Na Ramadhani O. Malilo, Durban, Afrika Kusini
SHEIKH Ahmed Hoosen Deedat (82) mwana Da'awah maarufu na mhadhiri mahiri wa Kiislamu ulimwenguni katika somo la mlingano wa dini kati ya Qur'an na Biblia, bado anaendelea na shughuli yake hiyo kwa mafanikio makubwa licha ya kuwa kitandani kwa maradhi ya kupooza mwili.
Sheikh Deedat alipatwa na maradhi hayo mwezi Mei, 1996 na kupoteza fahamu. Baada ya kupatiwa matibabu kwa muda wa wiki tatu mjini Durban, alihamishiwa Saudi Arabia katika hospitali ya Mfalme Fahd kwa matibabu ya juu zaidi.
Baada ya matibabu hayo yaliyochukua zaidi ya miezi 10, Sheikh Deedat alipata nafuu kwa kurudiwa na fahamu yake kamili. Lakini viungo vyake kuanzia mikono hadi miguu havikuweza kufanya kazi.
Hata hivyo, hali hiyo haikuwa kikwazo kikubwa kwa Sheikh Deedat kuendelea na shughuli zake huku akiwa kitandani. Hii ni kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kuona, kusikia, kufahamu na kuyaelewa mambo. Pamoja na hayo, Sheikh Deedat pia ana uwezo mkubwa wa kumbukumbu.
Mara tu Sheikh Deedat alipotambua kuwa mimi nimetoka Tanzania, aliniuliza: "Sheikh Aboud Jumbe hajambo?".
Kutokana na hali yake hiyo Sheikh Deedat anatumia mfumo maalum wa mawasiliano unaomuwezesha "kuongea" na hata kufanya majadiliano ya Qur'an na Biblia kati yake na viongozi wa Makanisa mbalimbali, baadhi yao kutoka Ulaya na Marekani wanaomtembelea nyumbani kwake.
Mfumo huo wa mawasiliano ambao anaonekana ameisha uzoea na kuumudu vizuri, unatumika kuwasilisha yale 'yanayosemwa' na Sheikh Deedat. Mfumo huo upo kama ifuatavyo:
Katika ukuta uliopo upande wa kichwani wa kitanda cha Sheikh Deedat, kumebandikwa karatasi ambayo imeandikwa herufi za alfabeti kuanzia A mpaka Z. Herufi hizo zimegawanywa katika orodha ya mistari mitano. Sheikh anaonekana kuwa ameisha zikariri herufi zote kama zilivyo pangwa katika orodha hiyo kwa kila mstari.
Wakati wa mawasiliano , mtu anaewasiliana na Sheikh, huzungumza kama kawaida na Sheikh husikia na kuelewa kama kawaida. Lakini Sheikh anapotarajiwa kujibu, msaidizi wake Sheikh au yule anayezungumza nae, hushika kalamu na karatasi na kumtazama Sheikh usoni. Kisha huanza kumtajia mistari na herufi moja moja kama zilivyopangwa katika ile karatasi iliyobandikwa ukutani nyuma ya kitanda chake.
Anapofika katika mstari au herufi ambayo Sheikh anaihitaji katika kutunga sentensi yake, Sheikh hutoa ishara ya kukonyeza kwa kunyanyua sehemu ya kope za macho yake, na yule anaewasiliana nae huiandika ile herufi iliyoitikiwa na Sheikh.
Kwa mfumo huo, sentensi hutungwa hadi kukamilisha kile kilichosemwa na Sheikh.
Kutokana na uzoefu walionao katika kutumia mfumo huo kwa kiasi cha miaka mitano, wasaidizi wa Sheikh, wafanyakazi, na wana Da'awah wa IPCI (Islamic Propagation Centre International), mwanae Sheikh (Bw. Yusuf Ahmed Deedat), na hata mkewe Sheikh; wote hao wana uwezo wa kufanya nae mawasiliano kwa wepesi mkubwa sana.
Wepesi huo umemwezesha Sheikh kufanya mijadala kadhaa ya kidini nyumbani kwake na watu mbalimbali wakiwemo wachungaji na maaskofu wa makanisa mbalimbali ya Kikristo. Kati yao wamo walioukubali ukweli wa Uislamu na kusilimu.
Awali nilipofika katika ofisi za IPCI mjini Durban ili kuomba fursa ya kumuona Sheikh Deedat, sikutegemea kuwa ombi langu lingelipokelewa kwa urahisi, kwa kujua kuwa Sheikh amekuwa kitandani kwa muda mrefu kutokana na maradhi hayo ya kupooza mwili .
Hofu yangu ilitokana na kufahamu kwangu kuwa, mtu anapokuwa kitandani kwa maradhi hayo kwa muda mrefu, hupatwa na matatizo mengine kama vile maradhi ya ngozi, michubuko au vidonda kutokana na kulala upande mmoja kwa muda mwingi.
Hali hiyo haiwi tu usumbufu mkubwa kwa mgonjwa mwenyewe, bali pia kwa wale wanaomuuguza.
Hivyo ni jambo la kawaida kwa wagonjwa wa aina hii kutopokea wageni wengi, na wanapotokea, wageni hao huwa hawakai kwa muda mrefu na mgonjwa huyo.
Lakini kinyume chake, nilishangaa kuona watu wale wa IPCI wananihimiza kwenda kumuona Sheikh na kunieleza kuwa Sheikh anapenda sana na kufurahia kutembelewa na hata "kuzungumza" na wageni kwa muda mrefu.
Sheikh Deedat anaishi katika mji mdogo uliopo katika kitongoji cha Lotusville Verulam kilomita 30 kutoka Durban.
Nyumba yake si kubwa. Jengo lake ni la wastani, aina ya "bungalow" lililozungukwa na bustani iliyo hai kutokana na uangalizi mzuri.
Chumba alichomo Sheikh Deedat ni kikubwa kilichozungukwa pia na madirisha makubwa yanayopitisha hewa na mwanga wa kutosha.
Anapokuwa hana wageni, Sheikh huangalia TV na kusikiliza Radio. Vyombo hivyo vya habari vimewekwa vizuri kwa sehemu ya juu mkabala na kitanda chake. Wakati mwingine hutazama kaseti kwenye video au kusomewa magazeti na msaidizi wake.
Kitanda cha Sheikh kimetengenezwa kwa teknolojia iliyozingatia hali yake. Kina swichi inayokigeuza katika hali ya kumuwezesha mgonjwa kutizama upande autakao.
Nilifika kwa Sheikh majira ya mchana baada ya Salat Dhuhur. Nilipokewa kwa furaha kubwa na wenyeji wangu akiwemo mkewe Sheikh na msaidizi wake.
Sheikh mwenyewe pia alionekana kuwa mwenye uso wa furaha. "Gari lenu lilipokaribia geti tu, Sheikh aliniambia kuna wageni nje", ni maneno ya msaidizi wake aliyekuja kufungua mlango na kunikaribisha ndani.
Nilisafiri kwa basi toka Durban hadi Verulam, kisha nikakodisha Taxi kuelekea nyumbani kwa Sheikh Deedat. Pale IPCI (Durban) nilipewa anuani kamili na kuelekezwa jinsi ya kufika nyumbani kwake.
Lakini nilipofika Verulam sikupata taabu ya kumuelekeza dereva wa Taxi niliyokodisha. Sheikh Deedat ni maarufu sana na kila mtu katika mji wa Verulam alielekea kupajua nyumbani kwake.
Mimi nimekuwa nikiishi Afrika Kusini kikazi kwa zaidi ya miaka mitano. Nimeishi Cape Town na Johannesburg. Nimeshuhudia jinsi Sheikh Deedat alivyo maarufu katika nchi hii kama vile alivyo katika nchi mbalimbali nje ya Afrika Kusini.
Nilianza kuujua umaarufu wa Sheikh Deedat tangu alipofanya ziara yake Dar es Salaam, Tanzania mwanzoni mwa mwaka 1980, alipoalikwa na wanafunzi wa Kiislamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika semina kubwa iliyoandaliwa na jumuiya ya wanafunzi hao (MSAUD). Wakati akiwa Dar es Salaam Sheikh Deedat alipata pia fursa ya kufanya mihadhara kadhaa katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jengo lililokuwa la Elimu ya Watu Wazima mtaa wa Lumumba na kwenye Msikti wa Ijumaa Kitumbini.
Ilielezwa wakati ule kuwa mara tu Sheikh Deedat alipopokewa na wenyeji wake toka uwanja wa ndege, aliombwa aende akajipunzishe kidogo. Sheikh alijibu: "Nyinyi mnajua, mimi sikuitikia mwaliko wenu ili nije kulala. Nimekuja kufanya Da'awah".
Sheikh Deedat pia anaikumbuka ziara hiyo na akaniuliza kama MSAUD bado wana mwamko wa kiharakati za kuendeleza dini na jamii yao kama ilivyokuwa katika enzi hizo. Aliwasifu viongozi wa MSAUD wa wakati huo kwa kuweza kumualika Tanzania wakati nchi hiyo haikuwa na uhusiano wa kibalozi na Afrika Kusini, na kufanikisha ziara yake licha ya kuwepo vipingamizi kadhaa kutoka kwa viongozi wa Makanisa.
Alimkumbuka pia Mzee Aboud Jumbe Rais mstaafu wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania ambaye pia anasema aliwahi kumualika Zanzibar.
Baada ya ziara hiyo ya Sheikh Deedat mjini Dar es Salaam, hamasa ya wahadhiri wa Biblia iliibuka upya nchini Tanzania.
Mimi ni mwenyeji wa Kigoma ambako kuna historia kubwa ya kufundishwa kwa somo la mlingano wa dini, na harakati za mahubiri ya mlingano wa dini unaotumia Qur'an na Biblia.
Miongoni mwa wanaharakati maarufu waliofundisha masomo hayo Kigoma ni Sheikh Marijani Songoro na Sheikh Mussa. Sheikh Marijani ni marehemu sasa. Yeye aliwahi kuandika na kuchapisha vijitabu kwa lugha ya Kiswahili kuhusu somo hilo huko Mombasa Kenya katika miaka ya 1930 ambavyo vilitumika sehemu mbalimbali ya Afrika Mashariki.
Miongoni mwa vijana wengi wa Kigoma waliohitimu kwa Masheikh hao ni pamoja na marehemu Ngariba Musa Fundi na Bw. Kawemba Ali Mohammed ambao waliibuka na kufanya kazi kubwa chini ya uongozi wa Sheikh (Mwalimu) Abubakar Mwilima.
Tofauti ya harakati hizo za mlingano wa dini ambayo mtu anaweza kuiona kati ya Tanzania na Afrika Kusini, ni kwamba nchini Tanzania ambako hivi sasa kuna vikundi vingi vya Da'awah ya mlingano wa dini, vikundi hivyo havionekani kufanya kazi zake kwa uhuru unaostahili kama ilivyo kwa vikundi vinavyoendesha shughuli hizo huko Afrika Kusini.
Itakumbukwa kuwa viongozi wa Makanisa nchini Tanzania wamekuwa wakilalamika mara kwa mara wakiihimiza serikali kuzuia vikundi vya Waislamu kama vile AL-MALLID, Khidmat na vinginevyo ili visiendeshe shughuli zake.
Aidha, watu wenye kusikiliza mikanda ya mahubiri ya vikundi hivyo nchini Tanzania wamekuwa wakikamatwa au kutishwa na vyombo vya dola.
Huku Afrika Kusini mambo hayo hakuna kabisa. Wala watu wanaosilimu hawabughudhiwi hata na jamaa zao. Kwa kweli Afrika Kusini kuna uhuru wa kutosha wa mtu kuchagua na kuabudu dini aitakayo.
Hali hiyo ndiyo iliyomwezesha Sheikh Ahmed Deedat kuifanya kazi hiyo ya mahubiri kuanzia enzi za ujana wake katika miaka ya 1940 hadi hivi leo, kwa mafanikio makubwa.
Katika ziara yangu ya kumtembelea na kumjulia hali Sheikh Deedat, lipo jambo nililoliona ambalo nisengependa kumaliza makala haya pasipo kulihadithia. Jambo hilo inawezekana si la kushangaza; lakini mimi limenishangaza.
Jambo hilo ni hali ya mwili wa Sheikh Deedat. Licha ya kulala kitandani kwa kiasi cha miaka mitano, mwili wake hauna vipele, malengelenge, michubuko wala vidonda ambavyo huonekana kwa watu wengi wenye maradhi ya kupooza mwili wanapokuwa kitandani kwa muda mrefu.
Mwili wa Sheikh Deedat ni mororo na hauna dalili zozote za matatizo hayo hata katika maeneo ya mgongo na mbavu ambazo huzilalia sana katika muda wake huo.
Hayo niliyathibitisha kwa macho na mikono yangu mwenyewe baada ya wenyeji wangu kuhisi kuwa katika mazungumzo yetu nilionesha hofu ya Sheikh kuwa katika matatizo hayo.
Baada ya kugundua hofu yangu hiyo, mkewe Sheikh hakufanya ajizi ya kumgeuza na kumvua shati ili kunipa fursa ya kuitoa khofu niliyokuwa nayo.
Mbali ya kuwa mororo, mwili wa Sheikh pia ulionekana unajoto la kawaida kwa mtu yeyote asiye kuwa na maradhi ya kupooza. Na alionekana kupata hisia pale alipoguswa viungo vyake kama vile mikono na miguu.
Baadaye, mwanae Sheikh, Bw. Yusuf Ahmed Deedat, alieleza kuwa madaktari walisema Sheikh anakitu kilichoganda na kukata mawasiliano ya mishipa ya fahamu kuanzia sehemu ya nyuma ya shingo yake. Na kwamba madaktari hao walihofu kufanya operesheni ya kukiondoa kitu hicho kwa kuwa huenda kingemwondolea kabisa unafuu aliokuwa nao.
Bw. Yusuf alisema kwamba ingawa huo ndio uliokuwa uamuzi wa wakati huo (1997), hivi sasa kuna madaktari wengine ambao wamekuwa wakifuatilia hali yake Sheikh kwa kutaka kumfanyia matibabu mapya. Hawa wamevutiwa na hali ya Sheikh kuwa na fahamu njema, uwezo mkubwa wa kumbukumbu, mwili mororo na wenye joto na hisia za kawaida. Madaktari hawa wana tamaa ya kumuanzishia aina mpya ya matibabu, kwa kutumia vifaa vya teknolojia mpya ya kimatibabu ya aina ya maradhi hayo.
Lakini wakati watu wanahangaika na hali ya Sheikh Deedat, yeye mwenyewe haonekani kusumbuliwa na hali hiyo. Anaonesha kuipokea hali yake hiyo kwa mikono miwili, na kwa dua iliyomo kwenye Qur'an ambayo aliwaamrisha wasaidizi wake waiweke kwenye fremu na kutungikwa mkabala na kitanda chake; Qur'an 21:83:
Na (mtaje) Ayyubu, alipomwita Mola wake (akasema): "Mimi imenipata dhara, nawe ndiwe Unayerehemu kuliko wote wanaorehemu".
Mbali ya aya hiyo, pembeni, karibu ya kitanda chake, kuna maneno mengine yaliyobandikwa. Haya yanaonekana kuwa ni wosia wake Sheikh Deedat kwa wanaharakati, wana Da'awah na wote wale wanaojishughulisha na masuala ya kutumikia jamii. Wosia huo ni huu:
Mwanadamu ana uwezo wa kufanya mambo makubwa; na wala hakuna kikomo kwa mtu kufanya mambo (mema) ili mradi tu mtu huyo asifanye hayo kwa kujitafutia sifa binafsi.
Nimegundua pia katika safari yangu ya kumtembelea Sheikh Deedat kuwa watu wengi kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni , mbali ya kumtembelea, wanawasiliana nae kwa salamu na dua za kumtakia kheri. Hivyo nimeona bora niwape anuani yake kwa wale watakaopenda kumtumia dua za Eid el Hajj, Muharram na kadhalika:
Sheikh Ahmed Deedat,
49 Trevernen Road,
Lotusville, Verulam 4340
Simu: (27) (32) 5331790, South Africa
au kupitia Jumuiya yake ya IPCI:
Sheikh Ahmed Deedat,
c/o IPCI
124 Queen Street,
Durban 4001,
South Africa.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |