KUMBUKUMBU ZA MWEMBECHAI


Maprofesa walaani mauaji ya Mwembechai


AN-NUUR Dhulhija 1418, Aprili 24-30, 1998

WAHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wameelezea wasiwasi wao ju ya hali inayojengeka nchini ambapo mateso na mauaji ya kiholela hufanywa na vyombo vya serikali bila kukemewa.

Aidha, wameonesha kusikitishwa kwao na vitendo vya baadhi ya viongozi wa serikali kujiingiza katika masuala ya Misikiti, kutoa amri waumini wenzi wao wadhuriwe, polisi kuwavamia watu waliokimbilia ndani ya nyumba takatifu za ibada kisha kuwaita siasa kali na tamko la Kardinali kuunga mkono mauaji wakati Maaskofu duniani kote wamekuwa wakipigania haki.

Hayo yameyasema katika jopo lililoandaliwa na chama cha wanataaluma wa Sayansi ya Jamii Chuo Kikuu Dar es Salaam - University Political Science Association (DUPSA) kwa kushirikiana na taasisi ijulikanayo kama The Philosophical Club.

Jopo hilo lililofanyika Aprili 17, katika ukumbi wa Nkrumah liliwajumuisha wazungumzaji watano ambo ni Dk. A.F. Lwaitama, Prof. Issa Shivji, Prof. Samwel Maghimbi, Prof. Haroub Othman na Dk. H.M. Njozi.

Akiongea katika jopo hilo, Prof. Shivji alisema kwamba tatizo kubwa watu hawataki kujifunza kutokana na historia. Alisema kwamba mwaka 1976 ilianzishwa operesheni mauaji huko Mwanza na Shinyanga katika operesheni hiyo watu wengi walikamatwa na kuteswa sana.

Katika maelezo yake Prof. Shivji alielezea jinsi mwanamke mmoja Muislamu (jina tunalihifadhi) alivyoteswa mwaka 1976 hadi akalemaa mguu na kupoteza kabisa hisia zake za kike (sex urge).

Profesa Shivji anasema kwamba kilichosikitisha katika mauaji hayo kuna mtu alifuatwa chooni alikokuwa amejificha akapigwa risasi na kuuliwa na mwingine alifuatwa jikoni alikojificha na kupigwa risasi.

Katika mauaji ya mwaka 1976 amesema Prof. Shivji baadhi ya watu walijiuzulu wakiwemo Mawaziri. Mwaka 1986 walijiuzulu pia japo wa ngazi za chini na baadhi ya taasisi kama Chuo Kikuu zilikemea.

Lakini amesema Prof. Shivji kinachosikitisha katika awamu hii watu wanauliwa hakuna hata kauli iliyotolewa kulaani! Watu wote kimya wakati kila leo watu wanafanya semina juu ya haki za binadamu na utawala mzuri.

Kuhusu madai ya vurugu, Prof. Shivji alieleza kutatizwa kwake ni nani hasa alifanya vurugu katika mazingira ambapo mtu anaambiwa na polisi kaa chini anakaa halafu anaanza kupigwa.

Dk. A.F. Lwaitama wa Idara ya Isimu na Lugha za Kigeni alieleza kushangazwa kwake na jinsi vyombo vya habari vilivyopotosha suala la Mwembechai. Alisema wengi wamekuwa wakiandika yale yanayowapendeza watawala au wanayotaka wao wenyewe.

Aidha, Dk. Lwaitama alihoji kwamba inakuwaje serikali iseme haina dini na wakati huo huo inaingilia masuala ya Misikiti. Lakini lililomshangaza zaidi alisema ni kuona wanaoshutumu Waislamu na kutuma polisi wawapige ni viongozi ambao ni Waislamu. Dk. Lwaitama alionesha kusikitishwa kwake kwa hatua ya Kadinali Pengo kuunga mkono mauaji wakati Maaskofu duniani kote hupigania haki za binadamu.

Lakini pamoja na hayo Dk. Lwaitama alionesha pia kushangazwa kwake kusikia kwamba Maimamu wanaotaka kukutana na Rais Mkapa wanakamatwa na kwamba gazeti la AN-NUUR nalo wanataka kulifungia.

Profesa Samwel Maghimbi yeye alitahadharisha juu ya hatari ya kitu alichokiita "fundamentalism". Alisema katika hali za jamii ambapo pana tabaka lile la wenye nacho na wengi wasio na kitu hohe hahe wasio na cha kupoteza ni rahisi kwa hawa wasio kuwa na mbele au nyuma kuingiliwa na siasa kali.

Prof. Haroub Othman yeye alisema anashangazwa kwamba inakuwaje Tanzania ambayo imeyaridhia matamko ya OAU na Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu, lakini bado watu wananyimwa haki hizo.

Alisema hata huko Palestina askari wa Israel wakikabiliana na Intifada ya vijana wa Kipalestina wenye kutumia mawe hawatumii risasi za moto. Kwa hiyo alisema alikuwa haelewi alivyolitizama tukio la Mwembechai kwamba ilikuwa Tanzania au Afrika Kusini zama za siasa za kibaguzi.

Akizungumzia mgogoro wa Mwembechai katika mtazamo wa kihistoria Dk. Njozi H.M alisema kwamba tatizo halianzii Mwembechai bali ni la wakoloni walio Wakristo walipotangaza rasmi chuki yao dhidi ya Uislamu na mikakati ya kuutokomeza.

Alionesha jinsi mtazamo na mikakati hiyo ya wakoloni ilivyoendelezwa na serikali ya Tanzania huru ambapo viongozi wa serikali huahidi kulipa kanisa Katoliki nafasi bora lakini wakati huo huo hutangaza kwamba hakuna kuchanganya dini na siasa na na kwamba serikali haina dini.

Kuhusu madai yanayotolewa kwamba Waislamu wanakashifu Ukristo; Dk. Njozi alisema kwamba awali Wakristo walikuwa wamewabatiza sana Waislamu na haikuonekana ni tatizo.

Lakini Waislamu walipoanza kuhubiri na kuwasilimisha Wakristo ikaonekana ni kuhatarisha amani.

Mwaka 1987 Mwalimu Nyerere alidai kwamba wanaoendesha mihadhara wamechoka na amani. Maaskofu wakalipigia kelele hadi kutoa tamko la kumwaga damu.

Akitoa maoni yake katika jopo lililofurika wasikilizaji, Profesa Chris Peter Maina wa Kitivo cha Sheria, aliungana na Prof. Shivji kuonesha kwamba nchini hapa unajengeka utamaduni wa mauaji ya ovyo akatoa mfano wa mauaji ya Bw. Imran Kombe.

Binti mmoja akitoa mchango wake alisisitiza umuhimu wa kuundwa kwa tume ya uchunguzi juu ya tukio la Mwembechai.

Alisema kwamba japo serikali inadai hakuna haja ya kuunda Tume lakini yenyewe mara inadai ni balozi zinahusika, mara wafanyabiashara, wahuni na kadhalika. Katika hali kama hiyo amesema kwamba ukweli haujajulikana hivyo kuundwa tume ni muhimu.

Mchangiaji mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja alisema kwamba Waislamu wamesaidia kuanzisha mapambano dhidi ya madhalimu na kwamba watawaunga mkono.

Katika kuhitimisha maelezo yake Profesa Shivji alisisitiza umuhimu wa wananchi kutokubali kugawanywa. Alisema watu kakaa kimya na kutokukemea mauaji ni dalili ya kugawanywa.

Aidha, alisisitiza kwamba haki na malalamiko ya wanyonge yasipuuzwe, kwani itafika mahali watasimama kupigania wenyewe.


Hii ndio hali ya nchi yetu


AN-NUUR Dhulhija 1418, Aprili 24-30, 1998
 

MAMA wa Shinyanga (jina tunalihifadhi) anahadithia mateso na madhalilisho ya kutisha aliyoyapata akiwa mahabusu.

"Tulikuwa tumechanganywa - wanaume na wanawake. Tuliingia kwenye jumba la stoo tukiwa tunakimbia. Mimi, kwa kweli nilianguka mlangoni kwenye kizingiti. Wanawake wote waliingia ndani. Tulivyoingia tuliamrishwa kuvua nguo haraka. Halafu tukaamrishwa kujipanga ukutani. Mwanaume mmoja mzee aliyekuwa mbele yangu aliamrishwa kulala kichalichali. Akakubali.

"Mmoja wetu akaamrishwa kumpaka yule mzee maji ya pilipili mdomoni, puani, machoni na kwenye sehemu za siri. Hilo lilifanyika, pilipili ikaingizwa ndani (ya sehemu zake za siri). Aliamriwa asiamame na kwenda pembeni huku akipigwa kila alipopewa amri. Mzee yule alikuwa akilia kwa mwasho wa pilipili na alipigwa ili aache kupiga kelele.

"Ikafika zangu yangu. Niliamrishwa nilale kichalichali. Nikatii amri. Pilipili ikatiwa machoni, mdomoni, masikioni na kwenye sehemu zangu za siri. Maganda na mbegu za pilipili yaliagizwa, na yakasukumizwa ndani ya uchi wangu kwa wingi. Huku chini kulivimba kama mkate. Yule kijana aliyekuwa akinitia pilipili aliamrishwa asokomeze pilipili ndani ya njia yangu ya haja kubwa. Yule mtu alikuwa ni Mhaya. Ilibidi afuate amri. Njiani walikuwepo askari nyumba ya pili lakini walikuwa wamevalia kiraia. Mmoja alikuwa na mapilipili, mwingine alikuwa na fimbo. Walikuwa hawana sare. Niliambiwa niketi chini. Nikakaa. Niliambiwa ninyooshe miguu na mikono yangu. Nikapigwa kwenye sehemu zote za mikono. Kilikuwa ni kipigo kibaya mno. Nilikuwa naulizwa "umepata wapi mali" Jangili we!" Nilipigwa kafimbo kafupi. Nikawaambia jinsi nilivyopata mali yangu. Niliulizwa nilipate Honda. Nikasema niliinunua. Nikaachiwa. Nikarudi kwenye ile nyumba ya pilipili nikiwa napigwa na maaskari njia nzima na nikaamrishwa nichukue nguo zangu, nikazichukua.

Mwanamke yule alimalizia ushahidi wake kwa kusema kwamba:

"Ile operesheni ya Mwangh'ola ilikuwa mbaya sana. Mguu wangu wa kushoto sasa hivi umelemaa na sifaidi tena tendo la ngono. Uke wangu ulikuwa na majeraha kwa miaka miwili na sasa hivi umejaa makovu. Nimepoteza kabisa hisia (hamu) ya ngono".

"Hili tukio la kusikitisha la Shinyanga na Mwanza lilikuwa ndio "Black Hole" yetu ya calcutta. Haipaswi kupotea mawazoni mwetu sisi sote, tusije tukaridhika tu kama tulivyoonekana kwenye matukio ya Mwembechai na kwingineko", ameeleza Prof. Shivji mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipokuwa akielezea unyama huo katika ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu Dar es Salaam.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook