Kama yeye wawalevi
Haya haya Islamu, limeshatoka jawabu,
Rais katushutumu, kwa mambo yanotusibu,
Keshazirusha salamu, katika yake majibu,
Kama yeye ni wa walevi, tusemeje kwa vitendo?
Tulotaka tushapata, kazi kwetu masahibu,
Mwaka sasa umepita, tunasubiri majibu,
Tamaa sasa twakata, kwa sheria kuwa bubu,
Kama yeye ni wa walevi, tusemeje kwa vitendo?
Baa hizi kila kona, sheria zimekiuka,
Kafiri kazishehena, Islamu twauzika,
Madhila tunayoona, tangu wazungu kufika,
Kama yeye ni wa walevi, tusemeje kwa vitendo?
Wazee walipambana, madhila kuyaepuka,
Mkoloni kumbana, nchi ikaiepuka,
Sasa tunaudhiana, wazalendo wahusika,
Kama yeye ni wa walevi, tusemeje kwa vitendo?
Baa tusipohujumu, viblani zitafika,
Paka lini Islamu, madhila hayatatoka,
Tusimamishe kalamu, vitendo sasa vyataka,
Kama yeye ni wa walevi, tusemeje kwa vitendo?
M. Mwinyi,
Pangani,
Tanga.
1+1+1=1 kituko!
Nataka kukata shule, lengo kufuta ujinga,
Ndipo nagonga kengele, somo nitoe malenga,
Mje wako na kule, madawati nimepanga,
Mm! fumbo la utatu, hesabu zapiga chenga.
Kileleni sitoanza, vichwa nitaviboronga,
Bora darasa la kwanza, shule msijekuringa,
Ndipo mbele kuangaza, na vidato kuvisonga,
Mm! fumbo la utatu, hesabu zapiga chenga.
Nambieni walokole, nambari mkiziunga,
Jibu ndilo tatu lile! Sabato mtanipinga?
Chambueni polepole, Waroma hoja kujenga,
Mm! fumbo la utatu, hesabu zapiga chenga.
Haya! nyosheni vidole, maswali nimeshatunga,
Mungu anamaumbile, kama ya bwana Dilunga?
Ana miguu na nywele, kichwa kiuno na nyonga,
Mm! fumbo la utatu, hesabu zapiga changa.
Msipige makelele, jibuni sitaki ngenga,
Punje tatu za mchele, au ziwe za karanga,
Moja ni sawa jibule! hapo hamjajigonga?
Mm! fumbo la utatu, hesabu zapiga changa.
Vipi baba awe mwana, mtu akajifinyanga,
Tena mume, Sub-hana! tangu tumboni kichanga,
Kisha waje kulingana, ‘mungu’ mwenye mitulinga,
Mm! fumbo la utatu, hesabu zapiga changa.
Hichi kituko cha kale, beti nazitia nanga,
Sitaki vigelegele, somo nasema nafunga,
Zingatia vipengele, ni hoja sijawazonga,
Mm! fumbo la utatu, hesabu zapiga changa.
Dikupa Dikupatile Dikilema,
Dar es Salaam.
Damu kutiwa mchanga
Piga shaba! Piga yule! risasi wakamtwanga,
Chuki mtoto wa shule, polisi wakamlenga,
Akadhofu maumbile, na pingu wakamfunga,
Damu kutiwa mchanga, wapi yatoka sheria.
Piga yule! muongeze! akauawa Salehe,
Maiti muibuluze, tuwafundishe Masheikhe,
Fukia damu ioze, hakuna kuwasamehe,
Damu kutiwa mchanga, wapi yatoka sheria.
Kile kinywa cha Paroko, chanzo cha haya matanga,
Kaanzisha chokochoko, majungu alikaanga,
Mbona hasakwi aliko, Dola inavunga vunga,
Damu kutiwa mchanga, wapi yatoka sheria.
Vipi wale wauwaji, kizimba hawajatinga,
Kama siyo wakosaji, mbona dola yawakinga,
Wacha waseme majaji, sheria wakizipanga,
Damu kutiwa mchanga, wapi yatoka sheria.
Piga yule! piga shaba! na virungu kutugonga,
Kutupwa kama viroba, katika makarandinga,
Wazee na akina baba, rundo wakasongwa songwa,
Damu kutiwa mchanga, wapi yatoka sheria.
Mwisho kutwita wahuni, dola inapiga chenga,
Masheikh na waumini, inatucheka ujinga,
Ni kejeli si utani, sawa na kutusimanga,
Damu kutiwa mchanga, wapi yatoka sheria.
Idd Kikong’ona,
Morogoro.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |