HUKU Waislamu wakiendelea kuitaka serikali
iwafikishe mahakamani waliochochea, kuamuru na kufanya mauaji Mwembechai,
Jeshi la polisi nchini limetakiwa kutokufanya kazi kwa chuki.
Aidha, jeshi hilo limetakiwa kuwapekuwa watokao Vatican na Italia ambako imedaiwa ni makao makuu ya kikundi cha kigaidi cha Mafia.
Nasaha hizo zimetolewa na baadhi ya Waislamu kufuatia kukamatwa kwa mwenzao Sheikh Said na kupekuliwa na polisi.
Sheikh Said Kambi alikamatwa na kufanyiwa upekuzi kwa tuhuma kuwa anamiliki silaha isivyo halali. Aidha, Sheikh Saidi anatuhumiwa kupata mafunzo yanayodaiwa ya kigaidi kutoka Iran na Sudan.
"Magaidi wamewaona wanaosoma Uislamu Sudan, mbona hawawapekui waliosoma Vatican hao ndio tumesikia wakishiriki mauaji huko Rwanda", amesema Ustadh Mussa.
Ustadh Mussa ambaye ni mwalimu wa Madrasa Kigogo amewatuhumu polisi kufanya kazi kwa chuki.
"Polisi wakipelekewa fitna dhidi ya Waislamu haraka huchukua hatua kuwadhibu au kuwabughudhi bila kufuata sheria. Lakini hatuoni wakifanya hayo kwa Wakristo", alisema mmoja wa ndugu wa Said na kuongeza; "hiki ni kielelezo kingine cha dhulma na kupigwa vita Uislamu. "Vipi mtu kupata fursa kusoma Sudan au Iran iwe nongwa"? alihoji.
Bw. Said Kambi aliwahi kusoma katika Chuo cha Kiislamu - Islamic African Centre kilichopo Khartoum Sudan.
Akielezea kukamatwa kwake; Sheikh Said alisema mnamo Ijumaa ya Februari 11, mwaka huu, majira ya saa 11 jioni, akiwa nyumbani kwake, alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni rafiki yake, Abdallah na kumwambia kuwa yuko dukani kwake anamsubiri.
"Nilipopokea simu hiyo, sikujua kwamba yeye ni askari, lakini nilipofika dukani kwangu asubuhi, nikaambiwa kuwa mtu yule alikuwa ni polisi na kwamba alikuwa akinitafuta mimi", alisema Sheikh Said.
Alisema baada ya kufahamu kwamba alikuwa anatafutwa na polisi, aliamua kwenda kituoni hapo kufahamu zaidi alichokuwa akitafutiwa.
"Nilipofika kituoni hapo niliambiwa kwamba ninatuhumiwa kumiliki silaha isivyo halali na nikaulizwa kama nimepata mafunzo yoyote ya kijeshi kutoka Iran na Sudan", alisema Sheikh Said.
Sheikh Said aliongeza kuwa baada ya kuhojiwa na kuandika maelezo, aliongozana na polisi hao hadi dukani kwake ambako walipekuwa duka na stoo tatu kabla ya kwenda kupekuwa nyumbani kwake, Buguruni.
"Katika upekuzi huo, walidai kuwa wanatafuta tambi za Gruneti, bastola, mabomu na risasi ambazo walidai kuwa ninazimiliki kutoka Iran na Sudan", alisema Sheikh Said.
Akithibitisha kukamatwa kwa Sheikh mbele ya waandishi wa habari katika kituo kikuu cha polisi Jijini wiki hii, Mkuu wa upelelezi wa Makosa wa Jinai Mkoani Dar es Salaam, Bw. Said Mwema alisema kuwa tuhuma hizo dhidi ya Sheikh Said zimepokewa kutoka kwa mtu aliyemwita "msiri wao".
Bw. Mwema alisema hata hivyo, baada ya kumkamata Sheikh Said na kumpekua kazini kwake (dukani) mtaa wa Sikukuu, Kariakoo na nyumbani kwake Buguruni, hawakukuta silaha hizo.
Alisema baaa ya kumshikilia kwa muda wa masaa kadhaa kituoni hapo na kumhoji, baadaye walimwachia.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |