Saudi Arabia-2


Sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji

UFALME wa Saudia umefanya kazi kubwa kuasisi kama si kuendeleza sekta ya kilimo, kwa kuligeuza jangwa kuwa ukanda wa rutuba (green belt) unaozalisha mazao mbalimbali. Nchi hiyo kila mwaka hutoa mavuno ya kustaajabisha jangwani hususan ya mazao kama ngano, tende, matunda na mboga kadha wa kadha za majani na nyinginezo. Kiroja kwa nchi kama Tanzania yenye ardhi yenye rutuba asilia, hali nzuri ya hewa na nguvu kazi ya kutosha lakini watu wake wanaangamia kwa njaa na taifa lateketea kwa umaskini huku wanasiasa 'wakishiba' na kupiga domo kwa propaganda pofu za "kilimo ndio uti wa mgongo"

MAZAO ya mifugo na samaki ni tegemeo lingine jipya linalotoa tumaini jema la pato lingine tegemevu la taifa na muhimili mbadala wa uchumi toka katika mafuta hadi kwenye madini, kilimo, ufugaji na uvuvi.

Saudia hivi sasa pia ndio mtoaji mkubwa wa maua duniani, hususan mauaridi yanayolimwa katika jangwa lililogeuzwa kuwa sehemu ifaayo kwa kilimo, hivyo kuzalisha maelfu ya tani za maua muda hata muda na kuyauza katika nchi mbalimbali duniani, hususan barani Ulaya, Uholanzi ikiongoza kwa manunuzi.

Lengo la serikali hiyo ni kuwapa changamoto zaidi raia wake kujihuisha mno na sekta za kilimo na viwanda, ili kuongeza pato la taifa ukizingatia kuwa mafuta huenda yakapungua matumizi yake kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyoko usoni mwa dunia katika karne hii tuliyonayo.

Ili kuvutia sekta binafsi katika uwanja wa kilimo, ufugaji na maendeleo ya viwanda, serikali ya Kisuudi imeanza kugawa bure zaidi ya hekta 1,500,000 za ardhi isiyolimwa kwa wakulima na wafugaji kuiendeleza.

Aidha, serikali inajitahidi kwa kasi ya ajabu kujenga barabara (kwa maana ya barabara na si kumwaga changarawe na vijilami vya kulishia 'vichochoroni') katika ukanda wa kilimo ili kurahisisha usafiri baina ya miji na mashamba.

Serikali pia imechangia zaidi ya asilimia 45 za gharama za vifaa vikubwa na mashine nzito nzito za kilimo, na asilimia 50 za gharama za kununulia mbolea ndani na nje ya nchi pamoja na pembejeo nyingine.

Serikali inajitahidi kila uchao kuchimba visima virefu na mabwawa ya uhakika yanayotosheleza kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mwaka mzima (na si kugemea mvua kama Tanzania).

Ufalme wa Saudia aidha unatoa mbegu kwa gharama nafuu na wataalamu wa kilimo na ufugaji husukumwa mashambani kushirikiana bega kwa bega na wakulima katika jitihada hiyo.

Cha kufurahisha zaidi, serikali ya Saudia pia imefungua makampuni makubwa kabisa nchini humo kila moja likiwa na mtaji usiopungua Riali milioni 300 za Kisaudi yajihusishayo na uzalishaji wa mazao ya kilimo na ufugaji, aidha kuipa changamoto sekta binafsi izamie kuwekeza kwenye kilimo na ufugaji.

Kupitia taasisi yake iitwayo "General Foundation For Silo Harvest and Grain Mills", serikali ya nchi hiyo hununua mavuno yote ya mwaka ya ngano na mazao kadhaa mengineyo kwa bei "inayolipa".

Uzalishaji wa mwaka 1992 kwa ngano pekee ulikuwa tani milioni nne, wakati mwaka 1970 serikali ilizalisha tani 26,000 tu.

Uzalishaji wa tende nao ukapanda toka tani 240,000 mwaka 1970 hadi tani 700,000 mwaka 1992. Saudia ina mitende zaidi ya milioni 13.

Uzalishaji wa mboga za aina mbalimbali aidha uliongezeka toka tani 470,000 mwaka 1980 hadi tani 792,000 mwaka 1991.

Uzalishaji wa mabata mzinga mwaka 1992 ulifikia tani 470,000 na tani 113,000 za mayai. Na uzalishaji wa samaki nao ukafikia tani 50,000 mwaka 1992.

Kiwango cha fedha zilizotolewa na Benki ya Kilimo ya Saudia (Saud Agricultural Bank) kama mikopo kwa wakulima kwa mwaka 1412H (1992) ni Riali 358,019 zikijumuisha bilioni 26.5 za Riali hadi mwishoni mwa mwaka huo.

Benki hii iliyoanzishwa mwaka 1962 ilianza rasmi shughuli zake kati ya mwaka 1964/65 ikitoa mikopo isiyo na riba (kwa kuzingatia sheria za Kiislamu) kwa wakulima na miradi mbalimbali ya kilimo na maendeleo yake, na pia kununulia vifaa vya kilimo.
 

Maendeleo ya maji

Kitu kinachoangaliwa kama mboni ya jicho na serikali ya Saudia ni huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wake. Ambapo visima virefu visivyopungua 40,8100 vya maji halisi vilichimbwa na serikali ya Saudia, ukiacha vile 52,327 vilivyochimbwa na watu binafsi.

Kwa lengo la kuimarisha matumizi yasiyo shaka ya maji nyumbani (domestic use) na umwagiliaji (irrigation), serikali hiyo imeongeza mabwana 200 ya kisasa yanye uwezo wa kuvuna maji ya mvua kwa ujazo wa kiubiki (cubic) mita 450 milioni kwa siku.

Aidha, kuna vituo 29 katika ghuba ya Uarabu (Arabian Gulf) na kwenye pwani ya bahari nyekundu (Red Sea) au bahari ya Sham, vya kubadili maji chumvi ya bahari kuweza kunyweka kama maji safi na salama vyenye uwezo wa kuzalisha kiubiki mita 600 milioni kwa siku. Baahi yake pia huzalisha umeme kwa wakati huo huo!
 

Viwanda

Tangu utekelezaji wa mpango wa kwanza wa miaka mitano wa maendeleo katika mwaka 1970 serikali ikaelekeza macho yake ya umakinifu wake katika ujenzi wa viwanda imara na vikubwa kwa kuweka msingi madhubuti wa sekta ya viwanda.

Hivyo ikaanzisha ukanda maalum wa viwanda (special industrial zones) huko Riyadh, Jeddah, Al-Dammam, Al-Ahsan, Al-Qasim na Makkah Al-Mukarama.

Sambamba na hilo serikali ikaasisi majiji mawili ya viwanda (industrial cities) huko Jubail na Yanbu.

Viwanda vinavyofanya kazi nchini humo vimeongezeka toka 199 mwaka 1970/71 kwa mtaji wa Riali bilioni mbili nukta nane hadi viwanda 2,036 mwaka 1992/93 kwa mtaji wa bilioni 138.5 Riali za Kisaudi.

Viwanda hivi vimeuza nje bidhaa zenye thamani ya Riali bilioni tatu nukta tano huku idadi ya wafanyakazi ikiongezeka toka 14,000 mwaka 1970/71 hadi 175,000 mwaka 1992/93.

Maingizo ya jumla ya miradi ya viwanda yalikuwa 151.2 bilioni za Riali mwaka 1992 na hilo ni ongezeko toka 33 bilioni za Riali mwaka 1974. Hii inaashiria ongezeko la jumla la asilimia 40.1.

Jiji la viwanda la Jubail ambalo limetuama kwenye pwani ya mashariki ya ufalme wa Saudia, na jiji la viwanda ya Yanbu ambalo liko pwani ya magharibi ya nchi hiyo, yamekusanya viwanda vikubwa kadhaa na hata shirika kuu la viwanda mama (Saudi Basic Industries Corporation) au SABIC na mashirika mengine 'mazito' ya petroli na madini yamejichimbia katika majiji hayo.

Majiji hayo mawili yanamilikiwa na kuendeshwa na tume maalum iitwayo Royal Commission For Jubail and Yanbu.

SABIC lilianzishwa mwaka 1976 ikiwa na miradi ya vitega uchumi yenye utajiri wa 38 bilioni za Riali, ikiwa ni pamoja na viwanda vya kujengea viwanda.

Shirika lingine liitwalo Petromineral au Petromin liliasisiwa mapema zaidi, yaani mwaka 1962. Hili limepewa jukumu la kuendeleza sekta ya mafuta, gesi ya sili na madini nchini humo.

Viwanda vya msingi vya Saudia chini ya SABIC vizalishavyo mazao ya petroli vilizalisha tani 15.7 milioni mara SABIC ilipoundwa.

Idadi ya wafanyakazi wa SABIC na miradi iliyochini yake hadi sasa ni zaidi ya 11,137 ambapo asilimia 61 ni raia wa Kisaudia.

SABIC imepata faida maradufu toka 148 bilioni za Riali mwaka 1985/86 hadi bilioni 1,964 Riali za Kisaudi mwaka 1992/93.

Uwezo wa SABIC wa kuuza ng'ambo mazao ya petroli ulifikia bilioni sita nukta saba Riali za Kisaudia zikiwakilisha asilimia 66 ya uwezo wa jumla wa bidhaa za viwanda vyake ziuzwazo nje. Wastani wa mwaka kuuza ng'ambo bidhaa zake umeongezeka kwa asilimia 30 katika kipindi cha mwaka 1984 na 1992.

Nayo PETROMIN (Petroleum and Mineral Organization) linaendesha viwanda tisa vya kusafisha mafuta nchini humo. Ambavyo tangu mwaka 1991/92 vimekuwa vikizalisha mapipa milioni moja nukta nane kwa siku au milioni 657 kwa mwaka.
 

Umeme

Wakati nchi kama Tanzania "ikipogoma" na umeme wa mgao toka Kidatu, Mtera na ule wa Kihanzi pamoja na wa Dizeli, tayari Saudia ina mtambo wa umeme wa nishati ya jua (Solar energy) wenye uwezo wa kuhudumia vijiji 400 kwa wakati mmoja bila matatizo.

Mbali na teknolojia ya kisasa kabisa, serikali ya Saudia kupitia mfuko wake wa maendeleo ya viwanda (Saud Industrial Development Fund) inasaidia mitambo mingine ya umeme kwa kuanzisha miradi mikubwa mikubwa inayowahusisha watu binafsi kwa kupewa mikopo nafuu.

Jumla ya mikopo iliyotolewa na SIDF kati ya mwaka 1975 hadi 1986 kwa makampuni binafsi ya umeme imefikia Riali bilioni 37.9.

Tangu mwaka 1985/86 SIDF imejing'atua na kuachia shughuli hiyo shirika lingine liitwalo General Electricity Organization ambalo linasaidia miradi ya majengo moja kwa moja toka katika bajeti yake yenyewe kila mwaka.

Serikali pia husaidia kampuni ndogo ndogo kwa fedha, ushauri, utawala na uendeshaji chini ya wizara yake ya viwanda na umeme. Zaidi ya hapo huweka Tahfifu ya malipo ya umeme kwa wenye viwanda.

Kwa upande wa utoaji wa umeme kiwango cha umeme kilichozalishwa mwaka 1993 pekee ni 61,731,282 Mega Watts kwa saa. Idadi ya wafanyakazi wa sekta ya umeme imeongezwa toka 8,363 mwaka 1977 hadi 26,342 mwaka 1992 wakiwa na vifaa vya kisasa kama vitendea kazi, mishahara mizuri na marupurupu yake pamoja na bima.

Urefu wa jumla wa njia za umeme Saudia hadi mwaka 1990 ulikuwa zaidi ya kilometa 13,000. Umeme nchini humo umeenea hivi leo katika jumla ya miji, majiji na vijiji 5,445 nchi nzima.

Itaendelea toleo lijalo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook