MANISPAA Morogoro imeshutumiwa kutokana na tabia ya kujigamba kuwa inatengeneza barabara kadhaa za mjini hapa wakati huo ni mpango wa serikali kuu wa kuzijenga upya.
Shutuma hizo zimetolewa wiki iliyopita na Mhadhiri Mwandamizi wa Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo (IDS) katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Bw. Bernard Julius Kasimila wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Mount Uluguru mjini hapa.
"Viongozi wa Manispaa hii wanatushangaza sana, yaani wanawafanya wananchi hawaelewi taratibu za serikali kiasi cha kufikia kujigamba kuwa inatengeneza barabara hali ya kuwa huo ni mpango wa serikali kuu na Manispaa haihusiki kabisa", alisema na kuhoji kwanini wanazungumzia mambo haya wakati unapokaribia uchaguzi.
Aidha, Muhadhiri huyo alikemea tabia ya Manispaa hiyo kushindwa kusafisha masoko yake ambayo ni machafu wakati uwezo wa kuyasafisha wanao kutokana na fedha za ushuru na leseni wanazotozwa wafanyabiashara wa masoko hayo.
Vile vile aliilaumu Manispaa ya Morogoro kwa kutokuwa na mipango madhubuti ya kuhifadhi matunda ambayo yanaoza kutokana na hali ya hewa na hivyo kuwafanya wakulima kupata hasara ya mamilioni ya fedha na wakati huo huo kupatikana upungufu wa matunda hayo.
"Mtazamo wa Manispaa unaturudisha kwenye bajeti za miaka michache baada ya uhuru kwa kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili wakati vitu vingine vipo ndani ya uwezo wetu kuvifanya kwa kuzingatia vyanzo vya mapato yetu", alisema.
Wakati huo huo, Watanzania nchini wamefahamishwa kwamba ili waweze kuishi vizuri lazima wayatunze mazingira yao ambayo yatasaidia kudumisha afya zao kwa kutoshambuliwa na maradhi ya mara kwa mara yasababishwayo na uchafu.
Hayo yalielezwa Machi 13, mwaka huu na Afisa Elimu wa Manispaa ya Morogoro Bi Esther Mwangamila wakati akizungumza katika sherehe za siku ya skauti wa Afrika zilizofanyika katika ofisi ya mkoa ya chama hicho mjini Morogoro.
"Nimefurahishwa sana na mafanikio yenu mliyoyapata katika kuweka mazingira katika hali safi na kusaidia jamii kuepukana na magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu, hivyo natoa wito kwenu ninyi tena na Watanzania wote nchini kutunza mazingira ili kudumisha afya zetu", alisema.
Alisema kuwa baada ya kuondolewa JKT sasa
hivi shughuli zake nyingi zinatekelezwa na skauti kwa kufanya mambo mbalimbali
ya kusaidia na kuelimisha jamii hususan katika kupambana na vitendo viovu
vya uvutaji bangi, uporaji, ujambazi na umalaya ambao vitendo vingi vinafanywa
na vijana.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |