Kasumba inakwamisha Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia


Na Prof. M.M. Mulokozi
TUKI, Chuo Kikuu, Dar es Salaam

TATIZO la 'kasumba' lipo, ingawa siku hizi halizungumzwi. Hili ni tatizo la Mwafrika mweusi duniani kote. Chanzo chake ni kutawaliwa kisiasa, kitamaduni, kiuchumi, kielimu na kadhalika. Hili ni tatizo kubwa kuliko tunavyodhani, na sidhani kama tunafanya juhudi ya kutosha ya kupambana nalo. Mathalan, katika dunia ya leo ni Mwafrika pekee anayeikataa rangi yake na kujitahidi kuichubua ili kupunguza weusi, ni Mwafrika pekee anayekataa lugha yake ya asili, mavazi, teknolojia, hata majina ya kabila au taifa lake, na kukimbilia kuiga mambo ya wengine. Tatizo hili ni la kiitikadi na kisaikilojia na haliwezi kutatuliwa bila mapambano makali katika nyanja zote za ngazi zote za utamaduni, elimu, falsafa, lugha, burudani, sanaa na hatimaye siasa na uchumi.

Mtanzania mwenye kasumba hawezi kukuza Kiswahili, na lazima atapendelea Kiingereza kwa sababu anaamini kuwa kuongea Kiingereza ndio kuelimika, kuendelea au kustaarabika. Neno 'kustaarabika' halina maana ya kuwa kama Mzungu tu, bali lina maana ya kuwa kama Mwafrika pia. Kwa bahati mbaya, mtu mwenye kasumba aghalabu huiga mabaya badala ya mazuri kutoka kwa 'bwana wake', na yake mazuri huyaacha na kubakiza yale mabaya.

Kasumba inatufanya tuwe waoga na tusijiamini. Ndio maana viongozi wetu na wasomi wetu walio wengi wanathubutu kutamka kuwa haiwezekani kutumia lugha ya Kiafrika kufundishia, maana baadhi yao wanaamini kwa dhati kuwa Mwafrika 'ni duni' na hivyo lugha yake pia ' ni duni'. Njia pekee ya kufuta uduni huo ni kujaribu kwa kila hali kuwa kama "mzungu" au "mwarabu" au "Muhindi".

Tatizo la kasumba upande wa lugha tunaliona katika msimamo wa baadhi ya watu wenye madaraka ya kufanya maamuzi, ambao wanakataa kabisa kukubali Kiswahili kitumike kufundishia kwa madai kuwa "hakijakomaa" na "hakitakomaa" au kwa visingizio vya umataifa, kuwania teknolojia, ukosefu wa fedha na kadhalika.

Tatizo hili tunaliona shuleni ambako leo hii, mwaka 2000, watoto bado wanapigwa viboko kwa sababu ya kuongea Kiswahili au lugha zao za kikabila katika eneo la shule. Tunaliona miongoni mwa wanafunzi (na hata wazazi) ambao hawezi kuongea sentensi moja sahihi ya Kiingereza lakini bado wanataka wafundishwe kwa lugha ya Kiingereza. Yaani wako radhi kuikosa elimu kwa sababu ya kutojua lugha inayotumika kuliko kuipata kwa lugha yao ya taifa ambayo wanaifahamu vizuri!

Mwenendo wa sasa ulimwenguni ambao tumeiuita "utandawazi" (globalization) unasaidia kushadidia kasumba ambayo tayari tunayo.

Utandawazi kwa Mwafrika si "kutandawana" bali ni "kutandawazwa" , sisi tunakokotwa tu kuingiwa kwenye ulimwengu na utamaduni wa wengine, hususan wa Magharibi, na hatutakiwi kuchangia chochote katika kuumba ulimwengu mpya wa teknolojia na kitamaduni. Ndio maana tunashabikia "Manchester United" badala ya timu za nchi kama China au India, tunafurahia burudani kutoka Hollywood na Ulaya na kufuatilia kwa makini habari za kashfa za wanasiasa na wababe wa huko badala ya habari za kwetu, tunatumia silabasi za Kiingereza kufundishia watoto wetu katika "akademia" za bandia badala ya kutumia silabasi za Kitanzania, au angalau za nchi zilizoendelea zaidi kiteknolojia kuliko Uingereza, tunapokea na kushabikia wahubiri wa dini wa madhehebu ya kila aina kutoka Ulaya na Asia, lakini hatujiulizi kwa nini wahubiri Waafrika wa dini zetu, hawashabikiwi sana huko Ulaya na Asia. Tunafurahi na kujivunia miundo mipya ya magari kutoka Japan, Ulaya na Korea wakati sisi wenyewe hata kiwanda chetu cha baiskeli tumeshindwa kukiendesha na kuishia kukiuza kwa wageni.

Kwa ufupi, kila Mwafrika wa leo ana kiasi fulani cha kasumba. Kwa bahati mbaya, wale walio katika kazi za uongozi mara nyingi ndio wenye kasumba zaidi kwa sababu ya mazingira yaliyowakuza, elimu waliyoipata, mtindo wao wa maisha na nafasi walizo nazo. Kwa kuwa watu hao ndio waamuzi wa masuala ya sera, ikiwemo sera ya lugha na utamaduni, ni wazi kuwa kasumba yao ni kipingamizi kikubwa cha utekelezaji wa sera ya lugha ya kufundishia.

Kasumba ya wakubwa mara nyingi hufungamana na tatizo la ujuaji. Kwa kawaida viongozi wa kisiasa na kiserikali wakitaka kufanya maamuzi kuhusu jambo zito la kisera huwasiliana kwanza na wataalamu wa nyanja inayohusika na kupata ushauri wao. Lakini katika suala la lugha kila kiongozi ni mtaalamu, hawapendi na hawatafuti ushauri wa wataalamu wa kweli wa uwanja huo, ambao ni wanaisimu na wanataaluma wa elimu. Ujuaji wao unachukua nafasi ya ujuzi.

Ni wazi kuwa tunahitaji kuwa na ibara za kisheria kuhusu matumizi ya lugha hapa nchini, kuanzia katika Katiba ya nchi, hadi katika sheria zinazohusu shughuli na vyombo mbalimbali vya umma na vya binafsi, yakiwemo mashirika, shule, vyombo vya habari, shughuli za biashara na kadhalika. Mathalan, liwe ni kosa la jinai kwa mtu kusambaza nchini Tanzania bidhaa isiyokuwa na maelezo katika lugha ya Kiswahili kwenye ganda lake. Sheria kama hiyo si muhimu katika kutunza heshima ya taifa tu, bali pia ni muhimu kwa usalama na uhai wa walaji.

Itaendelea toleo lijalo
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook