IKIWA imebaki miezi sita tu kabla Watanzania kuwachagua viongozi watakaowaongoza kipindi kingine cha miaka mitano, dalili za kutaka mabadiliko zimeanza kujitokeza.
Uchunguzi unaonesha wananchi wengi wamekata tamaa na namna mambo yanavyoendeshwa na serikali iliyopo madarakani karibu katika kila eneo.
Kuzidi kuporomoka kwa uchumi wa nchi, kushamiri kwa rushwa, miundo mbinu mibovu, huduma mbaya za afya na uongozi wa nguvu kazi usiojali hisia za wananchi, ni baadhi ya mambo yanayotajwa kuwakatisha tamaa wananchi wengi.
Tatizo sugu la maji jijini, bobomoa isiyofidia na serikali kukataa kulipa mafao ya wazee waliokuwa wafanyakazi wa iliyokuwa jumuiya ya Afrika mashariki ni mambo mengine yaliyowahuzunisha na kuwakasirisha wananchi.
"Ni fedheha jiji la kimataifa kukosa maji mpaka wakazi wake walazimike kupanga foleni kwenye madimbwi na mifereji ya maji machafu halafu viongozi waendelee kujinadi kuwa wanashughulikia kero za wananchi", anasikitika mwananchi mmoja wa ubungo Jijini.
Mwananchi mwingine mkazi wa magomeni alimwambia mwandishi hakuna ambacho Tanzania yaweza kujivunia mbele ya mataifa mengine ukiondoa umaskini wake.
" Labda viongozi wetu wanaona fahari nchi yetu kuitwa maskini zaidi duniani vinginevyo kwa miaka yote 40 ya kuwepo kwao madarakani pangelionekana jitihada za kimatendo kuboresha hali ya nchi yetu", alisema mwananchi huyo huku akishutumu ung'ang'anizi wa viongozi hao ilhali wakijua hawana mipango yoyote ya kuiendeleza nchi.
Kipi ambacho CCM kwa miaka 40 ya utawala wake imeweza kubuni na kukitekeleza kwa ajili ya kuwapatia hali bora wananchi wa Taifa hili ambacho inaweza ikasimama hadharani kujivuna ni miongoni mwa maswali yanayoulizwa na wananchi katika makundi na mikusanyiko mbalimbali.
"Uchumi wa nchi umevurugika, elimu imeshuka, michezo imekufa, maadili yameporomoka, hali zetu za maisha zimekuwa ngumu zaidi, watu wenye kuguswa na matatizo ya watu hawawezi kuwa na nyuso za kusimama kuomba waendelee kuongoza kwa vipindi vingine", anasema Bwana Daud mkazi wa Ilala jijini.
Labda kwa kulijua hilo ndio maana viongozi wa chama tawala na serikali yake hukimbilia kujitapa kwa amani na utulivu uliopo nchini hali ambayo haitokani na jitihada ya yoyote yule.
Matatizo ya watu kufa kwa njaa kule Ifakara Morogoro na Kilwa ni hali ambazo huenda zikachangia kuanguka kwa chama tawala katika uchaguzi ujao.
Serikali imekuwa ikishindwa hata kusambaza chakula cha misaada kutokana na kukosekana usafiri na ubovu wa miundo mbinu.
"Serikali inafanya nini kama inashindwa hata kusambaza misaada inayopokea kutoka kwa wahisani?" anahoji Bwana Mbena mkazi wa Kilombero.
Kwa kuyajua hayo inadaiwa ndio maana viongozi wa CCM na serikali yake inavifanyia hila vyama vilivyodhamiria kuleta mageuzi ya kweli nchini.
Hata hivyo, hilo huenda lisiwe na tija kutokana na wananchi wengi hasa wa mijini kuanza kupembua chuya kutoka kwenye mchele.
Labda hatari kubwa kwa vyama vya upinzani ni ule uwezo wa chama tawala wa kuvitumia vyombo vya dola, vyombo vya habari hasa Radio ya Taifa na Tume yake teule ya uchaguzi kukinufaisha.
Lakini kwa mwamko huu uliojitokeza kwa wananchi unaotokana na kutokuwa tayari kuendelea kuvumilia hali ngumu za maisha zinazowakabili , nini hali ya baadaye iwapo CCM itatumia hila na mabavu kubaki madarakani?
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |