto itolewayo na maendeleo na kuweza kupambana vilivyo katika soko la nchi jirani na soko la kimataifa, na katika kutambua kuwa ukweli kwamba uongozi wenye ushindani katika karne 21, utategemea kiwango na ubora wa elimu na maarifa (uk. 4) (Tafsiri ni yangu).

Pamoja na kwamba malengo haya yamewekwa kwenye dira ya sasa, lakini sio mambo ya ajabu. Ni masuala ya msingi ambayo kila taifa linabidi lijiweke mkakati wa kufaa kuyafikia. Na malengo haya ndiyo yaliyosababisha wataalamu wengi wa elimu na lugha nchini wagundue kasoro za sera ya lugha na kuanza kuipigia kelele kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, kwani taifa lolote haliwezi kufikia malengo haya muhimu ya maendeleo kama sera ya lugha ya kufundishia inaruhusu lugha mbili zitumike katika mfumo wetu wa elimu, yaani Kiswahili katika shule za msingi na Kiingereza katika shule za sekondari. Kwa hiyo, ili malengo haya yaweze kufikiwa ni lazima serikali ikubali uamuzi wake wa kubadili sera ya lugha kama ilivyofikiwa hivi karibuni. Vinginevyo, matarajio ya dira hii yatakuwa ndoto tupu.

Itaendelea toleo lijalo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook