Maoni Binafsi

Waandaaji wa 'Kiti moto' acheni jazba za udini


MNAMO siku ya Jumatatu Machi 13, 2000 katika hoteli ya Kilimanjaro, Masai Studio waliandaa kipindi maarufu cha KITI MOTO. Na mgeni mualikwa siku hiyo alikuwa ni Msajili wa Vyama vya kisiasa nchini Mhe. George B. Liundi.

Baada ya maelezo mafupi ya Mhe. Liundi, kama kawaida ilitolewa nafasi kwa wananchi waliohudhuria kipindi hicho kuuliza maswali, miongoni mwao alipewa nafasi mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Adrian, yeye alimuuliza mgeni rasmi suala lifuatalo. Ninanukuu:

"Mhe. Msajili wa vyama, baada ya chama cha siasa kupata usajili wa kudumu, hatua inayofuata ni kukitangaza kwa wanachama ili kupata wanachama. Ninavyofahamu mimi, si lazima chama kitangazwe na viongozi pekee wa chama hicho, bali hata wanachama au mpenzi yeyote wa chama hicho. Na miongoni mwao ni pamoja na viongozi wa dini mbalimbali, lakini ajabu ni kwamba katika nchi hii, kuna baadhi ya viongozi wa dini fulani wanaoruhusiwa kupigia kampeni baadhi ya vyama pamoja na wagombea wao, na wengine hawaruhusiwi kufanya hivyo.

"Ushahidi ni huu, mnamo mwaka 1995 katika kampeni za uchaguzi mkuu, aliibuka kiongozi mmoja wa kanisa na kuwashawishi wafuasi wake kwamba ni lazima nchi hii achaguliwe kiongozi (Rais) mcha Mungu. Nami ninavyofahamu ni kuwa, mcha Mungu kwa Mkristo ni Mkristo mwenzake. Ajabu ni kwamba kiongozi huyo hakuonekana kuwa kafanya kosa. Lakini walipojitokeza baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu na kuongea kampeni walishambuliwa kwa maneno kuwa wanachanganya dini na siasa. Swali ni kwanini viongozi wa Kanisa wao wako huru kusema lolote linaloihusu nchi lakini kwa Waislamu ni tofauti na hivyo?". Mwisho wa kunukuu.

Kabla hajamaliza swali hilo alifuatwa na mtu mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni mtayarishaji (Producer) wa kipindi hicho na kumshambulia muulizaji kwa maneno makali mno, vitisho pamoja na kumnyang'anya Mic ili asiendelee kuuliza maswali yake. Akadai kwamba maswali yanayohusu mambo ya dini hapa hayaruhusuwi.

Ninamnukuu: "Mimi hapa ni Mkristo hivyo siwezi kuruhusu maswali kama hayo". Mwisho wa kumnukuu.

Hata kijana huyo alipoomba kubadili swali alikataliwa katakata. Sasa swali nawauliza waandaaji wa kipindi hicho MASAI STUDIO kuna baadhi ya watu ambao wanaruhusiwa kuuliza maswali na wengine hawaruhusiwi yanayohusu dini?

Ushahidi ni huu; siku alipokaribishwa kwenye kipindi kilichorekodiwa katika hoteli ya Peacoc, Mwenyekiti wa Chama cha CUF Mhe. Profesa Ibrahim Lipumba kuna mwandaaji wa kipindi hicho na mwananchi mmoja walikishutumu chama hicho kuwa ni cha Kiislamu. Hapakuwa na bughudha na wala kunyang'anywa Mic.

Sasa naomba mtueleze kama kuushambulia Uislamu katika kipindi hicho ni ruhusa na kuusema Ukristo ni dhambi. Mimi naamini kuwa viongozi wa dini ni viongozi wa jamii. Wanapopongoza vema ni kuijenga vyema jamii na wanapotoka ni kuipotosha jamii.

Sasa si vizuri kuwatetea pale wanapolaumiwa kwa makosa wanayoyafanya viongozi wao wamelikumbatia kanisa kwa muda mrefu mno. Na imefikia hata baadhi ya nyimbo za kanisa kufanywa za taifa. Tazama kitabu (Chuo Kidogo cha Sala Uk. 86). Sasa nashauri kwamba kusiwe na ukiritimba katika uaandaaji wa kipindi au tuelezwe kuwa kusudio ni kwa baadhi ya watu.

A. Msabaha,

Dar es Salaam.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook