Kilichotokea Senegal kutokea Tanzania Oktoba?


Na AHMED HUSSEIN

AKIWA nchini Zambia, Rais Benjamin Mkapa alimtumia salamu za pongezi Rais mpya wa Senegal bwana Wade.

Pamoja na salamu hizo Rais Mkapa alisema wakati umefika kwa waafrika kujenga utamaduni wa kuikubali demokrasia ya kushindwa na kushinda kupitia utaratibu wa kura.

Rais Mkapa alisisitiza kuwa viongozi walioko madarakani hawanabudi kuiga mfano wa Rais Abdou Diouf wa Senegal wa kukubali matokeo ya kura za wananchi.

Chama tawala Senegali kwa kweli kinastahiki pongezi kwa kuonesha ujasiri wa kukubali matokeo japo kilikuwa na uwezo wa kuyakataa kwa mbinu na hila za miaka 40 ya uongozi wake.

Katika uchaguzi wa nchi hiyo hapakuwa na yale tuliyoyazoea katika chaguzi zetu hapa nchini ambapo wizi wa kura, vitisho, kucheleweshwa kwa makusudi maboksi ya kupigia kura, mizengwe katika kuhesabu kura nakadhalika, hutawala zoezi zima la upigaji wa kura na matokeo yake.

Kwa hakika kama kauli ya Rais si ya kisiasa, hapa nchini napo demokrasia ikaheshimiwa kama ilivyoheshimiwa Senegali ambako chama tawala kimeangushwa, hapana shaka, mabadiliko yaliyotokea nchini humo pia huenda yakatokea hapa nchini mwezi Oktoba, mwaka huu.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi nchini, wanakiri kuwa CCM haina vigezo muhimu vya kushinda uchaguzi wa Oktoba. Ni dhahiri, kwa kulijua hilo, ndio maana CCM wamefanya hila za kubadilisha katiba. Halikadhalika CCM - Zanzibar wanagoma kuweka Tume huru ya uchaguzi.

Utafiti wa sasa unaonesha wapinzani Zanzibar wana asilimia tisini (90%) ya ushindi na kwa upande wa Bara wana asilimia Sabini (70%) ya ushindi iwapo wapinzani hao watafaulu kudhibiti wizi wa kura na udanganyifu katika zoezi la kujiandikisha na kupiga kura.

Zaidi ya hivyo, ushindi wao utapatikana iwapo tume za uchaguzi hazitakumbwa na mizengwe kama ilivyotokea mwaka 1995, hasa Zanzibar.

Hatua ya CCM kukataa ushiriki wa wapinzani katika shughuli za tume za uchaguzi sio tu kinathibitisha hofu ya chama hicho kushindwa katika uchaguzi huo, bali inaashiria pia kutokea kwa mizengwe hiyo.

Wengi wanahoji, kwani kuna ubaya gani wapinzani kushirikishwa katika zoezi la kuhesabu kura jambo linaloweza kusaidia kuondoa mashaka na tuhuma za wapiga kura dhidi ya tume ya sasa iliyoundwa na Rais wa CCM ambaye pia, inatarajiwa, atakuwa mgombea.

Wapiga kura hao wanahofia kuwa Tume hiyo haina uwezo wa kutangaza ushindi wa mgombea urais wa upinzani kwa hoja kuwa, mgombea urais mtarajiwa wa CCM mpaka muda huo bado atakuwa bosi wa tume hiyo!

Kama Jaji Kisanga alifokewa hadharani kwa kule kutoa kwake tu mapendekezo ambayo, Serikali ilikuwa na hiari ya kuyakubali au kuyakataa kama ilivyofanya, Je Jaji wa Tume ya uchaguzi atakuwa na ujasiri gani "kumuangusha" bosi wake hasa ikizingatiwa ukweli kuwa angekuwa busara zaidi kama pangelikuwa na Serikali ya mpito kama ilivyowahi kupendekezwa na wapinzani huko nyuma ili kumpunguzia nguvu mgombea urais ambaye ni Rais.

Au walau basi, kazi ya Jaji huyo wa Tume ya uchaguzi ingefanywa na mtu huru hata kutoka nje katika uchaguzi wa Rais tu na aendelee na wajibu wake kwa upande wa ubunge. Maadam tu mtu huyo akubaliwe na vyama vyote.

Kwa kweli hilo kwa kiasi fulani lingeondoa wasiwasi wa wapinzani kuhujumiwa kura zao.

Itakapotokea hujuma kwa misingi ya kuogopana, kulindana au kulinda maslahi na ajira, ni wazi watakaodhulumiwa ni wananchi wapiga kura na sio wagombea wa upinzani kama inavyodhaniwa. Kura ni mali ya wapiga kura na sio mali ya wagombea.

Kwa msingi huo, hata jukumu la kudai Tume huru ya uchaguzi sio la viongozi wa vyama vya upinzani pekee bali ni letu sisi wapiga kura.

Ili kuweza kudhibiti njama za CCM za kuvuruga uchaguzi na kuwanyima wapiga kura haki yao ya kuamua nani awe kiongozi wao, wapiga kura wanao wajibu wa kuchukua hatua mbalimbali kama vile;

Mosi, kufanya maandamano ya amani nchi nzima kudai kuwepo kwa wajumbe wa upinzani katika tume za uchaguzi japo kwa kipindi kile cha mpito tu cha uchaguzi hasa hasa kutoka vyama vitakavyosimamisha wagombea.

Hata hivyo maandamano hayo yasiwashirikishe viongozi wakuu wa vyama. Watoke viongozi waandamizi au wajumbe tu wa vyama hivyo.

Pili, matokeo ya uchaguzi na wabunge yatangazwe sambamba na vyombo vya habari kutokea vituoni. Sio kunyamaza kama ilivyofanywa Zanzibar pale matokeo ya kura za urais yalipokuwa mabaya kwa CCM.

Tatu, CCM imeamua kutopokea pesa kutoka kwa wahisani kuendeshea uchaguzi kwa kuwa inajua wahisani hao watataka pawepo na uchaguzi huru na wa haki, kwa hiyo ni jukumu la viongozi wa upinzani kuwaalika wageni wakubwa kutoka nje ili kuidhibiti CCM isiweze kupora madaraka kwa nguvu.

Nne, uchaguzi usilale au kufika usiku wa giza. Na Tume ichukue data tu kutoka vituoni sio kuhesabu upya kura usiku wa manane au kwa masiku chungu mzima kama wanakisomo wa ngumbaru, huku F.F.U. wakitisha watu na mitutu ya bunduki.

Shughuli ya kuhakiki kura, kama italazimu, ifanywe kwa kumpyuta baada ya hatua zote muhimu kuchukuliwa.

Tano, wawakilishi wa vyama vya upinzani vituoni waandaliwe kwa kufanyiwa semina ili waweze kukabiliana na vituko vya CCM. Wawe wenyeji wa maeneo husika ili kudhibiti mamluki.

Vyama vya upinzani vipeleke wasimamizi wao maeneo ya vijijini ambako inaonekana wananchi wengi hutishwa au kurubuniwa na chama tawala wakati wa kupiga kura.

Aidha mawakala wa vyama vya upinzani wawe watu makini wenye uchungu na wawe tayari kwa lolote kulinda kura za vyama vyao.

Sita, Mbinu iliyotumika Pemba kudhibiti wizi wa kura wa CCM, itumiwe na wapinzani nchi nzima.

Kwa ujumla, mipaka ya demokrasia ikichungwa ipasavyo, CCM itang'oka tu Bara na visiwani. Za mwizi ni arobaini. kama ilivyopigwa mweleka 'CCM' ya Senegal, CCM ya Tanzania nayo ijiandae!

Wananchi tujiandikishe kwa wingi na tujitokeze kwa wingi kupiga kura.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook