Na O. Kiputiputi
WAKATI wa utawala wa Kiingereza, malengo ya elimu ya sekondari nchini yalikuwa kutayarisha vijana wachache ili kuitumikia serikali. Vijana walipewa elimu ya sekondari ili waje kuwa waalimu, matabibu, mabwana shamba na kadhalika. Kwa vile wakati ule lugha ya kazi serikalini ilikuwa Kiingereza, hivyo basi, dhima ya lugha ya Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia ilioana na malengo ya Kiingereza, yaani lugha ya kuendesha shughuli za serikali maofisini. Hali kadhalika, malengo ya kufundisha lugha ya Kiingereza shuleni ili wanafunzi waitumie kama lugha ya kazini mara wamalizapo masomo yao yalikuwa sawa.
Hivyo basi, kwa wakati ule nafasi na hadhi ya Kiingereza ilikuwa juu sana nchini. Wanafunzi walilazimika kujifunza Kiingereza kwa bidii zote, kwani lugha hiyo, licha ya kuwahakikishia kazi nzuri mara tu wamalizapo masomo, ilikuwa pia ni ishara kubwa ya umaarufu; vijana wengi walipenda kujitambulisha na watawala kwa kufahamu lugha yao. Mtu aliheshimika kwa kukifahamu vizuri Kiingereza. Na kwa muda mrefu umahiri katika lugha ya Kiingereza ilikuwa ndicho kipimo cha usomi wa mtu. Mtu aliyeweza kuongea Kiingereza kizuri alipewa hadhi kubwa katika jamii hata kama alikuwa mfanyakazi wa ndani kwa Mzungu. Hivyo wanafunzi walilazimika kujifunza lugha ya pili ili kupata maendeleo ambayo kila kijana aliyahitaji.
Hata hivyo, makubaliano haya kati ya malengo ya kufundisha Kiingereza na malengo ya elimu ya sekondari yalidumu hadi tulipopata uhuru. Baada ya kupata uhuru, wansiasa walifanya mabadiliko makubwa sana. Kwanza katika harakati za kudai uhuru, walitumia lugha ya Kiswahili, na mara baada ya kupata uhuru, lugha ya Kiingereza nayo ikaanza kupigwa vita. Lugha hii ilihusishwa na wakoloni wenyewe na mtu yeyote aliyependelea kuongea Kiingereza aliambiwa ana kasumba ya kikoloni.
Katika mwaka 1967, Kiswahili kikafanywa kuwa lugha ya taifa na lugha rasmi. Hapo hadhi ya Kiingereza ikazidi kudidimia wakati huo huo hadhi ya Kiswahili ikapanda. Hivyo basi ule umuhimu wa kujua Kiingereza ukaanza kupungua kwani haikuwa tena lugha ya kufanya kazi. Vijana walijua wangeweza kupata kazi bila kufahamu vizuri Kiingereza na hata wakishapata kazi lugha ya kazini haikuwa tena Kiingereza. Kwa hiyo umaarufu wa Kiingereza uliendelea kuporomoka.
Kama vile haitoshi, malengo ya elimu ya sekondari yakabadilishwa. Kama ianvosemwa kwenye Essays on Socialism madhumuni ya elimu ya kujitegemea yakawa
..kuhamisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine mkusanyiko wa busara, hekima na maarifa ya jamii, kutayarisha vijana ili kuwa wanachama wazuri katika jamii na kutoa mchango wao mzuri katika kuilinda na kuiendeleza jamii hii (Nyerere Uk. 132).
Kama tunakubaliana na malengo hayo elimu, yaani kuwaandaa vijana ili wawe wanachama bora wa jamii hii na pia waweze kutoa mchango wao katika kuilinda na kuiendeleza jamii hii, ni dhahiri kuwa mabadiliko haya ya elimu lazima yaonekane kwenye mfumo mzima wa elimu. Malengo haya ya elimu hayawezi kufikiwa kwa kutumia lugha ya Kiingereza ambayo ni lugha ya kigeni inayozungumzwa na watu wachache tu chini ya 5% ya Wanzania wote (Schmied, 1988). Ni vizuri sasa elimu ya sekondari ikatolewa kwa Kiswahili lugha inayotomiwa na watu wengi ambapo zaidi ya 90% ya Watanzania wote (Benki ya Dunia, 1988; Rubagumya, 1991). Hebu sasa tuangalie japo kwa ufupi kilichosababisha watoa sera wang'ang'anie lugha ya Kiingereza kwa muda wote wa zaidi ya miaka 30.
Matatizo yaliyotokana na sera ya lugha
Kwa muhtasari Qorro (1997) amehitimisha matatizo makubwa ya aina nne yatokanayo na sera ya sasa ya lugha ambayo ni:
Njia isiyofaa ya kufundisha lugha ya Kiingereza.
Kukosekana kiungo kati ya elimu ya shule za msingi na shule za sekondari.
Ushiriki duni wa wanafunzi wawapo darasani
Athari nyingine kubwa kwa jamii nzima ya Tanzania.
Kama anavyodai Qorro (1997), watu wengi wanaosisitiza Kiingereza kiendelee kutumika kama lugha ya kufundishia, hasa wale waliosoma katika miaka ya 1940 na 1950, wanaamini kuwa wanafunzi wanaweza kujifunza lugha ya Kiingereza vizuri zaidi kama wataitumia lugha hiyo kuwa lugha ya kufundishia, kama ilivyokuwa zile enzi zao walipokuwa shule.
Akipinga mtazamo huu potofu Qorro anadai, licha ya kushuka kwa hadhi ya Kiingereza, zamani lugha hii ilifundishwa na Waingereza wenyewe. Hivyo ilifundishwa vizuri zaidi. Mafundisho mazuri yaliyofanyika wakati ule hayakuendelezwa kwa kizazi kipya. Leo kuna watu wachache sana wenye uwezo wa kufundisha Kiingereza vizuri. Zamani kulikuwa na vitabu vya aina mbalimbali na vya kutosha kufundishia, siku hizi si ajabu kukuta wanafunzi watano au zaidi wakishirikiana kitabu kimoja. Zamani Kiingereza kilikuwa lugha ya kufundishia tangu darasa la tano. Shule nyingi zilikuwa za bweni na hivyo, mazingira yaliruhusu kukuzwa kwa Kiingereza badala ya lugha nyingine (Qorro, 1997:130).
Kwa kuwa wanafunzi wengi hawaelewi Kiingereza, walimu wngi wa shule za sekondari na vyuo hufundisha kwa kutumia lugha zote mbili yaani Kiingereza na Kiswahili. Kwanza hutaja somo kwa Kiingereza kisha mwalimu hufasiri somo hilo kwa Kiswahili ili wanafunzi waelewe. Karibu sehemu kubwa ya maswali na majibu kuhusu somo huendeshwa kwa Kiswahili, ingawa mwalimu huandika mambo muhimu kuhusu somo hilo kwa Kiingereza. Kwa vile wanafunzi hawaelewi vizuri Kiingereza, basi hulazimika kukariri mambo yote muhimu yanayoandikwa na mwalimu na huyarudia hivyo hivyo kwenye mitihani wanapoulizwa. (Qorro 1997:133).
Aina hii ya kujifunza ambayo kwa upande mmoja waalimu wanalazimishwa na sera ya lugha na kwa upande mwingine wanafunzi wanalazimishwa kutokana na uelewa mdogo wa Kiingereza, inaonekana kuna mfarakano kati ya dhima ya lugha na nafasi au hadhi ya lugha hiyo katika jamii hiyo (Soma pia Mdee, 1999).
Itaendelea toleo lijalo
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |