IWAPO wasomi watatambua kwamba tamaduni hizi zisizofaa (chafu) ni gonjwa hatari toka nje ya mipaka ya jamii yao iliyotwaharika, linalolenga nafsi zao, nina hakika wana uwezo mkubwa wa kuuepuka na kupambana vilivyo na jitihada zote zinazotaka kuueneza kwenye taasisi za elimu. SAYYID ALA MAUDUDI anaendelea...
MIMI binafsi napenda ziwepo jitihada za kuunda hisia itakayopambana vikali na uchafu huu kwenye jamii ya wanafunzi wa Kiislamu ili wabaki kuwa barua inayosomeka katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mambo haya mawili ni miongoni mwa mambo yanayowahusu wanafunzi wenyewe, endapo watashikamana nayo ipasavyo basi nina hakika wataweza kuangamiza kabisa uchafu wote unaoenea kwa kasi mno kwenye taasisi zetu za kitaaluma.
Baada ya hayo hivi sasa nitachunguza kwa ufupi tu wajibu na majukumu ya srikali juu ya suala hili.
Ugonjwa mbaya wa rushwa
Jambo la kwanza ambao linaipasa serikali itafakari ni kuwaje, ni sababu gani inayofanya rushwa izidi maradufu?
Ugonjwa huu mbaya hivi sasa limeukumba umma wa Kiislamu. Kadhia hii angamizi imepelekea mifumo yote ya sheria kutofaa kabisa, kwa kuwa kila sheria iwekwayo kwa minajili ya kurekebisha, sheria hiyo huvunjiliwa mbali na sehemu zile zinazotegemewa kuongoza utekelezaji wa sheria hiyo!
Tena kila hatua ichukuliwayo na wawekaji sheria inafungua mlango mwingine mpya na mwepesi wa rushwa!
Zaidi ya hapo kwa 'msaada' wa rushwa hiyo wafanya magendo hutorosha nje ya nchi vitu ambavyo taifa lingali likivihitaji mno. Kwa lugha nyingine ya wazi zaidi ni kuwa rushwa inawalea vilivyo maadui zetu.
Hebu pigeni hatua zaidi na mtafakari kwa makini, mtu huyu anayewahami wananchi wenzake kwa ajili ya rupia mia moja kwa mfano, sidhani kama aweza kuona haya wala vibaya kuuza siri za serikali kwa maadui endapo atahakikishiwa hongo ya rupia elfu kumi?
Wakati ugonjwa huu hatari wa rushwa ukienea kwa kasi ya ajabu nchini, kiasi cha kuwaambukiza maelfu kama sio mamilioni ya watu kiasi cha kuwa tayari kuitoa muhanga dini, itikadi, uaminifu wake na hata nchi yake kwa gharama nafuu ya kukidhi maslahi yake binafsi.
Kwa hivyo, wale watakao kueneza uovu miongoni mwa wananchi wenzetu, wanaweza kabisa kuwatumia wasaliti hao kuyafikia malengo yao mabaya, kama ambavyo maadui hao wawezavyo kuwatumia katika kuuangamiza umma kwa njia nyinginezo.
Chanzo cha kuenea kwa rushwa
Hebu fikiri kidogo, ni kitu gani hasa kisababishacho jambo hili liumizalo?
Ni wazi kwamba wale walitendalo jambo hili (wanaojihusisha na rushwa) si wengine, bali ni ndugu zetu wasomi, Tena wao ndio wanakamata majukumu muhimu ya uendeshaji wa serikali na jamii kiujumla.
Wala majukumu hayo hayakamatwi na wanavijiji wasiojua kusoma.
Pia ndugu zetu hawa (wasomi) wamepata elimu yao katika vyuo vyetu vya kisasa.
Hii inaonesha kuwa kuna kasoro katika mfumo wetu wa elimu, mfumo ambao unatuzalishia idadi kubwa ya watu waliopatwa na ugonjwa wa rushwa.
Endapo tutautafakari mfumo wetu huu wa elimu upya, tutang'amua kwamba msingi mkubwa wa kasoro yake unatokana na kuwa mfumo huu unaidhoofisha ile misingi ya itikadi, utamaduni na tabia zetu za Kiislamu, badala ya kuiimarisha.
Pia mfumo huu unazusha tuhuma mbaya juu ya itikadi hizo na unawalazimisha baadhi ya watu kuzihama kabisa itikadi hizo. Ni wachache sana wanaotakia mfumo huu wakiwa salama bila ya kupata msukosuko wa itikadi katika nyoyo zao.
Wakati hali ilivyo ndio kama nilivyosema, jambo ambalo inatupasa tulitafakari ni kwamba, iwapo itikadi za wasomi wengi zimekuwa nyonge na dhaifu, je tuna kitu gani ambacho kitatuwezesha kuwafanya wasomi hao wawe na tabia njema?
Mtu asiyemugopa Mwenyezi Mungu wala adhabu ya siku ya malipo, hivi kitu gani kitamzuia asiwe mwongo, dhalimu na mzembe katika majukumu yake?
Mtu asiyetaka kufuata na kunyenyekea kitu kilicho na upeo wa mbali zaidi kuliko yeye mwenyewe na ambacho kiko nje ya maslahi yake binafsi, vipi mtu huyu ataweza kuwakinaisha ayatoe mhanga maslahi yake binafsi kwa ajili ya kutetea tabia njema?
Ili kumkinaisha mtu aweze kuitoa mhanga nafsi na mali yake ni lazima kuwepo utiifu na utawala wa juu zaidi. Naye Muislamu hana utiifu mwingine isipokuwa kumnyenyekea na kumtii Mwenyezi Mungu, Mtume wa Mwenyezi Mungu na Uislamu kwa ujumla.
Iwapo tutaudhoofisha utiifu huu katika nyoyo za watu na kuufanya uwe mnyonge kama nyumba ya buibui, ni lazima kutazuka ubinafsi katika nyoyo zao na watakuwa hawaoni vibaya kukitoa mhanga kitu bora, kitukufu na chenye thamani kubwa (Uislamu wao) kwa minajili ya kupata maslahi yao binafsi.
Itaendeleo toleo lijalo.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |