Wakazi wa Jangwani wahoji, wahame waende wapi?


WIKI moja toka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Yusuph Makamba kutoa amri ya kuwaondosha kwa nguvu, walio mabondeni wameeleza wapo tayari kuondoka endapo serikali itawalipa gharama zao na kuwapeleka mahala penye huduma za kijamii.

"Sisi tuko tayari kuhama hapa endapo serikali itatulipa gharama zetu zote na kutupeleka sehemu yenye huduma za jamii kama hospitali, barabara, shule pamoja na maji", amesema Mzee mmoja.

Wakaazi hao wa bonde la Jangwani Minazini wamedai wanasikia tu kuwapo kwa viwanja vinavyogaiwa lakini wao mahala hapo hakuna aliyepewa kiwanja na serikali.

"Sisi ni wakazi wa Jangwani Minazini hakuna hata mmoja ambaye amepewa kiwanja huko anakodai Makamba", alisema kiongozi mmoja wa hapo. Aidha, aliongeza kuwa yeye ameishi hapo miaka mingi.

Wakiongea na AN-NUUR wiki hii, wakazi hao wamesema kuwa si kama hawana akili kuendelea kukaa hapo au wanapenda bali hawana imani na huduma itakayotolewa huko watakakopelekwa. Waliufananisha mpango huo na operesheni vijiji ya 1974 na kusema kuwa huenda hii ikawa operesheni mabondeni.

Wakazi hao wa Jangwani Minazini walieleza kuwa suala la wao kuondoka mabondeni hasa hapo Minazini, viongozi wanashindwa kueleza ukweli kwani sehemu ile tayari imeshauzwa kwa Ithnasheri (Wahindi).

"Hapa bwana ni biashara hata kama watabomoa wataanzia hapa kwingine kote ni uongo tu. Walionunua hapa wanataka kuonana na sisi, uongozi unawazuia. Mwaka jana walikuja hapa baada ya mafuriko na waliongea na mimi kama mjumbe", alisema Mjumbe wa eneo hilo.

Mama mmoja mkazi wa hapo alieleza kuwa hivi karibuni walifika watoto wa Kihindi wa sekondari maeneo hayo na kuwaeleza kuwa waondoke wanataka kujenga maghorofa.

Mama huyo alieleza kuwa mwaka juzi (1998) walitembelewa na Mkuu wa wilaya Ilala na kumuomba watekelezewe mambo muhimu endapo watawahamisha hapo, walidai wapewe pesa za gharama za nyumba zao, au wapelekwe katika maeneo yenye huduma zote za kijamii lakini hawajajibiwi hadi leo.

"Tangu hapo hakuna kilichojibiwa isipokuwa agizo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa kuwa tuhame sasa twende wapi?" alihoji mama huyo.

Aidha, walieleza kuwa kama suala la mabondeni na mafuriko pia wakamuamishe Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi Msasani kwani hata kwake mafuriko yalifika.

Walisema serikari isitumie nguvu juu ya suala hilo walieleza kama kweli wanawaonea huruma wawatayarishie nyumba na wawahamishe sio tu kusema tumewapa viwanja, hali si wote waliopewa hivyo viwanja.

Walitoa mfano miaka ya nyuma kuwa watu waliokuwa maeneo ya Faya (sasa hivi) walijengewa nyumba Magomeni, waliokuwa Buguruni walijengewa Mburahati na hata Malawi Cargo waliwalipa wakazi wa pale gharama, "Kwanini serikali leo inashindwa hivyo?", walihoji.

AN-NUUR ilifika ofisi za Mkuu wa Mkoa kuonana na Mh. Yusuph Makamba kuulizia suala hili, hata hivyo, iliambiwa kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa na kikao cha ulinzi na usalama. "Mkuu ana kikao cha ulinzi na usalama", alisema Katibu wake.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook