Kuporwa shule ya Waislamu:
Mwenge kuwaka moto Jumapili


MAMIA ya maelfu ya Waislamu mkoani Kilimanjaro wanakutana Jumapili kuinusuru shule ya Mwenge kuwa miliki ya matajiri wachache. Pamoja nao, watakuwepo wengine kutoka mikoa ya jirani, Arusha, Tanga na hata Dar es Salaam.

"Uamuzi mzito" juu ya shule ya Mwenge unatarajiwa kutolewa katika mkutano huo. Imeeleza kwa kifupi sana barua ya mwaliko wa mkutano. Katika kikao cha Jumapili wanatarajiwa kuwepo wakongwe wa EAMWS ambao wataelezea historia ya shule hiyo.

Historia hiyo itajumuisha kuonesha jinsi wazee wa Kiislamu walivyotoa nguvu na mali zao kuijenga shule hiyo miaka ya 1950.

Imeelezwa kuwa, kikao hicho ni muhimu kwa Waislamu wote kwani ni moja ya fursa za kueleza udhalimu na dharau wanayofanyiwa Waislamu.

Kwamba wakati wengine wanarudishiwa majengo ya shule na vyuo vyao vilivyotaifishwa, Waislamu yao wanapewa watu wengine bila hata wao wenyewe kupewa taarifa.

Waislamu ambao watakuwa na dharura ya kutokufika wametakiwa kuwapa nauli watu wengi kadri iwezekanavyo kuwawakilisha.

Baadhi ya Waislamu wenye watoto Mwenge wamedai zoezi hili ni kazi ya "wakereketwa wa Kanisa" walioshika nafasi nyeti serikalini ili kufuta historia ya Uislamu iliyosimikwa na Sheikh Mohammed Ally Sharif.

Sheikh Ally Shariff ndiye aliyeweka jiwe la msingi la shule hiyo ya Muslim miaka ya 1950.

Wamedai kuwa kama walivyotumia ukereketwa wao kuzuia ujenzi wa Msikiti Chuo cha Ushirika, ndivyo hivyo wanataka kuifuta historia ya Muslim School Moshi.

Hata hivyo, Afisa Elimu wa Manispaa, Mama Mandara, aliye mstari wa mbele katika suala hili, amedai yote hayo yanafanywa kwa nia njema.

Naye Kamishna wa Elimu Bw. A.S. Ndeki amesema, shule hiyo inafanywa "English Medium" kukidhi matakwa ya wazazi kuwa na shule kama "Arusha School".

Taarifa kutoka Moshi zimeeleza, shule hiyo ambayo awali ilikuwa Muslim School 'inaporwa' na matajiri wachache kuifanya ya binafsi..

Katika kutekeleza azma hiyo imedaiwa unafanywa udanganyifu kusingizia 'maamuzi ya wazazi'.

Barua Na. PYBC 160/226/01/02 ya Kamishna wa Elimu inatoa kibali shule hiyo kuwa English Medium School ikidai inazingatia uamuzi wa wananchi na wazazi.

Lakini wakati barua hiyo imeandikwa Januari 12, 2000, hakuna kikao chochote si cha wananchi wala wazazi wenye watoto Mwenge kilichowahi kukaa kutoa maamuzi hayo kabla.

Kikao pekee kilifanyika Januari 27, tena kwa baadhi tu ya wazazi, na ilikuwa kupewa taarifa.

Hoja ya wazazi na Waislamu wenye shule yao ni kuwa iwapo wazazi matajiri wanaotaka shule binafsi watoto wao wasome kwa Kifaransa au Kiingereza wapewe ardhi wajenge na sio kupora shule ya "walalahoi".

Aidha, wamehoji kwanini serikali isiwape majengo ya iliyokuwa Kibo Sekondari ambayo imehamishiwa karibu na KCMC.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook