Waislamu 10 wakamatwa Mwanza
WAISLAMU 10 walifikishwa mahakamani
wiki hii kufuatia kufanyika kwa dua iliyowaombea waliouliwa Mwembechai
Jijini Dar es Salaam Februari 13, 1998.
Waislamu hao ni Abubakar Kabunda, Amir Jondama, Abdallah na Ilunga Kapungu.
Wengine ni Ismail Sinani, Abubakar Ayub na Hamduni Malisali.
Katika kundi hilo wamo pia Rashid Mmisi, Abdallah na Ndeki Shaaban.
Waislamu hao kwa pamoja wanatuhumiwa kuandaa kongamano bila ya kibali na kutoa maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi dhidi ya serikali.
Mbele ya Hakimu Machila Mangina, Mwendesha Mashitaka katika kesi hiyo Na. 164/2000 Ispekta Henry Mwenda aliyataja maneno hayo ya uchochezi kuwa ni kusema serikali ya Rais Mkapa inapokea maagizo toka Makanisani hasa Kanisa Katoliki.
Mwendesha mashitaka huyo alidai maneno hayo yangeweza kuleta uhasama miongoni mwa wananchi wa dini tofauti hali ambayo alisema ingeweza kuhatarisha amani.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 25, mwaka huu na washitakiwa wote wako nje kwa dhamana.
Akielezea tukio la kukamatwa kwao, mmoja wa washitakiwa hao Bwana Ilunga alisema waliandaa kongamano ambalo pamoja na mambo mengine iliombwa dua kuwaombea Waislamu waliouawa Mwembechai jijini kufuatia uvamizi wa polisi katika eneo hilo.
Ilunga alieleza kuwa kongamano hilo ambalo lilihudhuriwa na umati mkubwa wa waumini lilifanyika Msikiti wa Tawfiiq uliopo eneo la Igogo mjini humo.
Alisema yeye pamoja na wenziwe walikamatwa majumbani mara baada ya kumalizika shughuli hiyo majira ya alasiri.
Baadhi ya watuhumiwa walidai kuwa walipokuwa mahabusu yalikuwa yakitamkwa maneno na maafisa wa polisi kuwa kongamano waliloandaa lilikuwa ni mkutano wa siasa ambao ungehutubiwa na Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba.
Wakati huo huo, mwanafunzi aliyepigwa risasi na polisi na kupooza katika kadhia ya Mwembechai mwaka 1998 amechangiwa zaidi ya shilingi laki saba kwa ajili ya matibabu na Waislamu mbalimbali walihudhuria khitma Jumapili iliyopita.
Chuki Athumani ambaye alifika kwenye khitma hiyo akiwa amebebwa aliwatia huzuni kubwa waumini hao mara ilipotangazwa kuwepo kwake.
Khitma kwa ajili ya waliouawa Mwembechai iliwakusanya Waislamu wa Jijini na mikoani. Katika khitma hiyo salamu na matamko yaliyolenga kuishinikiza serikali iunde tume ya kuchunguza suala la Mwembechai yalitolewa.
Mhadhiri maarufu jijini Maalim Bassaleh akisoma risala maalum katika hafla hiyo alisema jazba za vyombo vya dola katika kutekeleza maagizo ya Kanisa ndiyo iliyosababisha mauaji ya Mwembechai.
Huku akisikilizwa kwa utulivu na maelfu ya waumini waliofurika katika Msikiti huo ambao unadhaniwa ni mkubwa kuliko yote jijini, Sheikh Bassaleh alisisitiza kutokuwapo kwa kinachodaiwa kuwa ni kashfa katika mihadhara ya Waislamu.
Amir wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi akizungumza katika shughuli hiyo alisisitiza dai la Waislamu la kutokutendewa haki sawa na raia wengine.
Naye Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, Sheikh Ponda alisema ingawa ukweli kuhusu mauaji ya Mwembechai unafahamika serikali imekuwa ikiendesha propaganda dhidi ya wale wanaosimama kuikumbusha wajibu wake.
Sheikh Ponda aliwataka Waislamu wasimame imara ili kuirejesha nchi katika haki na amani ya kweli.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |