Mafunzo ya Surat Ruum - 2


"WARUMI wameshindwa katika nchi iliyokaribu nao, baada ya kushindwa kwao, watashinda".(30:2-3).

Hali ya zama zile ilikuwa ya mapambano ya mara kwa mara baina ya koo, makabila au mataifa. Qur'an ilianza kushuka zama hizi.

Vita kati ya Warumi na wafursi mwaka 610 mpaka 628 iliyotajwa katika sura hii ilikuwa na athari yake kisiasa na kidini.

Qur'an imelitumia tukio hili kama fursa ya kufikisha ujumbe kutokana namna lilivyokuwa mashuhuri zama hizo.

Muktadha tunaoujadili hapa si zile siasa za umwamba za Himaya zile kubwa zama hizo wala si ile Sympathy ya kiimani iliyooneshwa na Waislamu kwa warumi (wakiristo) dhidi ya makafiri wa kifursi bali namna Qur'an inavyoyashughulikia matatizo ya jamii kwa kuuchimba mzizi wake. Kabla ya kuziangalia baadhi ya aya za sura hii hebu tudonoe kutoka kwa baadhi ya waandishi tuone historia ya wanaadamu ilivyokosa amani ya kweli chini ya himaya za ujahili.

Mwandishi mashuhuri wa masuala ya historia Toynbee ameandika ya kwamba historia ya mwanaadamu inafuata duara ya vita na amani kwa uwiano sawia, ambao kwa uchache hukamilisha mzunguko wake kila baada ya miaka 100. Kwa mtazamo wake, historia ya ulaya ilikamilisha mzunguko huo kipindi cha kati ya 1815-1914.

Akina Napoleon Bonaparte wa Ufaransa (1769- 1821), Benito Mussolin wa Italy (1883-1945), Adolf Hitler wa ujerumani na kadhalika, ni haiba maarufu si tu kwa historia ya ulaya bali ulimwenguni ambazo hutajwa kila unapoelezwa unyama ambao wanaadamu wamekuwa wakifanyiana kila karne.

Yawezekana kama ilivyoandikwa na mtaalamu mmoja wa usuluhishi wa migogoro kuwa kuzusha vita ni kujaribu kushinikiza "suluhisho" la tatizo au hali fulani.

Hata hivyo mtaalamu maarufu wa migogoro, vita na mambo ya kijeshi bwana Quincy Wright anasema ni maradhi yaliyojikita katika jamii ambayo kinga au tiba yake ni haki, usawa na uadilifu.

Historia ina mifano mingi kuonesha usugu wa maradhi hayo kiasi kwamba hata ile iliyoonekana kuwa mikataba ya amani au "upatu" wa kiulinzi madhumuni yake hasa ni kudumisha vita.

"Ushirika wowote wa kijeshi ambao shabaha yake ni kuepusha vita hauna maana wala msingi wowote, anasema Adolf Hitler.

Mengi yameandikwa ikiwa ni pamoja na tafiti nyingi kufanywa kubainisha sababu zinazopelekea vita ambavyo mara nyingi huchukua ushuru mkubwa wa roho za watu na uharibifu wa mali ambapo wanawake na watoto huwa wahanga wakubwa.

Mwanamapinduzi ya kikomunist V.I. Lenin katika upembuzi wake ametaja maonevu na machungu yaliyosababishwa na utawala kiritimba wa kibepari dhidi ya wanyonge kuwa yalikuwa kichocheo cha mapambano na vita miongoni mwa jamii.

Mwanahistoria Bernard Brodie anahusisha milipuko ya vita na matatizo ya kiuchumi, siasa na saikolojia.

Geofrey Blainey katika "The cause of war" ametaja tamaa ya upanuzi wa mipaka kwa Taifa moja dhidi ya jingine, ubaguzi, ukandamizaji, harakati za kudai uhuru, mapinduzi na ukombozi kuwa ni miongoni mwa sababu zilizoibua vita katika jamii mbali mbali.

Qur'an imeeleza utukufu wa uhifadhi wa uhai wa mwanaadamu ikizingatia mazingira ilimoshukia. Zama zile na mpaka leo ulimwengu umezama katika ufisadi ambao hufanya uhai wa mwanaadamu kuwa si chochote. Tukirejea maelezo tuliyotangulia kuyatoa kuhusiana na himaya kuu nne zilizolizunguka bara Arabu mwaka wa 610 Miladia, tunakuta sehemu nyingi za ulimwengu watu wakiuawa, kuchomwa moto au kuzikwa wakiwa hai. Walichinjwa kama wanyama au kuteswa hadi kufa ili tu kuwafurahisha waliokuwa na hadhi au mabwana katika jamii.

Katika kipindi cha siasa za utumwa na ubwanyenye burudani mashuhuri ilikuwa ni kushuhudia pambano baina ya watumwa wawili wenye mapanga, mshindi wa pambano hilo ni yule aliyefanikiwa kumfyeka mwenzake. Hapo wapenzi hushangilia na kurejea nyumbani wakisimuliana pambano lilivyokuwa zuri. Au wakati mwingine mtumwa alilishwa vizuri sana kwa muda fulani halafu alipoonekana kuwa ana siha nzuri akatumbukizwa katika uwanja wenye kuta ndefu pande zote ili apambane na simba mwenye njaa. Kule kuhangaika kwa mtumwa kutaka kujinusuru ndio burudani yenyewe.

Wengine ilikuwa kuuana ni sehemu ya mila na desturi zao au kulitokana na imani za uchawi na sherehe.

Kwa mfano maeneo fulani kaskazini ya Tanzania ilikuwa kijana mwenyeji wa huko alipotaka kufunga ndoa alilazimika kuwinda mtu mwanaume wa kabila nyingine kama awindavyo mnyama, alipofanikiwa kumuua alikata uume wake kisha kuchomeka kwenye ncha ya mkuki kuonesha "ushujaa" kabla ya kukabidhiwa mke!

Unyama huu ulifanywa kwa fahari pasipo wahusika kuwajibika mbele ya sheria.

Ni katika mazingira kama haya Qur'an ilisimama kupiga vita unyama huo na kutangaza kwamba uhai wa mwanaadamu ni kitu kitakatifu na ikaweka amri kadhaa kuuheshimu, kuulinda na kuuhifadhi.

Ilipiga marufuku kutoa uhai wa mwanaadamu ispokuwa kwa hoja za kisheria mbele ya wasimamizi wa Haki. Na ikaweka mkazo kuwa jinai ya mauaji iandamane na adhabu kali kisheria.

Kwa mtazamo wa Qu'ran, kuwajibishwa mbele ya sheria husaidia kuleta amani na usalama katika jamii.

"Wala msimuue mtu ambaye Mwenyezi Mungu ameharamisha, ila ikiwa haki. Anakuusieni haya mpate kuyatia akilini". (6:151).

"Kwa sababu ya hayo tukawaandikia wana wa Israil ya kwamba atakaemuua mtu bila ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya fisadi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote; na mwenye kumwacha mtu hai ni kama amewaacha hai watu wote..." (5:32).

Itaendelea toleo lijalo
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook