Iliyosomwa katika 'Khitma' ya Mashahid iliyofanyika Msikiti wa Islamic Centre Magomeni, Jumapili alasiri, Februari 13, 2000
SIKU ya Alkhamis, tarehe 12 Februari, 1998, vikosi vya jeshi la polisi pamoja na askari wa kutuliza ghasia lilivamia eneo la Msikiti wa Mwembechai Jijini, majira ya alasiri na kuuzingira kwa masaa kadhaa kabla ya kuuvamia usiku wa manane na kuwakamata waumini waliokuwemo humo, wakiwemo wazee, wanawake na watoto.
Katika tukio hili, vikosi vya polisi vilivunja milango ya Msikiti, kulipua mabomu ya machozi na askari kuingia ndani ya Msikiti huo wakiwa na viatu miguuni.
Tukio hili lilitanguliwa na kitendo cha askari kumkamata kiongozi wa kikundi cha mihadhara cha Khidmat Da'awat Islamiya, Sheikh Magezi Shaaban Maranda majira ya saa 9:30 Msikitini hapo, na baadaye kuleta vikosi vya polisi kulizingira eneo la Msikiti.
Vitendo hivi vilizua hali ya hofu na wasiwasi ambavyo hatimaye ilipelekea mapambano baina ya raia na polisi baada ya polisi kuamua kuwatawanya waumini kutoka katika eneo hilo. Waumini wengi walitiwa mbaroni baada ya kupigwa sana.
Hali hii ilipelekea viongozi na waumini kuukimbia Msikiti kwa kuhofia usalama wao jambo lililosababisha jamaa ya swala ya asubuhi siku ya Ijumaa tarehe 13 Februari, 1998 isiswaliwe Msikitini hapo.
Kwa bahati waumini kutoka maeneo mbalimbali jijini walifika Msikitini hapo asubuhi ya tarehe 13 kuja kujua hali za Waislamu wenzao. Miongoni mwao akiwepo Bwana Ponda Issa Ponda, Katibu wa Kamati iliyoundwa Msikiti wa Mtoro wakati wa kadhia ya mabucha ya nguruwe 1993. Walivyoiona hali ya ukiwa Msikitini hapo iliyoashiria kuwa hata Ijumaa isingeswaliwa, wakasaidiana kuusafisha Msikiti Ijumaa ikaswaliwa.
Waumini wengi walikusanyika kutoka sehemu mbalimbali jijini pamoja na maeneo ya karibu. Lakini majira ya alasiri, vikosi vya polisi viliuzingira tena Msikiti na kuanza kuwatawanya waumini kutoka eneo hilo. Walifyatua mabomu ya machozi na risasi za moto ambapo hatima yake ni kuuawa kwa waumini kadhaa na wengine kujeruhiwa.
Mpaka leo idadi kamili ya waliouawa haijajulikana japo idadi rasmi iliyotolewa na serikali ni watu wawili. Zaidi ya hawa, mtuhumiwa mmoja alikufa kwa maradhi akiwa mahabusu. Miongoni mwa waliojeruhiwa ni kijana Chuki Athumani mwanafunzi wa kidato cha pili katika kituo cha Al-Haramain, ambaye mpaka sasa amepooza miguu.
Kufuatia matukio haya, jeshi la polisi kwa miezi kadhaa liliendesha msako na kamata kamata dhidi ya waumini na viongozi wa Kiislamu.
Waislamu, wakiongozwa na Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu Tanzania, wamehoji juu ya matumizi ya nguvu ya kuchupa mipaka yaliyofanywa na Jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla wakati wa matukio haya yaliyofikisha mpaka kuua. Waislamu wakadai iundwe tume huru kuchunguza suala hili na kuitaka serikali iwafikishe walioua katika vyombo vya sheria.
Kwa upande mwingine, Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania kwa kupitia wakili Said El-Maamry liliwasilisha maombi yake katika vyombo vya sheria ili uchunguzi wa kisheria ufanyike kuhusiana na vifo vilivyotokea kutokana na kadhia hii (Inquest).
Lakini badala ya serikali kuitikia na kuyafanyia kazi madai haya ya msingi, ilianzisha propaganda na kampeni ya kumsaka Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, wakimhusisha na uchochezi, badala ya kumkamata Paroko Lwambano ambaye ndiye aliyetoa matamshi ya kichochezi yaliyopelekea kadhia hii nzima.
Katika kuhitimisha taarifa hii, Kamati inatamka ya kuwa, katika kadhia hii nzima Waislamu wameonewa kwa namna zifuatazo:
Waislamu kuuawa pasina na sheria;
Serikali kukataa kufuata mkondo wa sheria katika kushughulikia malalamiko ya Waislamu juu ya suala hili;
Serikali kujaribu kuzima mihadhara ya Waislamu kwa kuitikia shinikizo la Kanisa na kwa kutumia mabavu bila kujali mipaka ya sheria;
Kunajisiwa Msikiti na kuvunja murua wa ibada kwa askari kuuvamia, kuvunja, kupiga mabomu ya machozi, kuwapiga na kuwakamata waumini wakiwa humo;
Kudhalilishwa na kunyanyaswa wanawake wa Kiislamu;
Waumini kutendewa vitendo vya kikatili, kinyanyasaji na kidhalilishaji wakati wa kukamatwa na wakiwa mikononi mwa polisi na magereza;
Kufungwa Msikiti wa Mwembechai kwa mabavu kwa wiki kadhaa na serikali;
Waislamu kunyimwa dhamana na hivyo kuwekwa mahabusu kwa muda mrefu bila sababu za msingi;
Viongozi na watetezi wa Waislamu kuandamwa kwa vitisho na shinikizo za mabavu ya Dola.
Mpaka tunavyotoa taarifa hii, jumla ya waumini 33 wanashitakiwa katika kesi tatu tofauti za jinai kuhusiana na kadhia hii. Mawakili bado wanadai shilingi milioni moja na laki tatu (1,300,000) ambazo ni jukumu letu sote kuzilipa.
Kijana Chuki bado anateseka bila matibabu. Na waliodhurika hawajapewa msaada wala fidia ya namna yoyote ile. Na Sheikh Ponda Issa Ponda inadaiwa anasakwa hali ya kuwa walioua wanatembea huru, kadhalika Padre Lwambano.
Kwa hivyo, Kamati Tanzania inapendekeza yafuatayo kwa hadhira hii iliyohudhuria hapa leo kwa ajili ya Dua ya kuwaombea ndugu zetu waliouawa pale Mwembechai:
1. Tuazimie kufungua kesi wenyewe dhidi ya waliowaua ndugu zetu. Aidha tulipeleke shauri hili katika vyombo vya kimataifa. Katika kesi hii tunao mashahidi muhimu walioshuhudia damu, mabaki ya mabomu na uchafu mwingine ulioachwa na polisi ndani ya Msikiti. Aidha, yupo Sheikh Ponda, yeye ndiye aliyewaonesha waandishi wa habari mabusati yaliyojaa damu na vifaa vya Msikiti vilivyodaiwa na serikali kuwa ni mikuki. Yeye ndiye aliyewaongoza waumini kufagia Msikiti na kuswali Ijumaa baada ya polisi kuuteka na kuunajisi jana yake. Kama ni uchochezi kaufanya Padri wa Kikatoliki Lwambano, asakwe na kukamatwa yeye.
Hatukubali serikali ihamishe ajenda katika kadhia hii wala kutupotezea shahidi wetu huyo muhimu. Na tunamtaka atembee kama mtu huru. Sote tunachukua azma ya kumlinda;
2. Tuazimie kufuatilia kisheria mpaka uchunguzi (INQUEST) wa vifo vya Mwembechai ufanyike;
3. Tuazimie kufungua kesi za madai kwa ajili ya fidia ya waliodhurika, kudhalilika na kunyanyasika kutokana na kadhia hii;
4. Tuazimie kujitolea kwa hali na mali ili tumpatie matibabu yafaayo kijana Chuki Athumani;
5. Tuazimie kujitolea kwa hali na mali ili kukamilisha malipo ya mawakili wanaosimamia kesi za Waislamu za Mwembechai; na,
6. Tuitake serikali ieleze ni kwanini haijamkamata Paroko Camillus Lwambano aliyeanzisha huzuni hii na wale askari walioua na waliowaamrisha kufanya hivyo.
WABILLAH TAWFIQ
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |