Zifahamu aina za maziwa


MAZIWA ni moja kati ya vyakula vitupatiavyo virutubisho aina mbalimbali katika miili yetu mfano maziwa hutupatia protein, mafuta, vitamini kama A na D madini kama kasiumu na kadhalika. Hutumiwa kama kinywaji baridi au moto kiungo katika vyakula au chakula pekee kwa watoto. Pamoja na umuhimu huu wa maziwa, kuna watu miongoni mwetu hatufahamu maziwa yalivyo. Tuyaone kwa ufupi.

Na Halima Juma

MAZIWA yanaweza kugawanyika katika mafungu manne, maziwa halisi (fresh), maziwa ya mgando, maziwa ya maji ya kwenye makopo au pakati (canned) na maziwa ya unga kwa ufupi hayo ndio makundi ya maziwa. Baada ya kuyafahamu tuyaangalie kwa undani.

Maziwa halisi (fresh) ni maziwa ambayo yamekamuliwa na kuhifadhiwa kama yalivyo. Hayajaongezwa wala kupunguzwa kitu chochote. Maziwa ili yatumike kama kinywaji au kuhifadhiwa ni lazima yachemshwe ili kuuwa wadudu hatari na wale wanaogandisha maziwa.

Maziwa yaliyochemshwa vizuri hukaa siku moja au mbili bila ya kuganda iwapo yatafunikwa kwenye chombo safi. Maziwa yakinywewa bila kuchemshwa huweza kuleta au kusababisha magonjwa mbalimbali kama kuharisha, kifua kikuu na hata magonjwa mengine yanayotokana na ng'ombe mwenyewe moja kwa moja au kutoka kwa mkamuaji na vifaa vya kuhifadhia maziwa yenyewe.

Unashauriwa kutokunywa maziwa baridi mitaani bila ya kuwa na hakika kama yamechemshwa au la. Vibanda vingi vya maziwa huuza maziwa halisi baridi bila ya kuchemsha. Ni bora moto kuliko baridi.

Aina nyingine ya maziwa ni mgando (soul milk). Maziwa yanayoganda wadudu wasio na madhara hukua ndani yake. Wadudu hawa hubadilisha baadhi ya chembe chembe za maziwa kuwa acidi ambayo hubadilisha pia ladha ya maziwa.

Wadudu waharibifu huwa si rahisi kuzaliana kwenye maziwa yaliyoganda na kuyafanya yadumu kwa muda. Maziwa ya mgando pia yapochunjwa maji huwezakukaa muda bila ya kuharibika. Maziwa ya mgando yaliochujwa maji huitwa "cheese".

Ni vyema ifahamike kuwa si maziwa yote huwa ni salama. Kama nilivyoeleza hapo awali, maziwa yanaweza kubeba wadudu wa magonjwa kutoka kwa ng'ombe, mazingira ya ukamuaji na vyombo vya kuhifadhia au mkamuaji mwenyewe. Kwa sababu hizo basi ni vigumu kwa maziwa kuwa salama.

Watu wengi hugandisha maziwa bila ya kuchemsha. Imani yao ni kuwa wadudu watakufa au hawatazaliana tena. La hasha. Kutozaliana si sababu ya kutochemshwa. Wadudu wapo, ila hawataendelea kuzaliana. Hivyo watakudhuru pamoja na uchache wao. Ni vyema kuyachemsha ndipo kuyagandisha.

Utakapochemsha, utauwa wadudu wanaodhuru, na wale wasioudhuru wamejaa tele hewani, maziwa yote yataganda bila wasiwasi. Tujihadhari sana na maziwa ya mgando ya mitaani, mabarabarani na hata migahawani. Wengi wao hawachemshi kabla ya kugandisha. Iwapo utakuwa na hamu sana, jiandalie kwako. Nunua fresh, chemsha, gandisha kwa ajili ya kesho. Takriban masaa manane hadi kumi maziwa yaliyochemshwa huanza kuganda. Hivyo waweza kuchemsha jioni na kutumika asubuhi au kuyagandisha asubuhi na kunywewa jioni.

Maziwa ya maji ya kwenye makopo au vifuko vya karatasi au nailoni ni aina nyingine ya maziwa. Tunaiita hii kuwa ni aina nyingine ya maziwa kwa sababu kadhaa, mojawapo ikiwa ni kule kupitia kiwandani. Maziwa halisi hupelekwa viwandani na kufanyiwa mabadiliko kadhaa.

Mathalan maziwa huwekewa madawa kwa ajili ya kuuwa wadudu na kudumu muda mrefu bila ya kuharibika. Mara nyingi huondolewa sehemu ya maji (evaporated milk) au hata kuondoa sehemu kubwa ya maji (condensed milk).

Wakati mwingine huongezwa virutubisho na hata kuchanganywa na sukari nyingi. Yale yenye sukari nyingi hudumu zaidi hata yanapofunguliwa kwani sukari huzuia wadudu kukua. Mara nyingi maziwa haya virutubisho vyake huharibiwa na madawa wakati wa utayarishaji. Pamoja na kuwa huwa wanaongeza virutubisho vingine, si mara zote huwa wanakuwa sahihi.

Jitahidi kila iwezekanavyo kunywa maziwa halisi kuliko yanayopitia viwandani. Ni jambo muhimu kuzingatia tarehe ya mwisho ya kutumika maziwa hayo. Ni lazima iandikwe kwenye kopo au kijifuko cha kuhifadhia. Ni jukumu la serikali kupitia shirika lake la viwango (TBS) kuhakikisha tarehe hizo ni za kweli au za kibiashara zinapelekea wanywaji (watumiaji) kuathiri afya yao. Kwa upande mwingine ni jukumu la mtu binafsi kuwa makini na kila anachokula kinywani.

Aina ya mwisho ya maziwa ni maziwa ya unga (died milk). Maziwa halisi huondolewa maji yote na kubakia unga. Vitamini zote ambazo huwepo katika maji hupotea, kama vitamini C na B. Lakini virutubisho vingine hubakia. Lakini yapo maziwa mengine huondolewa maji pamoja na mafuta. Haya huitwa (died skimmed milk).

Maziwa haya virutubisho hivyo kwa njia nyingine. Ni vizuri sana kuchunguza makopo au mifuko iliyohifadhiwa maziwa haya kuona ni ya aina gani na viwango vya virutubisho vilivyowekwa. Usipoteze pesa zako kwa kununua kitu kibovu. Maziwa yaliyo mazuri ni yale yaitwayo "whole died milk" ambayo yameondolewa maji tu. Kwa sehemu ambazo maziwa halisi ni vigumu kuyapata au hupatikana katika mazingira machafu, ni bora familia kutumia maziwa ya unga. Lakini kumbuka kuangalia tarehe ya kuharibika kila kilichopitishwa tarehe yake ya kutumika ni sumu.

Kwa upande mwingine, kuna maziwa ya unga ambayo hutengenezwa kwa ajili ya watoto. Haya huchanganywa na virutubisho mbalimbali ili kujaribu kuyalinganisha na maziwa ya mama. Hakika hilo haliwezekani kamwe. Iwapo mwanao itabidi atumie maziwa ya unga, angalia usije ukamnunulia maziwa ya wakubwa.

Tusiache kunywa maziwa katika milo yetu kadri tuwezavyo ili tuweze kuitunza na kuendeleza afya zetu pamoja na hayo ni vyema kufahamu aina gani ya maziwa inayokufaa.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook