MASHAIRI


Imesemwa kweli

Salamu Alaykum, ndugu zangu Islamu,
Dhulumani mmedumu, tangu ya kwanza awamu,
Kafiri kawahujumu, maisha kwenu magumu,
Imesemwa kweli, utawala tuung’oe.

Si shule sio kazini, ummah hauonekani,
Wakiuza mitaani, virungu watabaini,
Waislamu jamani, wamejaa gerezani,
Imesemwa kweli, utawala tuung’oe.

Mkihubiri Jangwani, kibali tawanyimeni,
Mkifanyia kumbini, dola tawazungukeni,
Mkija Msikitini, Paroko tawafitini,
Imesemwa kweli, utawala tuung’oe.

Wakiwataka nyumbani, usiku watawajia,
Mukowa mahabusini, meno watawaumia,
Mukifika gerezani, hasira tawamalizia,
Imesemwa kweli, utawala tuung’oe.

Waloua kujifunga, si jambo la kutabiri,
Mipango waliipanga, mauaji yakajiri,
Pongezi wakazipanga, na kuzidisha jeuri,
Imesemwa kweli, utawala tuung’oe.

Haya haya Oktoba, dhalimu atutambue,
Alofanya sio haba, Islamu tutambue,
Kina kama kina baba, hili mwapaswa mujue,
Imesemwa kweli, utawala tuung’oe.

M. Mwinyi,
Pangani,
TANGA.



Akaaa!

Nani wa kujitokeza, mabegani alibebe,
Gwanda linalochukiza, eti apigie debe,
Kwetu aje kuliuza, pesa apate ashibe,
Akaa! kivazi cha ..., wateja tunakataa.

Twakijua ni cha ..., lengo waje watuibe,
Hiyo ndiyo yao kazi, tujifiche kama kobe,
Wakija na lao vazi, akili wasituzibe,
Akaa! kivazi cha ..., wateja tunakataa.

Hadharani tuwaseme, vinywa tuwakate ngebe,
Tuwachemshe waheme, tupu wakute mikebe,
Wachukie walalame, na matonge yawakabe,
Akaa! kivazi cha ..., wateja tunakataa.

Yeyote awe dalili, Joni au bwana Shebe,
Hakiwi kwetu halali, japo afanye ubabe,
Hata wa nchi za mbali, kama Rais Mugabe,
Akaa! kivazi cha ..., wateja tunakataa.

Hatu... waungwana, kuhadaika kwa debe,
Na ... tukaungana, tenda kuwapa washibe,
Wauwe na kujichana, haki za watu waibe,
Akaa! kivazi cha ..., wateja tunakataa.

Wateja tunakataa, na kuweka kauzibe,
Kufuga kundi balaa, mitaani watukabe,
Wauwe kama vichaa, wa vitani Entebe,
Akaa! kivazi cha ..., wateja tunakataa.

Idd Kikong’ona,
Morogoro.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook