Na Abul-Ala Maududi
SIFA njema anazistahiki Mwenyezi Mungu pekee na amani iwafikie waja wake aliowateua (mitume).
Baada ya hayo na kabla sijaingia katika maudhui ninayotaka kuizungumza kwenu, napenda kuelezea furaha iliyo moyoni mwangu kutokana na hali ninayoiona katika vyuo vyote vilivyopo katika ulimwengu wa Kiislamu na usiokuwa wa Kiislamu.
Hali yenyewe ni kule kuona kuwa katika vyuo hivyo vipo vikundi vya vijana wazuri ambao nyoyo zao zimepata mwangaza wa itikadi ya dini (ya Kiislamu).
Vijana hao wanayaheshimu majukumu yao hapa ulimwenguni wakiwa kama Waislamu na kwa ajili hiyo wametoa juhudi zao zote katika kuiendeleza itikadi ya Kiislamu katika vituo vya taaluma mbalimbali.
Hili ni tukio ambalo inampasa kila anayeupenda ulimwengu wa Kiislamu aliridhie, aliheshimu na kulifurahia. Kwani hizi ni miongoni mwa fadhila za Mwenyezi Mungu kwa umma huu dhaifu kwamba katika vyuo na vituo mbalimbali vya malezi wanapatikana vijana wanaofahamu wajibu wao na kuutekeleza kwa juhudi na maarifa pamoja na kuwepo fikra na tamaduni za kimagharibi katika mifumo ya malezi na elimu katika nchi za Kiislamu.
Ama maudhui ninayotaka kuzungumza kwenu ni kuwa: Je, ni jukumu lipi linalowapasa vijana, hasa wanafunzi, kulitekeleza ili kuujenga ulimwengu wa Kiislamu?
Hali tofauti, tatizo moja:
Kabla ya jambo lolote, inawapasa mzingatie katika akili zenu kwamba maneno yangu haya yanawahusu wanafunzi katika nchi ambazo baada ya kuwa katika ubeberu wa kimagharibi kwa muda mrefu, na baada ya kushindwa na mataifa hayo (ya magharibi) katika nyanja zote za maisha, (nchi hizo zinazojiita kuwa za Kiislamu baada ya kuwa hivyo hatimaye) zimejisalimisha (tena) mbele ya fikra na ustaarabu wa kimagharibi.
Nyanja zote za maisha ya nchi hizo za Kiislamu ikiwemo ya elimu, zimekuwa zikifuata nadharia na mifumo ya kimagharibi.
Kwa hakika, hali na mazingira ambayo ulimwengu wote wa Kiislamu unavyoishi hivi leo yanafanana na kwa hiyo wanafunzi katika ulimwengu huo wanakabiliwa na tatizo moja:
Taifa la Kiislamu, si nchi za Kiislamu
Jambo la pili ambalo inapasa msilisahau ni kwamba ninaposema nchi za Kiislamu sikusudii mipaka yake ya majimbo, milima, mito au majangwa (mipaka ya kijiografia). Ninachokusudia ni watu wanaoishi katika nchi hizo.
Inaeleweka wazi kuwa watu hutoweka na kwamba kila mmoja ana muda wake maalum wa kuishi.
Kwa hiyo basi, iwapo tunataka ustaarabu, utamaduni na mfumo wetu wa maisha udumu katika nchi hizi, basi hilo halitafanikiwa ila tu tutakapoyabeba kwa uaminifu (mkubwa) yale (mafundisho halisi au sahihi ya dini yetu) tuliyoyarithi kwa wahanga wetu na kuyafikisha kwa vizazi vijavyo.
Si hivyo tu, inatupasa tuviandae vizazi vijavyo ili navyo viweze kubeba amana hiyo na kuifikisha kwa vizazi vinavyofuatia.
Mataifa hudumu na kutoweka
Mataifa ambayo yametoweka ulimwenguni kiasi kwamba hayana athari yoyote, sio kwa sababu ya kutokuwepo kizazi chao, bali ni kwamba maadili halisi ya mataifa hayo hayapo tena kutambulisha utaifa wake.
Kwa mfano, wakati tusemapo Taifa la Babilon (Iraq hivi leo) au Taifa la Kifirauni (hivi sasa Misri) limetoweka tunakusudia kuwa sifa na athari za ustaarabu waliokuwa nao umefutika kama si kutoweka kabisa.
Ama vizazi vya Kibabel na Kimisri bado vipo na vinazaliana, isipokuwa tu ule ustaarabu uliojulikana kuwa ni wa Kibabiloni na wa Kimisri ndio uliotoweka bila kuacha athari yoyote (ya maana).
Hali hiyo ya kutoweka kwa ustaarabu wa Wababel na Wamisri inatokana na kwamba, vizazi vilivyofuatia havikuwa na sifa ambazo zingeviwezesha kuyabeba yale waliyoyarithi kutoka kwa wahenga wao na kuyafikisha kwa vizazi vyao (warithi wao).
Imethibitika kuwa, Taifa lolote likikosa ustaarabu wake wa kitaifa (utamaduni wake ambao ndio kielelezo cha uhai na utashi wa Taifa hilo katika maisha ya kila siku ya watu wake) na likajivika ustaarabu wa Taifa jingine, hiyo ina maanisha kwamba Taifa hilo limetoweka na kupotea kabisa.
Historia nayo inatoa ushahidi kwamba, makabila 12 ya Waisraeli yametoweka kabisa duniani na historia hadi sasa haijayagundua.
Hiyo haina maana kuwa makabila hayo yameangamizwa na kung'olewa mizizi yake duniani, bali kwamba maadili yake ya Kiisraeli yamekufa na hayakurithiwa tena na vizazi vilivyofuatia.
Kutoweka kwa utamaduni wa Kiisraeli katika makabila haya ndiko kulikoyafanya yaingie kwenye mataifa mengine hadi vizazi hivyo hivi leo vimekuwa havijulikani kuwa ni vya Kiisraeli.
Kwa hiyo, kuendelea kwa uhai wa Taifa lolote lile duniani kunategemea maandalizi mazuri na thabiti ya kizazi cha baadaye na kukifanya kiwe tayari kulinda sifa za Taifa lake, kwa kuwa maudhui hii ina umuhimu wake mkubwa, nataka niitoleee ufafanuzi kidogo.
Itaendelea toleo lijalo
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |