JUMUIYA za Kiislamu, kwa pamoja zimetakiwa kuanzisha mfuko utakaotoa mikopo isiyo na riba kwa akina mama Waislamu.
Wakiongea na gazeti hili, baadhi ya akina mama Waislamu wamesema wamekwama kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi kwa kukosa mitaji.
Wamesema, licha ya kuwa yapo mashirika na taasisi zinazotoa misaada kwa akina mama, lakini taasisi hizo zina mitazamo yao na watu inayowapa kipaumbele.
Aidha, wamesema misaada ya taasisi hizo ni yenye riba, jambo ambalo ni tatizo.
Akinamama hao ambao waliongea na Mwandishi wa habari hizi baada ya kumalizika kwa semina yao ya siku nne, wamesema, wanaimani Halmashauri Kuu wana uwezo wa kulitatua tatizo hilo.
Katika semina hiyo, ilielezwa kuwa kukosekana kwa mikopo isiyo na riba imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi ya wanawake wa Kiislamu nchini.
Aidha, kukosekana kwa wataalamu Waislamu wanaojishughulisha na maendeleo ya Waislamu, kunakwaza juhudi za Waislamu wa kawaida.
Wakizungumza katika semina hiyo ya wanawake Waislamu iliyofanyika jijini Dar es Salaam, washiriki kutoka Bukoba, wametoa wito matatizo hayo yatatuliwe ili kuunusuru ummah wa Kiislamu.
"Hatuna wataalamu wa kutosha katika nyanja zote. Tumekosa mikopo isiyo na riba", wameeleza akinamama toka Bukoba wakichambua matatizo yao.
Aidha, ukosefu wa hospitali na zahanati zenye kuendeshwa kwa maadili ya Kiislamu limetajwa kuwa tatizo jingine la kushughulikiwa kwa haraka.
Akina mama toka Songea wamesema, ukosefu wa hospitali zenye maadili ya Kiislamu ni tatizo sugu.
Wamesema tatizo hilo linapelekea kunyanyaswa akina mama na kukiukwa kabisa murua wa Kiislamu katika utoaji wa huduma za afya.
Akinamama walioongea na gazeti hili baada ya semina wamesema Halmashauri Kuu ya Waislamu chini ya Balozi Abbas Sykes, ina wataalamu wa kutosha na uwezo wa kukusanya fedha kutatua matatizo hayo.
Wameitaka Halmashauri hiyo ilitazame kwa makini suala la kuwaimarisha Waislamu kiuchumi na kuboresha huduma za afya.
Semina ya akina mama Waislamu iliyofanyika Msikiti wa Mwenge Februari 9 - 12, 2000, iliwajumuisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Ripoti za harakati za akina mama zilitolewa na kuweka mikakati ya kuziboresha kwa siku zijazo.
Dodoma
wawakumbuka mashahidi wa Mwembechai na kusema:
Hakuna utawala wa sheria
KUKATAA kuwafikisha wauaji mahakamani ni kielelezo kuwa utawala wa sheria haupo Tanzania.
Baya zaidi, serikali imekuwa ikivunja katiba kwa mabavu kwa kuyabariki mauaji na kuzuia uchunguzi.
Serikali imekuwa ikiwaandama waathirika (Waislamu) huku ikiwaacha huru Paroko Lwambano na wale waliofanya mauaji ya kinyama.
Waislamu mjini Dodoma wameyaeleza hayo katika kuwakumbuka wenzao waliouliwa na polisi Mwembechai mwaka juzi.
Ustadh Mussa Said amesema kauli za viongozi wa serikali juu ya mauaji hayo zinakiuka uhuru wa vyombo vya sheria. Aidha, amesema kuzuia kwao uchunguzi na mahakama kufanya kazi yake, ni kuwanyima raia haki zao.
Ustadh Mussa ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Msikiti wa Masjid Ghazal amesema waliouliwa Mwembechai walikuwa raia wema wa nchi hii. Na kubwa zaidi ni Waislamu wenzetu.
Maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya Mwembechai yaliandaliwa kwa kuoneshwa kwa kanda za mauaji yenyewe na ile ya Diamond Jubilee ya Baraza la Idd - el-Fitri iliyowakusanya Waislamu wa Dar es Salaam kutafakari majibu ya Rais Mkapa kuhusiana na kadhia hiyo, ambapo Rais Mkapa alisema suala la Mwembechai ni la wahuni.
Pamoja na kuadhimisha kumbukumbu hizo hapa mkoani, Mkoa wa Dodoma ulikuwa miongoni mwa mikoa iliyoitikia wito kutoka kwa ndugu zao wa Dar es Salaam wa kuwataka kutuma wajumbe (wawakilishi) kuhudhuria kumbukumbu za mauaji ya Waislamu yaliyofanyika Mwembechai, Februari 13, 1998 na jeshi la polisi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |