Mkakati wa kuondoa umaskini ni mbinu za kutafutia kura
Ndugu Mhariri
MIMI siafikiani na wale wanaotumia msamiati wa Kiingereza "Poverty Eradication stragegy" kwa sababu, kisarufi neno "Eradicate" maana yake ni kuondoa na mizizi au kwa neno jingine kung'oa.
Kwa maana hiyo, msamiati huo unatafsirika kama "mkakati wa kuondolea mbali umasikini". Kwa mtazamo wangu na naamini wa wengi msamiati huo haushabihiani na mazingira unamofanyia kazi.
Kwa kiwango cha umaskini tulichofikia, si rahisi kuuondoa umaskini kwa jamii yote kwa kipindi cha miaka ishirini na tano ikiwa tu imeshindwa kwa miaka arobaini. Labda tupate serikali nyingine lakini hii ya CCM haiwezi.
Hivyo, kwa maoni yangu, heri ungetumika msamiati huu "Poverty Alleviation Strategy" kwa sababu neno "Alleviate" lina maana ya unafuu. Kwa hiyo, tafsiri ya msamiati huo ni "mkakati wa kupunguza kiwango cha umaskini".
Endapo muujiza utatokea na kutuwezesha kufanikisha mkakati huo, hapo sasa ndipo tutakapostahiki kutumika maneno "kufuta" au "kuondoa" kwani sasa tutakuwa tunapambana kung'oa mizizi ya umasikini.
Baada ya masahihisho haya sasa napenda kuukosoa mkakati wenyewe. Kwanza nasema mkakati huo umechelewa mno. Ni sawa na watu waliotembea kwa mguu kuelekea sehemu ya mbali. Baada ya kuutwanga mguu kwa kilometa nyingi kiasi cha kuchoka na kukata tamaa ya kufika, mkuu wa msafara, badala ya kuwafariji kuwa karibu tutafika yeye anawaambia wenziwe jamani sasa ndio tunaanza safari.
Kitendo cha kutangaza mkakati wa kuondoa umaskini elfu mbili hii tena baada ya miongo miwili na nusu ijayo, kimezidi kuwavunja moyo wananchi.
Wananchi wamesubiri mno na wamepewa ahadi nyingi sana zingine zimo katika ilani ya uchaguzi ya CCM bila utekelezaji wowote. Bado tena wanaongezewa ahadi huku wakiambiwa wao ndio wanaotakiwa kufanikisha mkakati huo.
Kwa kweli wananchi hasa wakulima wamejitahidi mno lakini wamekosa msaada wa serikali.
Hivi leo wananchi wanaolima korosho, kahawa, pamba na mazao mengine wanapoteza ari ya kulima mazao hayo kwa kukosa soko lenye maslahi kwao.
Licha ya kulima mazao hayo yenye soko la kimataifa, hali za wananchi hao bado ni mbaya. Umasikini wao uko pale pale.
Kwa hiyo, kuwataka wananchi hawa watokomeze umaskini na kujiletea maendeleo huku serikali ikibweteka isishughulikie miundo mbinu, pembejeo wala soko lenye faida, ni sawa na kumtaka kinyonga aruke kwenda mwezini wakati huo mwendo wenyewe tu ni wa kusuasua.
Vivyo hivyo, watu wasio na ajira ambao ndio wengi katika jamii utawashirikisha vipi katika mkakati huo, wachangie nini? Na serikali itawasaidia vipi?
Nina wasiwasi, mkakati huo unalenga zaidi katika maslahi ya kisiasa kuliko ya kiuchumi. Hii ni mbinu nyingine ya CCM ya kutafuta kura za walalahoi.
Wananchi tuwe makini sana, wakati wa kupewa ahadi hewa, mikopo na misaada ya kuturubuni umefika. Tulidanganywa hivi hivi mwaka 1995 na moto tumeouona, sasa ole wetu CCM ishike tena madaraka miaka mitano ijayo.
Mwenye sikio la kufa lisilo sikia dawa shauri yake tena. Wewe msaada au mkopo chukua lakini kura yako usimpe mgombea wa CCM na hakuna mtu atakayekuona.
Hebu safari hii tuwape kura zetu wapinzani walioungana na tuwaepuke wale wabinafsi wasiotaka muungano wa vyama. Hao lengo lao ni kugawanya kura zetu ili CCM ipite walau kwa kura mbili tatu.
Mtego walioutega CCM kupitia badiliko la katiba kujitafutia nafasi ya kushinda japo kwa kura chache, nina hakika, unaweza kuwanaasa wao wenyewe iwapo wapiga kura tutakuwa na nguvu moja.
Hivi sasa CCM ipo kwenye kitanda cha buriani, tuhakikishe tunaizika Oktoba kwa kumpa kura zote mgombea atakaewekwa na vyama vilivyoungana ambao tumeona msimamo wao bungeni dhidi ya muswada wa mabadiliko ya katiba.
Batuli Hussein,
Morogoro.
Mtwara, Tanga na Kigoma tumeumizwa na siasa za udini za CCM
Ndugu Mhariri
Miji ya bandari katika nchi nyingi duniani ndio huwa mbele kimaendeleo kutokana na shughuli za kiuchumi kupitia bandarini. Kwa maneno mengine miji hiyo ndio vitovu vya maendeleo ya Taifa.
Lakini jambo la kushangaza na kusikitisha hapa Tanzania miji ya bandari ndio iko nyuma kabisa kimaendeleo ukiondoa Dar es Salaam.
Licha ya kuwa na bandari, hali za kiuchumi katika miji ya Mtwara, Tanga na Kigoma ni mbaya mno hadi kuwafanya wananchi hasa vijana waikimbie miji yao hiyo. Vijana wengi wa kusini wanalazimika kukimbilia Dar es Salaam kuuza vyombo na vinasamu ili wapate japo hela ya kula.
Si bahati mbaya iliyoiangukia miji hiyo bali ni sera za udini za CCM kwa shinikizo la Kanisa Katoliki ndizo zilizoididimiza miji hiyo.
Baada ya wakereketwa hao wa siasa za udini kufanya sensa na kuona Waislamu ndio wengi katika mikoa hiyo, wakaona kuiendeleza miji hiyo kutainua Uislamu na Waislamu jambo ambalo Vatican haitaki hata kulisikia.
Serikali ya awamu ya kwanza ndiyo iliyoanzisha kampeni za udini za kuiangamiza kiuchumi mikoa hiyo. Iweje mkoa kama Mtwara wenye zao kuu la biashara korosho ukawe duni hata kukosa barabara miaka yote?
Sasa mengi yemekwishasemwa, lililobaki ni jukumu la wananchi wa mikoa husika kutumia haki yetu ya kidemokrasia na kujikomboa kwa kura zetu.
Kwa faida yetu, ni heri tuchague chama kitakachoongoza nchi bila kujali dini ili na sisi tuingizwe kwenye mtandao wa maendeleo.
Mpenda haki,
Mtwara.
Mwembechai iwe 'anuani' ya dhulma
Ndugu Mhariri
KATIKA kipindi cha ukoloni wazee wetu walijitoa muhanga kupambana na dhulma hii hadi mkoloni akaondoka.
Baada ya mkoloni kuondoka wazee wetu walidhani kuwa tayari adui ameshaondoka na kwamba sisi wajukuu zao tutaishi kama raia wengine katika nchi hii.
Wazee waligundua kuwa dhana zao zimeruka patupu baada ya kung'amua kuwa wakoloni waliandaa Waafrika wa kuendeleza dhulma dhidi ya Uislamu na Waislamu. Na cha kusikitisha walioandaliwa walikuwa wabaya zaidi ya walimu wao wakoloni.
Waliunda serikali na kuweka mikakati ya siri na ya kujificha sana ya kumdhulumu Muislamu katika nyanja zote. Hatimaye leo Waislamu wamekuwa majeruhi wa mikakati ya makafiri katika nyanja zote, na kila kukicha makafiri (wasio Waislamu) wanatafuta njia mpya ya kudumisha dhulma huku wakiwa wametia pamba masikioni, hawasikii chochote kutoka kwa Waislamu.
Uzoefu unaonesha kuwa anayedhulumu huwa haachi mpaka anayedhulumiwa aamue kivitendo kukataa kudhulumiwa. Na katika hili Waislamu tunatakiwa tuielezee dhulma tunayofanyiwa kupitia serikalini, katika sehemu zote nchini na nje ya nchi hadi ieleweke barabara mpaka kwa watoto wa darasa la kwanza ili tuanze kuingia katika utendaji.
Na katika kuielezea dhulma hii tukio la Mwembechai linatakiwa liwe ndio "ANUANI" ya kuwaitia watu. Kwa tukio hili tutafanikiwa sana kwani linaonesha kilele cha dhulma, na kwa bahati nzuri tukio hilo limerikodiwa katika kanda za video.
Hivyo Waislamu popote pale walipo wahakikishe wanapata mkanda wa video wa mauaji ya Mwembechai na mkanda wa video wa Ustadh Pona unaoelezea tukio la mauaji katika ufasaha wake ili tuelimishe ummah.
M. Mwinyi,
Pangani,
Tanga.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |