BARUA


Nnauye na propaganda ya kovu la mguu!

Ndugu Mhariri

NI ukweli usiopingika kuwa mabadiliko aliyoyaonesha Rais Benjamin Mkapa hayalingani na jinsi alivyokuwa akiyapokea matatizo ya Waislamu pale Diamond Jubilee. Bila shaka Rais aliyatupilia mbali madai ya Waislamu hasa baada ya kupewa kuhinikizwa na Kanisa hasa Kanisa Katoliki.

Baada ya kusoma "Interview" kati ya mshauri wa kisiasa wa Rais na gazeti la RAI ninaanza kugundua kuwa kumbe wanaomshauri Rais vibaya kuhusu masuala ya Waislamu wapo wengi!

Mhe. Moses Nnauye alipokuwa akihojiwa na gazeti la hilo kwanza alitakiwa kueleza dini yake ndipo alipodai kuwa yeye ni Muislamu safi lakini si Mujahidina!!

Mwandishi alipomtaka atoe maoni yake kuhusu madai dhidi ya dhulma kwa Waislamu nchini ndipo Mhe. huyo alipokuja na propaganda ya kuanzia karne!

Alichofanya kwa mujibu wa gazeti la RAI ni kufunua suruali yake na kuonesha kovu ambalo kwa madai yake linamkumbusha mbali sana!!

Kwa mujibu wa Mhe. Nnauye Waislamu wengi walipokuwa wanatakiwa kwenda shule walikuwa wanakimbia kwa kuhofia kuwa kwenda shule ni sawa na kwenda kula nguruwe!

Mhe. huyo anadai yeye kama Muislamu ni miongoni mwao waliokuwa wakiwakimbia askari wa kikoloni waliokuwa wanawataka waende shule na katika kuwakimbia huko ndipo alipopata kovu hilo la mguu!!

Anachojaribu kutuhadithia Mhe. huyo ni kuwa hakuna dhulma bali Waislamu hawapendi kusoma!! Ninaona hii "propaganda ya kovu la mguu" yaweza kuwa ya kuanzia karne kwa sababu Bwana huyo hajatueleza ilikuwaje hata Waislamu wakati huo wakawa na dhana kuwa kwenda shule ni kula nguruwe kwani ushahidi ushatolewa kuwa ufugaji nguruwe ilikuwa ni stratejia maalum kwenye shule za misheni ili, kwanza kuwazuia Waislamu wasisome na pili hata hao watakaojiunga na shule hizo waiasi dini yao.

Na ninadhani iko wazi ndio sababu hata yeye anaitwa Moses badala ya Mussa ingawa anadai jina si tatizo kwake, lakini kama si tatizo kwanini hakuitwa jina lake la asili la Mussa wakati kwa madai yake baba yake alikuwa Sheikh?

Tukiachilia mbali mambo ya historia ambayo yamejaa propaganda tupu kama hii ya kovu la mguu, Waislamu hivi leo hawawadai wakoloni wawape haki zao bali ni serikali ya CCM. Mbona hazungumzii dhulma inayoendelea sasa maofisini, mashuleni na kadhalika baada yakaribia miaka 40 tangu hao wakoloni waondoke badala yake anatuletea propaganda zilizopitwa na wakati?

Vile vile napata wasiwasi na "Uislamu safi" wa Mhe. huyo kwani angekuwa Muislamu safi asingedai kuwa yeye si Mujahidina!! Tunavyojua sisi Muislamu safi lazima atakuwa anajua tafsiri sahihi ya neno Mujahidina kuwa ni mtu anayefanya juhudi.

Sasa Muislamu safi gani asiyefanya juhudi katika dini yake. Mhe. huyo naona kazama kwenye propaganda za vyombo vya habari ambavyo hujaribu kupotosha ukweli kuhusu ni nani hasa Mujahidina na wala hajaonesha jitihada yoyote kutafuta ukweli.

Hata hivyo, kwa vigezo vya CCM anaweza kuwa "Muislamu safi" ila kwa tafsiri sahihi ya Uislamu Waislamu safi wote huwa hawapati nafasi nyeti ndani ya serikali yake kwani wanauelewa Uislamu wao na wanapenda kuutekeleza kwa vitendo na sio kutuletea hadithi za makovu ya miguu ambazo hazitusaidii Waislamu hivi leo.

Hata hivyo, hatuna budi kumshukuru kada huyo kwani amezidi kututhibitishia kuwa Rais hana mpango wowote wa kushughulikia madai yetu kwani kama washauri wenyewe ambao wanajidai ni Waislamu safi ndio hao ambao Rais akiwauliza kuhusu uhalali wa madai ya Waislamu badala ya kumshauri vizuri wanapalilia ulaji wao kwa kumwonyesha makovu ya miguu tutegemee nini?

Hivyo basi, wakati tukiwakumbuka mashahidi wa Mwembechai tutie nia kuondoa dhulma sisi wenyewe na si kumsubiri yeyote ambaye hayupo. Dawa ni kutumia vizuri sanduku la kura kuwaweka watu wenye ufahamu na si watu wanaopiga hadithi za makovu ya miguu!

Mvungi, A.F.,
Morogoro.



Uasherati ndio unaoongeza idadi ya watu

Ndugu Mhariri

KUMEKUWA na kampeni za kudhibiti ongezeko la watu nchini kupitia taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo fulani vya habari.

Lakini kuna jambo moja lisilosahihi katika kampeni hizo. Wahusika wanadai kuwa familia nyingi zinazaa watoto kiholela. Shutuma nyingi zinaelekezwa kwa wanandoa.

Wakati ukweli ni kwamba watoto wengi wanaozaliwa hivi sasa wanatokana na vitendo vya kujamiiana nje ya ndoa.

Sababu kubwa inayochochea vitendo hivyo ni kudhibiti zinaa dhambi ambayo hata wanakampeni wenyewe, sijui kama wamesalimika nayo ndio maana wanahimiza watu waelezwe kwa uwazi mambo ya uke na ume badala ya kukemea uovu wa zinaa na kuitaka jamii ijiepushe nao.

Pamoja na hayo, mimi bado siamini kama Tanzania imekuwa maskini kwa sababu ya idadi kubwa ya watu. Bali kushindwa kwa sera za serikali kutumia rasilimali zetu ndio sababu halisi.

Tunaweza kupungua na bado tukabakia kuwa malofa. Tangu hapo ukimwi unatosha kabisa kutupunguza kama alivyosema Profesa mmoja wa sayansi ya jamii.

Wazungu hawana huruma na sisi na pengine wanaona ghasia sisi kuwepo duniani. Badala ya kutupatia teknolojia ya kutuwezesha kutumia rasilimali kedekede tulizonazo, wanatupa teknolojia ya kuua vizazi vyetu. Kama tutaendelea na ujinga wa kukopa mawazo yao tutakwisha.

Wingi si hoja, Nigeria ina watu zaidi ya milioni 120 karibu mara tatu zaidi yetu lakini bado imetuzidi kielimu na kiuchumi kuliko ambapo wenzetu wana idadi kubwa ya watu waliosoma kwa maana halisi ya kusoma.

Na kwa kweli pamoja na wao kuwa na mafuta, sisi tuna ralisimali nyingi, kwa ule uchache wetu, tungekuwa na maendeleo makubwa kabisa. Lakini wapi, serikali inashindwa hata kusambaza maji kwa wananchi wake licha ya vyanzo vya maji kuwa bwerere. Sijui hapa napo tusingizie nini.

Tusitafute visingizio, tushughulikie kiini cha matatizo. Na dawa ninavyoipendekeza mimi ni serikali ya sasa ing'olewe madarakani kwa kutumia kura za wananchi.

Mama Akili,
Morogoro.



Tumsaidie Chuki kwa kumtibu

Ndugu Mhariri

SASA ni kumsaidia Chuki Athumani na hivi sasa amelamaa. Mimi nilikuwa na ugonjwa wa mgongo siwezi kukaa mgongo ulikuwa unauma sana huko Dubai, nilikwenda kutibiwa na fedha yangu huko Slovakia. Hapo mwanzo inaitwa Chekoslavakia halafu wakagawanyika Slovakia na Chek-Rep.

Huko Slovakia kuna kijiji kinaitwa Pistany. Kijiji hiki ni hospitali ya walemavu. Watu ambao wana ugonjwa wa kupooza.

Kijiji cha Piestany ni hususan hospitali, watu kutoka Arabuni, Marekani, Ujerumani na kote duniani wanakuja kutibiwa hapo ni hodari sana kwa ugonjwa wa waliolemaa. Mimi nilipona mgongo wangu nilikaa miezi miwili hospitali, hospitali hiyo ndani yake ni hoteli mahala pa kula na kutibiwa, ni hospitali kubwa sana hiyo.

Sasa naomba Chuki Athumani apelekwe kwa haraka akatibiwe. Nawapa uhakika atapona kwa sababu nimeona watu wamepona kama yeye ugonjwa wake, hamtaamini atapona.

Sio tumuone na kumtia katika gazeti tu na kumhurumia, sasa tumpeleke Slovakia, amini msiamini atapona na kumuona anatembea.

Sasa ni kumfanyia michango kwa haraka sana. Siku ya Ijumaa kumchukua yeye binafsi na kigari chake Msikitini kila ijumaa mkapata pesa siku ya Ijumaa ile, mnazibadilisha kwa dola, mnaziweka na Ijumaa nyingine mnafanya hivyo hivyo, na hakika atapata fedha nyingi kwa kumhurumia alivyo.

Na hivyo hospitali ya Piestany nina hakika atapona InshaAllah, sasa sijui katika hospitali hiyo itamchukua miezi mingapi, miezi 6 au mwaka. Hospitali hiyo malazi, chakula na matibabu sio fedha nyingi sana. Mimi miezi miwili nilitoa kama dola 4200 sijui sasa. Lakini nina hakika atapona na atakwenda, mtashangaa.

Mnaweza kumpeleka kwa miezi miwili kwanza kuona matibabu ya hospitali hiyo na mkarudi naye, halafu mumpeleke tena atibiwe. Sio tumuone katika gazeti tu.

Sasa Slovakia Embassy iko Kenya Nairobi, mnakwenda kupata maelezo zaidi na kuhakikisha kuwa anaweza kupona hapo mtaamini, hapo Slovakia Embassy.

Tujaribu mwezi mmoja tu tuone manufaa yake anaweza kupona? Kuna kila namna ya mashine kufanya mguu uwe na nguvu na pia mishipa ikafanya kazi vizuri.

Na tuitumie hii kumbukumbu ya mauaji kumsaidia huyu mtoto sio watu kujazana bila faida yoyote, tukaomba dua na kuondoka huo utakuwa upuuzi. Tujae na tuazimie mambo ya kufanya likiwemo hili la kumtibu huyu mtoto.

Bwana Omar,
D'Salaam


OIC, Radio ni muhimu kwa Waislamu Tanzania Bara

Ndugu Mhariri

NAPENDA unipe nafasi nitoe maoni yangu katika gazeti letu AN-NUUR.

Kwanza, napenda kusisitiza kuwa sasa umefika wakati sio tena wa kuomba tu ila ni utekelezaji wa masuala yetu halafu tuangalie ni nani anayetaka kutuharibia maendeleo yetu katika jamii ya Waislamu, kwani kudai haki ni mojawapo ya ibada.. Nasema hivyo kwa sababu zifuatazo. Waislamu wa Tanzania Bara tumekuwa tukikataliwa haki zetu za kimsingi kwa muda mrefu.

Kwa ushirikiano ulio madhubuti tusiibembeleze serikali hii wakati haitusaidii kitu tuwe na Istiqama tumtegemee Allah (s.w.) ndio Muumba Instansurullah ya nsururkum. Shime alieykum tunaanzia kwa mabalozi, mawaziri, Maamir kote nchini tuhamasishane na tulete mafanikio katika jamii yetu ya Kiislamu ili iweze kufaidika katika nyanja zote.

Hivyo shime Aleykum Jamia wakati ndio huu. Watakaotuchafulia mambo yetu kiutekelezaji tukiwaona tu bora tue nao kama vile wenzetu wa Chechnya, sasa tumechoshwa na tabia ya utawala huu. Viongozi wetu leteni OIC Tanzania Bara na Radio Islamia.

Yusuf Athman Sasya,
Dodoma.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook