BARUA


Shime Moro tujibu changamoto ya Luanda

Ndugu Mhariri

NAPENDA kumshukuru Bwana Luanda K.S. (Nolo) kwa shairi lake maridadi lilitoka katika toleo lililopita la gazeti hili.

Shairi hilo limetoa changamoto kwa Waislamu Morogoro kuweka kumbukumbu ya tukio la kinyama la miaka kadhaa iliyopita ambapo polisi wa serikali ya CCM walivamia Msikiti wa kiwanja cha ndege usiku na kumlipua kwa mabomu pamoja na kuunajisi kwa viatu.

Kutokana na shambulio hilo, Waislamu wawili walipoteza roho zao. Ndugu yetu Luanda ametushauri kuwafanyia Khitma mashahidi hao utakapofika mwezi Julai.

Hata hivyo, mimi naona kuwa, kwa kuwa muda mrefu sana umepita, ni vema tufanye hima kufanya khitma hiyo wakati wowote kuanzia sasa. Halafu mwezi Julai tufanye Ijitmai ya kumbukumbu ya uvamizi wa polisi na mauaji.

Hitma hiyo iwashirikishe watu wote mkoani na nje ya mkoa ili ukweli kuhusu tukio lile ueleweke ipasavyo na Waislamu wa Morogoro na mikoa mingine waelezwe nini cha kufanya kulipiza kisasi cha unyama tuliofanyiwa.

Fursa hiyo pia itumike kutoa tathmini ya madhila na dhulma tuliyotendewa Waislamu kabla na baada ya uhuru.

Ni matumaini yangu kuwa Waislamu Morogoro tutalipa uzito unastahili suala hili wakati tukielekea Oktoba- InshaAllah.

Said Fikirini,
Morogoro.


Heko Maimamu kwa kuikataa CCM

Ndugu Mhariri

NAPENDA kutumia nafasi hii kuwapongeza Maimamu wa Dar es Salaam kwa kutoa tamko la kuunga mkono kampeni za kisiasa za kuing'oa CCM madarakani mwezi Oktoba mwaka huu.

Kwa hakika, hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wa Kiislamu kutoa kauli ya pamoja dhidi ya CCM. Mwaka 1995 viongozi wa dini ya Kiislamu walilaumiwa na wananchi kwa kuipigia debe CCM.

Katika uchaguzi wa mwaka 1995, kura nyingi zilizoiweka CCM madarakani zilitoka kwa wananchi wa dini ya Kiislamu hasa hasa wale wa mikoa ya kusini na pwani.

Uteja huo wa Waislamu kwa CCM ulitokana na viongozi wetu kukosa msimamo thabiti. Mwaka huo walijitokeza makachero na madalali wa CCM waliojifanya viongozi na wasemaji wa Waislamu walipayuka Misikitini kudai kutetea haki za Waislamu huku wakiwa na agenda zao kibindoni.

Ni vema CCM ielewe mapema kuwa yeyote watakayempa "zawadi" safari hii, basi wajue wamempa "zawadi ya bure". Haitoambulia chochote.

Kauli iliyotolewa na Maimamu ndio msimamo wa Waislamu katika uchaguzi wa mwaka huu. Ni dhahiri wapenda haki na wapinzani wote wa CCM wamefarijika sana na msimamo huo wa wananchi wenzao.

Hivyo, wananchi kwa ujumla wetu, tuelekee kwenye vituo vya kupigia kura, mwezi Oktoba kwa azimio na lengo moja la kuhitimisha utawala wa CCM.

Kwali kweli, kidemokrasia na kiuchumi, nchi yetu inahitaji uongozi mwingine makini na madhubuti. Hata wakereketwa wa CCM wanaukubali ukweli huo japo hawawezi kuunena hadharani.

Naomba Maimamu wa mikoa yote ya Bara na visiwani walisambaze tamko la Maimamu wa Dar es Salaam kwa waumini na wananchi wa mikoani mwao. Kwa upande mwingine sina wasiwasi sana na msimamo wa Wachungaji kwani wao wako makini tena wengine wamo katika vyama vya upinzani.

Kwa kumalizia, nawaasa wananchi wa din zote kwamba wasimtii wala kumfuta kiongozi yeyote wa Msikitini au Kanisani mwenye msimamo wa kuipendelea CCM hata akiwa Sheikh, Imamu, Mufti, Askofu, Padri, Paroko au Kadinali.

Abdallah Dobi,
Dodoma.


CCM Chama Cha Wakristo?

Ndugu Mhariri

Dk. John Sivalon anatuonesha uhusiano uliopo wa muda mrefu kati ya Kanisa Katoliki, serikali ya Tanzania Bara (Tanganyika) na Chama Cha Mapinduzi tangu mwaka 1953.

Si hayo tu, pia malalamiko yote ya Wakristo yamekuwa yakipelekwa chamani badala ya serikalini. Na chama chenyewe ni CCM. Mathalan tumeshuhudia Kanisa hivi karibuni likiitahadharisha CCM juu ya Dk. Salmin kuongezewa muda wa utawala, ikimaanisha kwamba Kanisa ni sehemu ya utawala.

Na ndio maana leo hii kunaonekana dhahiri kupendelewa upande mmoja na kukandamizwa upande wa pili, yaani Waislamu na dini yao.

Inatupasa Waislamu tusisahau na pia tusikatae ukweli huo, kwa kuambatanisha na maelezo ya Almarhuum Sheikh Hassan bin Ameir katika waraka wake alioutoa Agosti 26, 1963. Katika waraka huo, alieleza jinsi lengo la kugombea uhuru lilivyobadilishwa na kufanywa kuwa ni kwa faida na manufaa ya dini moja tu baada ya uhuru wa Tanganyika.

Jinsi vilivyoletwa vimidla, baada ya uhuru wa Tanganyika na katikati ya bendera amesimama MARIA kabeba mtoto mchanga. Nyuma ya vimidla kumeandikwa "Maria mtakatifu ulinde uhuru wa Tanganyika".

Jinsi George Kahama alivyotumwa na serikali ya Tanganyika kuwa mwakilishi katika mkutano mkuu wa makanisa ya Roma. Jinsi bendera ya Taifa ilivyoshushwa nusu mlingoti nchi nzima kwa kifo cha marehemu Pope Yohane wa 23. Jinsi mkutano mkuu wa makanisa fulani wa Tanganyika ulivyofanyika ndani ya Bunge mwaka 1963.

Yote hayo yanatuthibitishia Ukristo wa CCM na serikali yake. Lakini CCM hiyo hiyo ndiyo inayovipaka matope vyama vyingine kuwa vinachanganya dini na siasa, kwa lengo la kuficha uhalisi wake.

Hata Waislamu waliomo CCM wamekuwa ngazi tu ya kutekeleza mipango ya kuimarisha Ukristo nchini.

Tuchukue mfano wa Zanzibar inavyokandamizwa kiuchumi na kisiasa na CCM ya Bara, ingawaje nchi zote mbili zinazoongozwa na serikali za CCM. Na lengo la Kanisa ni kumvunga kila Muislamu na kumdhoofisha kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, bila ya kujali yuko chama gani.

Jihadi ya Waislamu wote iko Oktoba, 2000, kwa kura zetu za "hapana" kwa CCM.

Akhukum bin Juma,
Zanzibar.


Wanafunzi Waislamu tukumbuke azma yetu

Ndugu Mhariri

NAPENDA kuwakumbusha wanafunzi Waislamu Tanzania kukumbuka azma yetu tuliyoiweka katika kikao cah TAMSA mwezi Desemba mwaka 1999 juu ya kumsaidia mwanafunzi mwenzetu aliyedhulumiwa kwa kupigwa risasi Chuki Athumani.

Kimsingi haina haja ya Waislamu Tanzania kuzungumzia tu kwa mdomo habari za Chuki Athumani bali ni kuonesha umoja wetu na umadhubuti wetu katika kuutetea Uislamu na haki za Waislamu Tanzania na kwingineko.

Kumpeleka Chuki Athumani kutibiwa kwa fedha za Waislamu na Waislamu kuendelea kuikumbusha serikali juu ya dhulma waliyoifanya ya kuwaua Waislamu na raia wa Tanzania wasio na hatia ni jambo la msingi kwa Waislamu wakati huu.

Fedha zichangwe kutoka kwa wanafunzi na Waislamu wengine kote nchini.

Wanafunzi Waislamu katika kila shule Tanzania wachangishe chochote watakachoweza kupata ili kuhakikisha kwa namna moja au nyingine mwanafunzi mwenzetu Muislamu mwenzetu anaishi na kupata huduma za kijamii kama inavyotakikana.

Waislamu wa Kilimanjaro Muslim Students Association (KIMUSA) tulishakubaliana kuchanga fedha kwa ajili ya Chuki Athumani na tayari fedha hizo zimeshachangwa katika shule mbalimbali tayari kupelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya kumnusuru Muislamu mwenzetu.

Wanafunzi Waislamu Tanzania tukumbuke kuwa Allah (s.w.) anachukizwa sana na wale wanaoyasema wasiyoyatenda Qur'an (61:3). Ni matarajio yangu kuwa InshaAllah mtatekeleza maazimio yetu ya kikao cha TAMSA.

AMIR,
KIMUSA
S.L.P. 8387,
HAI
MOSHI.


Tusiwadhalilishe Allah na Mtume wake

Ndugu Mhariri

KWA muda sasa kumezuka katika uzungumzaji wa mawaidha kwa baadhi ya wahadhiri kuwasikia wakimwita Mtume (s.a.w) "Profesa".

Yawezekana wanafanya hivyo kwa nia njema kabisa wakijaribu kumpa sifa yeye ndiye "Profesa wa Maprofesa" au "Profesa Mkuu", au labda pia ni katika jitihada ya kuyafanya mawaidha yao yaonekane ya kisasa zaidi na yanayokwenda na wakati.

Hata hivyo, pamoja na nia zao njema wanazoweza kuwanazo, ni maoni yangu kuwa huko ni kumkosea Mtume wa Allah na kumshusha hadhi yake kama Mtume wa Mungu. Ziko sifa na majina ya Mtume (s.a.w.) vile alivyosifiwa na kuitwa na Allah (s.w.) mwenyewe pamoja na vile Mtume mwenyewe alivyotufundisha.

Sote tunajua Uprofesa unavyopatikana, hauwezi asilani kulinganisha na Utume ambao umeambatana na kupokea Wahyi kutoka mbinguni. Kuvilinganisha hivi viwili ni kupoteza mizani na kumdhalilisha Mtume wa Allah.

Mtume (s.a.w.) mwenyewe katufundisha tumwite "mja wa Allah na Mjumbe wake", na hiyo ni hadhi kubwa sana mbele ya Allah kuliko hizo hadhi nyingine tunazomtafutia.

Vile vile wako waliofikia kumwita Allah (s.w.) eti ni "Rais wa dunia". Nao pia yawezekana ni kwa nia njema katika kumsifu Allah (s.w.) ili aonekane ndiye aliye juu ya Marais wote, yaani "Rais wa Marais". Bahati mbaya sana katika sifa zote na majina yote ya Allah (s.w.) hakuna Urais.

Hata kama itasemwa kuwa jina hilo limeazimwa tu ili kukidhi maana fulani iliyokusudiwa bado hoja hiyo haiwezi kusimama kwa sababu majina na sifa zote za Allah (s.w.) vinatosheleza hali zote zilizopo na zitakazokuja kuwepo, bali hata zilizokuwepo.

Hili nalo ni kosa na utovu wa shukrani kwa Allah (s.w.) ambaye katufundisha sifa na majina yake na akatuagiza tumuite na kumuomba kwa majina hayo. Manasara wamekosea katika kufru yao ya kumfanya binadamu Mungu lakini wanaweza kusema kuwa ni kumtukuza kwa ile hali ya kumtoa kwenye ubinadamu na kumkweza hadi kwenye uungu. Lakini isemweje kwa sisi tunaotaka kumtoa Allah (s.w.), Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo, kutoka kwenye uungu na kumleta chini kabisa kwenye Urais?

Saballah J.R.
Shinyanga.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook