Na O. Kiputiputi
AMA amemwazima mwalimu au rafiki yke fulani kwani hawaoni thamani ya kitabu kilichoandikwa kwa lugha ambayo haielewi. Lakini elimu ya sekondari ikifundishwa kwa Kiswahili wanafunzi watavithamini sana vitabu vya masomo yao.
Na kwa vile vitabu ndio hazina ya elimu basi wanafunzi wataanza kupata elimu ya kweli, na pengine kwa msaada mdogo sana wa mwalimu. Kwa maneno mengine endapo Kiswahili kitatumika kufundishia sekondari, ule ugomvi mkubwa uliopo sasa kati ya Wizara ya Elimu na wanafunzi huenda ukapungua kwa kiasi kikubwa kwani wanafunzi hawatahitaji sana twisheni kama ilivyo sasa.
Wanafunzi wanaojiweza wataweza kujisomea wenyewe peke yao au katika vikundi na kujadili mambo yaliyofundishwa mara wamalizapo masomo ya kutwa kuliko ilivyo sasa ambapo mwalimu analazimika kufundisha darasani na baadaye kwenye twisheni. Siku hizi twisheni imekuwa nafasi ya kitabu cha kiada. Hii ni tatizo kubwa sana katika mfumo wa elimu. Kitabu cha kiada kina nafasi pekee katika mfumo mzuri wa elimu. Nafasi yake haiwezi kuchukuliwa na kitu kingine chochote.
Pengine ushahidi mwepesi wa hoja ya kushuka kwa utamaduni wa kujisomea unaweza kuelezwa vizuri kutokana na usomaji wa magazeti. Siku hizi kuna aina nyingi ya magazeti yanayochapwa kwa Kiingereza na kwa Kiswahili. Waulize wauza magazeti wote watakwambia wauza magazeti mengi ya Kiswahili kuliko Kiingereza.
Ni kawaida kukuta watu kwenye mabasi, maofisini, mashambani, viwandani na kadhalika wakisoma magazeti. Magazeti haya yapo ya nyanja mbalimbali kama vile elimu, burudani, habari na kadhalika. Yote yananunuliwa tena kwa wingi karibu kila siku na watu wa aina mbalimbali pamoja na wanafunzi. Watu wanapenda kujua mambo mapya kila siku, sasa iweje wanafunzi ambao ndio kwanza wanatafuta elimu ili ije iwasaidie katika maisha yao hapo baadaye wanapenda kusoma magazeti lakini hawapendi kusoma vitabu vyenye elimu kubwa kubwa.
Elimu ya sekondari ikifundishwa kwa Kiswahili itawaandaa vyema vijana wetu kulitumikia taifa lao vizuri zaidi, kinyume na ilivyo sasa ambapo wasomi wa Afrika hawatayarishwi ili kuwasiliana na watu wao (Prah, 1994), yaani wasomi wachache ambao wana fursa ya kutumia lugha za Kizungu hawawezi kujiimarisha vilivyo katika lugha hizi ili hatimaye waweze kuwa wabunifu wazuri wa masuala ya sayansi na teknolojia. Akisisitiza zaidi, Prah anadai kuwa maendeleo ya kweli ya sayansi na teknolojia yataanza kupatikana pale tu ambapo maendeleo yenye misingi na asili ya utamaduni wa Kiafrika yatazingatiwa. Akifafanua zaidi Prah, anasema:
"Elimu ya sayansi na teknolojia lazima ijengwe kwenye kile kilichopo. Na kilichopo kwa Waafrika wengi huko vijijini ni elimu ya asili iliyojikita kwenye desturi, mila na utamaduni wa Mwafrika. Kuanzia hapa ndipo juhudi juu ya kuleta maendeleo na elimu ya kweli inafaa kuanzia endapo juhudi hizi zinahitajika kuwafikia watu wengi na hivyo kusaidia kuboresha maisha yao (Prah, 1994)". (tafsiri ni yangu).
Athari ya kutumia lugha ya kigeni kama lugha ya kufundishia sayansi na teknolojia katika nchi za dunia ya tatu, kama asemavyo Pattanayak (1986) ni udumavu wa akili na ukosefu wa ubunifu kwa watoto wa Kiafrika na kufifisha utamaduni wa asili. Lugha hizi za kigeni sio tu kwamba zinakwamisha ukuaji wa lugha za asili, lakini pia zinazuia mwingiliano kati ya sayansi na jamii, huzalisha teknolojia bandia isiyofaa kwa jamii. Hali kadhalika lugha hizi huzalisha wasomi ambao hupenda kuiga maisha ya nchi zilizoendelea.
Kwa muda mrefu elimu ya sayansi na teknolojia nchini Tanzania imebaki kuwa mali ya wasomi wachache tu. Hata matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa juu ya sayansi na teknolojia, kama vile njia bora za kilimo cha kisasa, uvuvi wa kisasa na kadhalika pia yamebaki kuwa mali ya wasomi wachache. Wananchi walio wengi hawana nafasi ya kuyafahamu kwani hawawezi kujifunza kwa vile elimu imekumbatiwa na Kiingereza ambacho hakieleweki vizuri na wengi.
Akisisitiza juu ya faida kubwa itokanayo na kufundisha sayansi na teknolojia kwa lugha ya asili Brock-Utner (1985) naye anatoa mfano wa mafanikio yaliyopatikana kwa jamii ya Sri Lanka baada ya kuanza kufundishia sayansi na teknolojia katika lugha za Sinhala na Tamil kama alivyonukuliwa Ranaweera.
"Mabadiliko kutoka Kiingereza na kutumia lugha ya taifa kama lugha ya kufundishia masomo ya sayansi yalisaidia kuondoa kikwazo kikubwa kilichokuwepo kati ya jamii ndogo ya wasomi wachache, kati ya wachache waliosoma na watu wengi ambao walikuwa hawakusoma sayansi, kati ya sayansi yenyewe na watu. Ikatoa hali ya kujiamini kwa mtu wa kawaida kwamba sayansi haipo mbali naye na anaweza kuifikia akitaka na kwa walimu na wanafunzi, ujuzi wa Kiingereza sio lazima uwe ndio sharti muhimu la kujifunza sayansi. (Runaweera 1976:423)".
Hatuna sababu yoyote ya msingi ya kutoamini kuwa hata Watanzania tutapata mafanikio endapo tutaanza kufundisha elimu ya sayansi na teknolojia kwa Kiswahili.
Kulikuwa na hofu pia miongoni mwa baadhi ya Watanzania kuwa kwa vile hakuna hata nchi moja ya Kiafrika Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyofanikiwa kuacha lugha ya kigeni na kufanya lugha ya Kiafrika kuwa lugha ya kufundishia, basi ni hatari kwa Tanzania kufanya hivyo. Lakini tukiacha Tanzania, hakuna hata nchi moja ya Kiafrika iliyoko kusini mwa jangwa la Sahara ambayo imefanikiwa kuwa na lugha ya taifa ya Kiafrika. Zote bado zinatumia lugha za kigeni kama lugha za taifa. Sasa wangeipata wapi lugha ya Kiafrika na kuifanya kuwa lugha ya kufundishia. Ama kuhusu faida ya kutumia lugha za Kiafrika kufundishia masomo ya sayansi na teknolojia maoni ya wanachuo katika vyuo vikuu vya Lesotho, Botswana, Swaziland na Afrika ya Kusini, Mdee (1999) anaorodhesha faida zifuatazo kama zilivyobainishwa na Prah (1995) katika mahojiano na wanachuo hao:
Wananachi wanaoishi vijijini wataelimika haraka sana.Waafrika watajiamini na kupenda utamaduni na historia yao.Waafrika watakuwa wabunifu.Lugha nyingi za Kiafrika zitakua.
Waafrika watafanikiwa kufanya vizuri katika masomo yao. Waafrika kwa ujumla wataelewa dhana ya sayansi na teknolojia. Waafrika watakaokuwa wajua sayansi na teknolojia wataongezeka.
Bila shaka wenzetu hawa wanatushangaa sana Watanzania, kwani licha ya kuwa na lugha yetu ya Taifa, Kiswahili na ambayo imeimarika na kufanikiwa katika masuala mengi kama vile kutuletea uhuru, umoja na mashikamano wa kitaifa, tunasita kukiruhusu Kiswahili pia kitusaidie kusukuma mbele maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo tunayahitaji sana, sasa tunasita kufanya hivyo.
Baada ya kuzungumzia mambo ya jumla kuhusu lugha ya kufundishia, hebu sasa tuangalie lugha ya wanasayansi na masharti yake.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |