Morogoro:
Kielelezo cha ufukara na sera za kibalakala nchini - 2

KWA mazingira tuliyoyaona leo hii ambayo yanajieleza yenyewe pato la mwana Morogoro wa tabaka la chini halizidi dola moja ya Kimarekani kwa siku wakati yule wa tabaka la kati halizidi kati ya dola tatu kwa siku, huku vigogo wakiingiza maelfu kama si malaki na mamilioni ya shilingi kwa siku, hali ambayo inaonesha pengo kubwa lililopo kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho.

Upo msemo mashuhuri kwa wanauchumi duniani : "If you fail to plan you plan to fail" ukimaanisha kuwa iwapo tumeshindwa kupanga basi ni wazi kuwa tumepanga kushindwa.

Itakumbukwa kuwa enzi zile za "chama chashika hatamu Chama tawala (CCM) mkoa kiliweka wazi kile walichokiita "Programu ya chama".

Programu hiyo ambayo ilitakiwa itekelezwe na wananchi wote chini ya usimamizi wa serikali ilikuwa na shabaha ya kukiwezesha chama hicho kuchambua maazimio yake (kama ilivyo kawaida ya chama tawala CCM kuongozwa na kuongoza nchi kwa maazimio, mara leo la Arusha, oo la Musoma, Iringa na kadhalika), kubuni kile walichokiita wenyewe (CCM) kuwa "njia sahihi ya kuyaelekeza (maazimio hayo) na kutathmini utekelezaji wake.

Programu hiyo ilijihusisha sana na uendelezaji wa kilimo cha mazao ya chakula na ya biashara, ufugaji na uvuvi.

Umuhimu mkubwa ukaelekezwa katika mashamba ya pamoja ya vijiji (vya ujamaa) ambapo kila mwanakijiji mwenye uwezo wa kufanyakazi ilimlazimu akadiriwe kiwango chake cha kilihudumia shamba hilo (kiwango ambacho hakikupungua nusu heka).

Aidha, kila mtu mwenye uwezo wa kufanyakazi mjini na vijijini "alilazimishwa" kulima si chini ya ekari moja ya zao linalohimili ukame na nyingine ya zao la biashara.

Mbali na hapo ukaasisiwa mpango mwingine wa kuhakikisha kwamba ile sheria ya kila mwana Morogoro mwenye uwezo wa kufanyakazi basi "lazima" afanyekazi ili "kujaribu" kuongeza uzalishaji na ufanisi katika 'rasilimali za uhakika' zilizokuwepo!

Sheria hiyo ikaitwa "nguvu kazi", na ikafanywa kuwa ni ya kudumu.

Sheria hiyo ikaanzwa kutekelezwa kwa vishindo, 'semina' kwa wananchi katika ngazi zote zikakithirishwa, maeneo ya kilimo yakatengwa na watu wakahesabiwa (hasa Morogoro mjini palipoorodheshwa jumla ya watu 85,968 kati yao wenye uwezo wa kufanya kazi ni 42,933 na wasio na uwezo huo ni 43,035. Aidha palipatikana watu 3,447 wasio na kazi, wafanyakazi maofisini 15,337 wakulima 15,829 na wafanyabiashara 3,984).

Chini ya mpango huo Morogoro mjini ilipima ekari 7,067 chini ya lengo la kulima ekari 13,600 kwa mujibu wa taarifa ya kazi za chama hicho (CCM) ya mwezi Januari 1982 hadi Desemba 1985 iliyotolewa na ofisi kuu ya CCM mkoani humo.

Aidha, Morogoro mjini ililima ekari 11,796 na kupanda zote, hata hivyo hakukuwa na takwimu zozote zilizoonesha tani za mazao yaliyovunwa wakati huo, kama ilivyo kuwa kwa wilaya ya Kilosa iliyolima ekari 1,684 na kupanda ekari 1,633 kati ya ekari 2,715 zilizolipimwa na ekari 3,000 zilizokuwa katika lengo.

Ni Morogoro vijijini pekee iliyooonesha takwimu sahihi za mazao iliyovuna (yaani ni tani 9,681) toka katika ekari 780 ilizolima na 691 ilizopanda kati ya 900 zilizopimwa na kuwekwa kwenye lengo la utekelezaji.

Chini ya zile zilizoitwa "Kamati za kusukuma uchumi kivita" mpango wa nguvu kazi ukaendeshwa kama "operation" wala si kama utaratibu wa kawaida wa kazi za viongozi husika katika ngazi zote kama lengo la muundo wa uendeshaji wake lilivyoonesha awali.

Kiuhakika mpango huo ulioanzishwa "kijazba" badala ya kitaalamu haukudumu bali ulikufa baadaye.

Cha kushangaza ni kwamba licha ya kuwepo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, bado mkoa huo unaongozwa na mipango butu na pofu isiyo na tija yoyote kwa maendeleo ya mkoa na wakazi wake zaidi ya kuwadidimiza. Hiyo ni kashfa kubwa, si tu kwa wasomi wa SUA pekee bali kwa Taifa kiujumla.

Kwa ufupi wa maneno, mpango mzima wa nguvukazi zaidi ya kutopangwa kitaaluma kwa kuzingatia hali halisi ya eneo husika jinsi ilivyo bali pia haukuwashirikisha kabisa wananchi wa eneo husika hususan wakulima (communication with farmers), mbali ya 'kuwaswaga' kibabe' kuutekeleza mpango wasioshiriki kuupanga. Semina tupu za kuburuzana hazikusaidia kufanikisha mpango huo.

Tukirejea katika kilimo chenyewe kiuhakika ardhi ya Morogoro inawzesha kabisa kulilisha eneo zima la Afrika Mashariki na kati kwa kutumia bonde moja tu la mto kilombero lenye ukubwa wa jumla ya hekta 336,740.

Bonde hili lenye rutuba ya kutosha limekusanya maeneo Luri, Mchilipa, Uwanda wa Lwasesa, Furuwa, Uwanda wa Sofi, Ruhiji, Mnyera, Mpanga, Kihanzi, Mgeta, Ruipa na hata Lumemo.

Ardhi ya mkoa huu imegawanyika katika maeneo makuu matatu muhimu kwa kilimo yaani eneo la milima na nyanda za juu ambalo limemeza milima ya Unguu, Uruguru, Rubeho na Mahenge kunakofaa sana kwa kilimo cha mahindi, viazi mviringo na vitamu, ngano, matunda kadha wa kadha, kahawa na hata migomba.

Aidha kuna eneo la ardhi tambarare na mabonde panapostawisha vitunguu, kunde, mpunga, maharage, choroko, korosho, ufuta, pamba na hata alizeti. Japokuwa wilaya zote zina mabonde, kipande kikubwa cha ardhi ya wilaya ya Morogoro na Kilombero kimemezwa kwenye eneo hilo.

Pia kuna eneo la miinuko chini ya milima, hususan katika baadhi ya sehemu za wilaya ya Morogoro na kuna kiasi kikubwa wilayani Kilosa. Katika eneo hilo mazao kama mpunga, matunda ya aina mbalimbali, mbegu za mafuta, mkonge, migomba na mahindi hustawi kwa uzuri na kwa wingi.

Licha ya neema hizi za ardhi nzuri Mwenyezi Mungu aliyoitunukia Morogoro, mkoa huo ndiyo kwanza unazidi kusheheni mlolongo wa maghala ya njaa na ufukara kila uchao!

Ukiwauliza hao "waheshimiwa" 'wanaoongoza' husukuma 'makapu' ya lawama zao kwa wananchi kuwa eti ni 'wavivu' unapowabana zaidi kwa nguvu ya hoja kuwa mtu halaumiwi kwa kuanguka kwake ila umeangalia pale aliposimama au alipojikwaa, basi vigogo hao huiacha hoja hiyo ya nguvu na kusingizia 'ukame'. Ukiuliza zaidi utaambiwa acha uchochezi!

Hapa ningependa kusherehesha kidogo kuwa kama upo mkoa wenye utajiri wa ardhi ifaayo kwa kilimo cha kiangazi barani Afrika basi Morogoro ni mmojawapo.

Utafiti uliofanywa na mwandishi unaweka wazi kwamba Morogoro ina zaidi ya hekta 424,000 zifaazo kwa kilimo cha umwagiliaji maji (kilimo cha kiangazi)!

Kichekesho ni kwamba si zaidi ya asilimia tatu tu ya eneo hilo ndilo linatumika kwa kilimo hicho, tena si kwa ukamilifu wake.

Ukiacha bonde la mto Kilombero, yapo mabonde mengine matatu makubwa yenye uwezo mkubwa mno wa kumfagia kabisa mdudu njaa hapa mkoani, nchini na hata nje ya mipaka iliyoizunguka Tanzania.

Kwa mfano, bonde la mto Wami lenye jumla ya hekta 26,1000 (Mkindo na Mgongola hekta 15,6000, Wami Dakawa hekta 10,500) endapo litaendeshwa vile itakikanavyo basi kitu kinachoitwa "umaskini" "ufukara" au "njaa" kitabaki katika jaa la historia ya kutisha, kushangaza, kuchekesha na hata kusikitisha ya Morogoro.

Au bonde la mto Luwangu lenye jumla ya hekta 26,950 lilikusanya Luhombero, Luwengu, Ruaha na Uwanda wa Chilombola, linaweza kabisa kuigeuza miundo mbinu yote ya kiuchumi na kijamii kiasi cha kuyafanya maeneo husika kuwa kielelezo cha maendeleo nchini.

Na hata bonde la mto Ruaha pekee likiwa na hekta 45,000 (Kidatu na Msolwa hekta 30,000; pamoja na uwanda wa Kiberege hekta 15,000) linaweza kabisa kuugeuza mkoa wa Morogoro kuwa "Hong Kong ya Tanzania". Badala ya viongozi wetu kufunga safari kwenda kushangaa maendeleo ya Wachina!

Uchumi wa Morogoro unategemea ufugaji kwa mazao yake, yaani nyama, maziwa, ngozi, mayai na mboleo.

Hadi mwaka 1988 mkoa ulikuwa na ng'ombe 515,038, mbuzi 160,318, kondoo 62,613, kuku 993,121, wanyama wengine kadri ya 86,509, jumla ya mifugo yote ikiwa 1,614,589.

Zaidi ya asilimia 80 ya eneo hilo lina ndorobo aidha kuna ukosefu wa maji ya kutosha katika eneo kubwa linalofaa kwa ufugaji ambalo linautajiri mkubwa wa nyasi nzuri za asilia.

Hali hiyo ya ndorobo, kutoanzishwa vijiji vipya vya kudumu vya ufugaji na ukosefu wa maji ya kunyweshea mifugo, umepelekea kiwango cha cha mifugo kubaki kama ilivy.

Jambo lingine linaloathiri sana maendeleo ya mifugo ni uchache na uduni wa huduma za mifugo hiyo. Tokea Desemba 30, 1988 hadi hivi sasa hakuna ongezeko lolote la maana la vituo vya huduma za mifugo chini ya takwimu za kutegemewa. Ambapo majosho yalikuwa 78 kimkoa! Vituo vitatu vya kupimia dawa ya josho, vituo 17 vya afya ya mifugo, machinjio 12, minada 17 ya mifugo, vibanio vinane, mabanda 10 ya ngozi, vituo vinne vya kutotoa na kulelea vifaranga, maabara nne na kituo kimoja cha madume bora.

Hadi wakati huu vituo vyote hivyo viko nyuma ya wakati kiteknolojia.

Itaendelea toleo lijalo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook