Jinsi ya kujenga imani ya kweli hadi kuufikia ucha Mungu


KWA msukumo wa silka yake, mwanadamu anawajibika kutambua na kutenda haki zinazogawanyika katika sehemu kuu tatu. Mosi, haki za Muumba wake. Pili, haki za nafsi yake na tatu haki za wanadamu wenziwe ambao hujumuishwa na kuitwa jamii. Ijapokuwa zipo pia haki za viumbe wengine lakini hapa tutazitazama aina hizo kuu tatu za haki. Mwandishi S. HUSSEIN anaelezea zaidi.

Haki za Muumba

AWALI ya yote, mwanadamu anatakiwa kumjua na kumuamini ipasavyo Muumba wake kwa kuziangalia ishara zote za kuwepo kwa Muumba huyo. Miongoni mwa nyenzo za kumuwezesha mtu kuziona ishara hizo ni akili ambayo kwa kuitumia vyema, huzaa tafakuri, udadisi, hoja, maarifa, utambuzi yakinifu na itikadi.

Mambo haya kwa pamoja humsukuma mtu kufanya utafiti ambao hatimaye huzaa imani thabiti. Wanasayansi kama Bwana Issac Newton waliweza kuamini kuwa dunia hii ina Mmuumba kutokana na utafiti.

Kwa utundu wake wa kisayansi, mwanasayansi huyo mashuhuri aliwahi kutengeneza sesere (sanamu) la kundi la sayari ikiwemo dunia yetu. Sanamu hiyo ikawa inazunguka mithili ya vile zinavyozunguka sayari hizo.

Kisha akamtania rafiki yake aliyekuwa akipinga kuwepo kwa Mungu, kwamba kisanamu hicho kimetokea chenyewe tu pasi na mtengenezaji. Yule Bwana mpinga Mungu akabisha kwa kumwambia Newton asimfanye yeye mjinga! Hapa akimaanisha kuwa haiwezekani kisanamu hicho kijitengeneze chenyewe.

Ndipo Newton alipomrudi jamaa huyo kuwa, vipi akatae kuwa sanamu ile haiwezi kujifanyiza yenyewe na wakati huo huo asiamini kuwa dunia hii ina Muumba!

Ni sawa na mtu anayekubali kuwa lile sanamu la Bisimini halikujitengeneza wala kujiweka lenyewe pale Posta (Dar es Salaam) halafu mtu huyo huyo akubali kuwa yeye katokea tu hapa duniani, hana Muumba!

Ama mwingine akatae kuwa taa za barabara zimejitengeneza na kujiwasha zenyewe lakini yeye huyo huyo aamini kuwa jua, nyota, mwezi vimejiumba na kujiwekea utaratibu wa kuzunguka vyenyewe. Utaratibu huo si tu ni muhimu kwa maisha ya viumbe vya dunia hii bali laiti ungelikuwa na hitilafu ndogo tu basi maisha hayo ya viumbe yangeangamia. Kweli inayumkinika kuwa jua, mwezi na nyota vimejiweka vyenyewe? Ni wazi kuamini hivyo ni kuifuja akili.

Yeyote anayetaka kumjua na kumuamini Mungu ipasavyo, anapaswa kuyatafakari maumbile kila wakati. Ajihoji maswali ya kawaida tu kama vile:

Je, ni mwanamahesabu gani aliyeweka utaratibu wa usiku na mchana kwa masaa yanayolingana? Je, usiku usingekuwepo maisha yetu yangekuwaje, na je mchana na usingekuwepo maisha yetu yangekuwaje?

Dunia yetu ina vitu vya rangi mbalimbali za kuvutia machoni, sasa jiulize, kama tusingekuwa na macho, mvuto huo wa rangi tungeupata vipi?

Binadamu hupenda sana nyama kama vile ya kuku lakini nyama hiyo inahitaji kukatwa na kutafunwa, ili ile ladha ipatikane kinywani, jiulize tusingekuwa na mdomo na meno ya kukata na kusaga, nyama hiyo tungeila vipi?

Mtu anapopata homa na hasa malaria, mdomo huwa mchungu yaani hupoteza ladha na hamu ya kula, hebu jaalia kama hali hiyo mdomoni ingekuwa ya kudumu hata tuwapo wazima, ulaji wetu ungekuwaje?

Vyakula vya wanadamu vyahitaji kuhifadhiwa kwa usalama wa afya zetu. Sasa angalia machungwa, ndizi, embe, mananasi, mapeasi, machenza, embe ng'ongo, mapapai, mapera na matunda mengine kama yasingevishwa maganda yasingekuwa salama kwa afya zetu kwani yangeshambuliwa na wadudu. Sasa nani aliyefanya kazi hiyo muhimu kwetu?

Mtazame mtoto anapozaliwa, anakuta chakula chake yaani maziwa ya mama yameshaandaliwa bila jitihada za mama yake na yeye mwenyewe mtoto anakuwa na tabia ya kunyonyanyonya bila kufundishwa na mtu. Na chuchu za mama zimechongoka kwa saizi ya kutosha kuingia kwenye kijimdomo cha mtoto. Jiulize fundi gani alofanya kazi hii.

Ili tuweze kuelewa na katika mazungumzo yetu ambayo ni muhimu kwa maisha yetu, tunahitaji midomo, ulimi, sauti na masikio. Jiulize kama tungeweza kusema halafu tusiwe na masikio au tungekuwa na masikio halafu tusiwe na mdomo au sauti, mawasiliano yetu yangekuwaje. Na kama ni mawasiliano ya ishara, je, tusingekuwa na macho, yangewezekanaje. Jiulize ni mtaalamu gani aliyefanya kazi hii muhimu?

Fikiria kama wanadamu wangelikuwa na jinsia moja ama wanaume watupu au wanawake watupu, ulimwengu wa watu ungekuwapo kweli? Jiulize nani aliyetutofautisha kijinsia na kutupa matamanio ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya maisha yetu?

Vivyo hivyo, fikiria wanyama kama ng'ombe, mbuzi, kondoo na hata ndege kama bata na kuku wangekuwa na jinsia moja yaani mafahari, mabeberu na majogoo watupu au makoo na majike watupu wangewiana vipi na mahitaji yetu, ikizingatia kuwa nyama, maziwa na mayai yao ni muhimu kwa maisha yetu sasa nani aliyeumba kiume na kike ili wanyama na ndege hawa wazaane kwa faida yetu?

Hebu vunja yai la ndege yoyote yule likiwa bado halijaatamiwa, utakachokiona ni maji ya udenda na kiini cha njano. Sasa chunguza kwa makini na hata kwa darubini kama utaweza kuona kichwa, macho, pua, mifupa, miguu, tumbo, manyoya, maini, figo, paja, utumbo, filigisi, mdomo, ulimi, mbawa na vidole.

Jiulize viungo hivi vinatokeaje katika yale maji ya ute na vinawezaje kujipanga kwa mpangilio bora unaotupatia kiumbe kinachojitengeneza. Na jiulize pia, yule ndege (mtetea) alijuaje kwamba akiatamia mayai yake kwa kipindi fulani atapata vifaranga ambavyo huvitunza kwa mapenzi kwa msaada wa mbawa zake?

Kuku hahitaji kufundishwa ili kujua kuwa mwewe ni adui wa vifaranga vyake na vifaranga hujihami hata bila kufundishwa kuwa mwewe ni adui. Kinyume na ile nadharia ya kijamaa wanayofundishwa watoto wa shule ya msingi kuwa uadui wa kuku na mwewe ulianza pale kuku alipomla buibui ambaye alikuwa njiani kwenda kuwatibu watoto wa mwewe waliokuwa wagonjwa.

Jaribu kumtazama buibui uone kama kweli anaweza kufanya shughuli ya uganga. Je, inaingiaje akilini kweli kuwa buibui anaweza kubeba mkoba wa dawa. Ni dhahiri hadithi za aina hiyo zililenga kuwatoa watoto katika itikadi ya kumuamini Mungu Muumba. Na badala yake waamini kuwa dunia hii haina Muumba!

Mtazame Panya, jiulize kwanini akimuona Paka anakimbia na kujificha. Mbona hakimbiii na kujificha akimuona mbuzi. Na Panya hujua kuwa Paka ni adui yake hata akimuona kwa mara ya kwanza tokea azaliwe. Hahitaji kufundishwa na mama yake. Nani kamfundisha jambo hilo ambalo ni muhimu kwa uhai wake.

Mtazame naye nyoka, kwanini akimuona nguchiro ananywea na kujificha kichwa chake, mbona akimuona sungura haogopi. Na kweli nguchiro ni hatari kwa maisha yake. Na nyoka hujua hatari ya nguchiro hata kama ni mara yake ya kwanza kukutana naye. Nani aliyemfundisha hivyo?

Pia muangalie swala jiulize kwanini hamuogopi tembo ambaye ni mkubwa na badala yake anamkimbia simba, jambo ambalo ni sahihi kwa usalama wake. Na swala hufanya hivyo bila kufunzwa. Nani basi aliyefunza?

Yatazame maji, angalia umuhimu wake kwa maisha yetu. Ona jinsi yanavyopatikana kwa wingi kukidhi mahitaji yetu. Je, yangekuwa yanapatikana kwa taabu kama almasi au dhahabu, maisha yetu yangewezekana kweli?

Jiulize kama mvua ingekuwa inanyesha siku zote usiku na mchana bila kuacha, maisha yetu yangekuwaje? Nani anaiamuru ije kwa msimu kwa manufaa yetu? Angalia Msumbiji wanavyohangaika.

Wengi wetu twapenda sana ubwabwa, hebu angalia kilimo cha mpunga.Tazama kiasi cha mbegu kinachotumika kwa shamba la ekari moja na linganisha na kiasi cha mavuno tunayopata. Debe moja la mbegu latoa magunia. Jiulize nyongeza inatoka wapi na je tungekuwa tunapata kiasi kile kile tunachokipanda, tungesalimika na njaa kweli?

Tazama wewe unavyotumia nguvu kukatua lindi la kufukia mbegu za mahindi, lakini angalia jinsi jani laini la mme huo linavyochomoza juu ya udongo uliofukilia mbegu na tizama namna punje zako mbili zinavyootesha mashuke. Ni muhisani gani anayetengeza namna hiyo?

Haya ni maswali ya kawaida kabisa ambayo hayahitaji hata elimu ya msingi. Iwapo mtu atasaili akili yake atamuona Muumba wake waziwazi.

Kwa kuitumia vyema akili yake, Mtume Muhammad (s.a.w.) aliweza kuitakidi kuwepo kwa Mungu hata kabla ya Utume.

Hata hivyo, akili yake pekee isingeliweza kumpatia mwongozo na utaratibu sahihi wa kumuabudu Mungu na kuwaelekeza wengine katika itikadi na ibada hiyo sahihi.

Kwa mantiki hiyo, binadamu anahitaji muongozo wa Mungu ili kukidhi matakwa ya akili na utafiti wake. Ndio maana mwanasayansi mashuhuri wa hivi leo Profesa Maurice Bucaille, baada ya kuthibitisha kisayansi kuwa Mungu yupo akaona ayafanyie utafiti maandikio matakatifu ili apate muongozo sahihi.

Akapekua Qur'an na Biblia na kuvichambua kwa kuvipambanisha na sayansi kuona kama maelezo ya vitabu hivyo yanakubaliana na utafiti wake wa kisayansi. Hatimaye maafikiano ya ajabu kati ya aya za Qur'an na data za kisayansi yakampelekea kusilimu huku akikiri kuwa sayansi bado ina deni kubwa kwa Qur'an kwani kuna aya za Qur'an zinazohusu maumbile ambazo sayansi haijaweza kuzijibu.

Itaendelea toleo lijalo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook