Wanafunzi Waislamu wadai kunyanyaswa Mtwara


SHULE ya sekondari Chidya iliyoko wilayani Masasi mkoa wa Mtwara imedaiwa kunyanyasa wanafunzi Waislamu kwa kuwazuilia baadhi ya haki zao.

Madai hayo yametolewa na wanafunzi Waislamu wanaosoma shule hiyo katika barua yao waliyoipeleka kwa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu nchini.

Kwa mujibu wa barua hiyo madai hayo ni pamoja na kuwekewa vikwazo wasihudhurie swala mbalimbali ikiwa ni pamoja na swala ya Ijumaa.

"Wanafunzi wa Kiislamu wanashindwa kutekeleza ibada hiyo kwani muda wa kutoka madarasani ni saa sita na robo halafu maji ya kujitayarishia yanapatikana umbali wa kilometa moja na nusu kutoka shuleni", imeeleza sehemu ya barua yao.

Kutokana na hali hiyo wamedai wanafunzi hao kuwa hulazimika kuchelewa kuanza swala ya Ijumaa wakati huo huo wakitakiwa wawepo darasani saa saba na robo kuendelea na masomo.

"Muda huo huo wa saa saba na robo tumewekewa jaribio la hesabu. Basi pindi tumalizapo ibada tunakuta wenzetu wameshamaliza jaribio na sisi tunakosa jaribio hilo kila Ijumaa na kuandikiwa sifuri kisha kuadhibiwa", wamedai wanafunzi hao ambao hata hivyo hawakujitaja majina katika barua hiyo.

Wanafunzi wameutuhumu uongozi wa shule kwa kile walichodai njama dhidi ya Uislamu. Kwa mtazamo wao wanafunzi hao wamedai kuwa hiyo ni njama na imekuwa ikisikika mara kwa mara kutoka ngazi za juu kuwa hawako shuleni hapo kuabudu bali kusoma.

Katika barua hiyo pia wanafunzi hao wameonesha vizuizi vilivyowekwa katika kila swala ili kuwafanya washindwe kufanya ibada shuleni hapo.

Aidha, imedaiwa kuwa wanafunzi wanaofahamu Uislamu huzuiliwa kuwafudisha wenzao.

Jitihada za gazeti hili kumpata mkuu wa shule kuhusiana na tuhuma hizo za wanafunzi Waislamu hazikufanikiwa kutokana na tatizo la mawasiliano.


Waislamu Songea waicharukia serikali

WAISLAMU mkoani Ruvuma wameishutumu serikali kuwa imekuwa ikiendesha harakati za kuwabana Waislamu kwa kuwaundia mabaraza yanayopokea maelekezo toka serikalini.

Wamesema mabaraza hayo yametumika kikamilifu kuwadhibiti Waislamu wasijiletee maendeleo.

Akizungumza katika Baraza la Idd lililofanyika Jumamosi mjini Songea, Mjumbe wa Umoja wa Vijana mkoani humo aliituhumu serikali kuwa ndiyo iliyosababisha matatizo katika jamii ya Waislamu.

Alisema kwa kuwa serikali ya CCM imeshindwa kutekeleza madai ya Waislamu kipindi chote cha utawala wake, basi itegemee kura ya pamoja ya hapana kutoka kwa Waislamu katika uchaguzi mkuu ujao.

Mwakilishi wa wanawake akizungumza kwa niaba alisisitiza dai la Waislamu kuitaka serikali iwafikishe mahakamani waliouawa Mwembechai.

Mama huyo aliyejitambulisha kwa jina la Sofia alisema serikali imeshindwa kuonesha uadilifu badala yake imekuwa ikipindisha ukweli.

"Tunataka iundwe tume kuchunguza vifo vya ndugu zetu waliolengwa kama nyati pale Msikitini Mwembechai", alimaliza Bi Sofia.

Baraza hilo lililoandaliwa na umoja wa vijana wa Kiislamu mkoani humo na kuhudhuriwa na mamia ya Waislamu limeelezwa kuwa limefungua ukurasa mpya wa Uislamu Ruvuma.


Waislamu Moro watakiwa kuzungumza siasa


WAISLAMU wana haki ya kuzungumzia mustakabali wao katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na siasa na utamaduni wao kinyume na propaganda kwamba hawatakiwi kuchanganya dini na siasa.

Hayo yameelezwa na Ustadh Said Ramadhani wakati akiongea na mamia ya Waislamu waliohudhuria Baraza la Idd katika viwanja vya shule ya sekondari ya Jabal Hira mjini hapa.

Alisema kuwa Maaskofu wamekuwa wakizungumzia mustakabali wa maisha yao na waumini wake katika nafasi za siasa, na hakuna anayewaambia wanachanganya mambo.

"Maaskofu wanapozungumzia kumchagua mcha Mungu wanajiangalia imani yao na hivyo sisi Waislamu tunayo haki ya kuelekeza waumini nani wa kumchagua katika chaguzi zijazo.

Aliendelea kusema kwamba Waislamu kigezo chao kikubwa ni Mtume Muhammad (s.a.w.) ambapo aliwahi kujiunga na chama cha kutetea haki za binadamu, hivyo Waislamu wanayo haki ya kushiriki siasa, kuingia chama chochote au kumchagua mtu ambaye wanaona anaweza kuwapatia haki za msingi kama raia.

Akizungumzia suala la kujielimisha Waislamu katika mambo yahusuyo dini yao, Ustaadh Said alisema, bado watu wengi wanatosheka na elimu walizokuwa nazo hali ya kuwa mambo yanabadilika na kuongezeka kila siku.

"Tusibweteke na elimu tulizokuwa nazo bali tusome na ninatoa changamoto kwa Waislamu wenye uwezo kufungua maduka na maktaba za vitabu vya Kiislamu ili kuweza kutoa fursa kwa waumini wetu kuweza kujifunza mambo ya msingi yahusuyo dini yao".

Katika baraza hilo lililohudhuriwa na mamia ya waumini, kulipitishwa maazimio kadhaa ambayo walioudhuria walitakiwa kuyafanyia kazi.

Maazimio yaliyoazimiwa ni pamoja na kila Muislamu kusoma Uislamu kwa ujumla pamoja na Waislamu kutakiwa kuanza kuwa kitu kimoja na kuhurumiana wao kwa wapo kama walivyoagizwa na Mwenyezi Mungu kupitia kitabu chake kitukufu Qur'an.

Pia Baraza hilo limeazimia kuwa kila Muislamu kuacha mara moja kuwafanya marafiki wale wote wanaowapiga vita katiaka dini yao wakiwemo wale waliohusika kwa namna moja ama nyingine kuwaua Waislamu pale Mwembechai na Msikiti wa Kiwanja cha Ndege mkoani Morogoro.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook