CCM yajinyonga yenyewe
MAJIBU ya Rais na matamshi ya kashfa ya baadhi ya viongozi wa CCM dhidi ya Waislamu yamezidisha chuki ya waumini hao kwa chama tawala.

Hali hiyo ilidhihirika Jumamosi iliyopita katika Baraza la Idd lililofanyika Msikiti wa Sinza Jijini ambapo maelfu ya Waislamu walitoa maneno ya kukilaani chama hicho na viongozi wake.

Ilikuwa kila ilipotajwa CCM au viongozi wake matamko ya laana yalifuatia.

Risala iliyosomwa na Mwenyekiti wa Msikiti wa Sinza Bwana Waziri Nkobo iliamsha Takbira pale ilipowataka waumini hao waelekeze hasira zao Oktoba wakati wa uchaguzi mkuu.

"Waislamu wana fursa moja tu nayo ni kutumia kura, fursa hiyo ni nadra sana inakuja mara moja kwa hiyo inabidi iwahiwe", imesema risala hiyo iliyoandaliwa na Jumuiya zote za Kiislamu Jijini.

Aidha, hata wale ambao ni wanachama wa CCM watapaswa kupiga kura ya hapana kwa Chama hicho ili kuonesha kwamba wana uchungu", aliongeza Sheikh Nkobo.

Sheikh Nkobo aliishutumu serikali ya CCM kwa kuwagawa Watanzania kwa misingi ya upendeleo.

"Sasa serikali ikionekana kuwa na upendeleo kama huu dhidi ya Uislamu, Waislamu wanatarajiwa wafanye nini? Waitii serikali na waiasi dini? Au waitii dini na waiasi serikali?, alihoji Sheikh Nkobo kupitia risala hiyo.

Kadhalika, aliishutumu CCM kwa kukiuka maadili ya TANU ya kujenga Taifa lenye kuzingatia haki kwa raia wote.

Bwana Said Rico, kiongozi wa kundi la Mihadhara jijini akizungumza katika baraza hilo aliwalaumu viongozi Waislamu wanaokwepa kuisema CCM wazi wazi.

Bwana Rico alisema Waislamu hawaitaki CCM kwa kuwa imeshindwa kusimamisha utawala wa haki kwa wananchi wote.

"Kama kipo chama chenye sera ya haki sawa kwa wote Waislamu hawana budi kukipa kura zao", alisisitiza kiongozi huyo.

Naye Amir wa Shura ya Maimamu, Sheikh Juma Mbukuzi aliwataka Waislamu kutekeleza kwa vitendo yale wanayoahidi.

Alisema kama Waislamu wamegundua udhaifu wa chama kilichopo madarakani, waelimishane nchi nzima ili itakapofika Oktoba wakinyime kura zao ili kiondoke madarakani.

Hafla hiyo ya aina yake ilihudhuriwa na maelfu ya Waislamu wakiwemo maafisa wa serikali na baadhi ya Wabunge Waislamu kupitia CCM.

Wakati huo huo, Amir wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi amesema Chama Cha Mapinduzi kinaelekea kimeshindwa kuongoza nchi.

Akiongea na gazeti hili nyumbani kwake jana, Sheikh Juma alisema CCM haiwezi kuondoa dhulma dhidi ya Waislamu, hivyo ambacho Waislamu wangepaswa kufanya ni kutafuta chama chenye sera na muelekeo.

Aidha, aliwataka Waislamu kuwa na vikao vya mara kwa mara kujadili hali ya uongozi wa jamii kabla ya uchaguzi mkuu.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook