KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI


Kakojolea bendera ya Mjumbe wa nyumba kumi

Ngurumo, Alhamisi Machi 10, 1966

MANENO Salum, Mnyamwezi anayekaa Tandamti Street, Dar es Salaam, jana alihukumiwa katika korti ndogo ya Kariakoo kulipa faini ya shilingi 160 ama kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kuiteremsha bendera ya mjumbe wa nyumba kumi akaichana chana na kuikojolea.

Maneno alitiwa nguvuni tarehe 23 mwezi wa jana saa tano na dakika tano usiku Nyamwezi Street akiinyararafu bendera ya Taifa.

Ilielezwa pale kortini mbele ya Hakimu Bw. Samwel Lwimba, kuwa yule mjumbe mwenyewe Juma Mgeni, Mzaramo, pamoja na watu wengine walijaribu asifanye kitendo chake. Lakini walishindwa ndio wakaitwa polisi.

Mashitaka

Kufika Polisi Stesheni, Maneno akafunguliwa mashitaka mawili. La kwanza, kufanya ghasia, la pili ulevi.

Mshitakiwa alikiri makosa yake bila kuwapo polisi ambao walimkamata, lakini alisema alifanya hivyo juu ya ulevi.

Hakimu Bwana Lwimba akamtaka mshitakiwa aseme chochote kabla ya kutoa hukumu yake.

Mshitakiwa akasema anao watu wanaomtegemea na anaomba apewe adhabu nyepesi ili wale watu wanaomtegemea wasipate tabu sana kutokana na adhabu yake.

Kosa la kwanza

Hakimu akamwuliza mshitakiwa: Je, ni mazowea yako kulewa? Mshitakiwa akajibu, ndiyo.

Hakimu akamwuliza Polisi kama mshitakiwa anayo makosa ya zamani kama haya, polisi asema hawana habari za mshitakiwa kuwa alipatikana na mambo kama hayo siku zilizopita.

Kosa baya

Hakimu akasema akimwambia mshitakiwa: Ingawa rekodi yako haijafika polisi, kuonesha hili ni kosa lako la kwanza, lakini nitakuhukumu kwa kosa hili: Sababu kosa lenyewe la kuteremsha bendera ya mjumbe wa nyumba kumi kuchana chana na kuikojolea na kulewa ni baya sana.

Akamuhukumu faini ya shilingi 160 ama miezi sita jela. Hakimu akampa mshitakiwa nafasi ya mwezi mmoja kukata rufani.

Mshitakiwa alikuwa hana faini Ndugu wa mshitakiwa alisimama kuomba muda wa kulipa faini.

Hakimu akakataa. Baada ya hakimu kutoa hukumu, Ngurumo ilimwona mwanamke mmoja ambaye bila shaka ni mkewe akifuta machozi.


Wakristo watakutana kesho

Ngurumo, Alhamisi Machi 24, 1966


 


CHAMA cha Wakristo hapa Tanganyika kitafanya mkutano wake mkbwa hapa Dar es Salaam katika Salvation Army kuanzia leo na kesho Ijumaa.

Mkutano huu utafuata baada ya mkutano wa kamati ambayo ilikutana tangu tarehe 7 Juni mpaka tarehe 8 Juni 1966. Kamati hii ndani yake mna wakuu wa Makanisa yote na dayosisi na mashirika yake.

Sababu kuu ya mkutano huu, imetajwa kwamba ni kutafuta uhusiano wenye nguvu zaidi. Bwana John Kamau, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wakristo nchini Kenya atatoa hotuba ambayo itakuwa kama ufunguo wa mkutano, hotuba hiyo itakuwa na kichwa cha maneno "Ahadi za Ushirika".

Mkutano wa mwaka huu umeelezwa kwamba utakuwa wenye shughuli nyingi na za maana sana. Kutakuwa na kubadili sura ya chama chenyewe, hii inajumlisha kupata misaada zaidi ya fedha kutoka hapa nchini.

Chama hiki kinanuia kufanya mabadiliko fulani katika katiba yake, moja ya mabadiliko hayo itakuwa katika chama kwa jina la Kiswahili, Tanganyika itabadilishwa kuwa Tanzania na jina hilo la Kiswahili inakisiwa kuwa litakuwa Jumuiya ya Kikristo Tanzania.

Chama kimeeleza kwamba wanachama wake ni wa kila aina ya Wakristo kama Moravian, Lutheran, Anglican, Mennonite, Makanisa ya Baptist, Mission kadha wa kadha na vyama vingi kama Y.M.C.A. na Y.W.C.A..


Marekani 2,559 wafa Vietnam

Ngurumo, Jumamosi Machi 19, 1966


 


HABARI kutoka Saigon zimeeleza kwamba katika mashambulio ya hivi karibuni, kati ya majeshi ya wananchi na yale ya Marekani, karibu askari 100 wa Kimarekani wamekufa na askari 800 wamejeruhiwa, na askari 8 mpaka sasa hawajulikani walikokimbilia.

Mapigano hayo yalichukuwa siku 6 mfululizo. Habari hizi zimeendelea kueleza kwamba haya yalikuwa mapigano makubwa sana ambayo bado hayajaanza kutokea tangu vita hivyo vya Vietnam kuanza.

Habari nyingine kutoka mjini Washington zinasema kuwa msemaji wa jeshi la Marekani amesema kuwa tangu hapo Marekani ilipopeleka majeshi yake Vietnam mpaka sasa, askari wapatao 2,559 wamekufa na wengi zaidi wamepoteza viungo vyao.


Kirundu achaguliwa Meya wa Dar


Ngurumo Jumatano Januari 5, 1966

HALMASHAURI ya Mji wa Dar es Salaam jana jioni ilimchagua Diwani Ramadhani Omari Kirundu kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kura 22 kati ya kura 27 zilizopigwa.

Aliyekuwa Makamu wa Meya, Diwani Francis Kashaija alipata kura mbili tu katika uchaguzi huo. Diwani Hija akapata kura moja na Diwani Simkoko kura moja na kura moja ikaharibika.

Diwani Kirundu amekuwa Meya wa Dar es Salaam kwa muda wa miaka mitatu mfululizo sasa.

Katika uchaguzi wa kumchagua Makamu wa Meya, Diwani Kashaija alipata kura 21 kati ya kura 27 zilizopigwa. Diwani Simkoko akapata kura tatu, Diwani Kungulilo kura moja na Diwani Chambuso kura moja. Kura moja iliharibika.

Nusu mwaka

Baada ya kutangazwa matokeo hayo na Deputy Town Clerk, Bwana Ganatra, Mheshimiwa Kirundu alisimama na akasema kuwa wao wataendelea kuwa Meya na Makamu wa Meya mpaka mwezi Juni, 1966 wakati uchaguzi wa Madiwani wote wa Halmashauri utakapofanywa na akamshukuru Makamu wake kwa msaada aliompa mwaka uliopita.

Maendeleo

Aligusia juu ya maendeleo yaliyofanywa na Halmashauri ya Mji mwaka jana, Diwani Kirundu alieleza juu ya kupanua mfereji wa maji mtaa wa Kariakoo, kupanuliwa kwa masoko huko Magomeni, Temeke, Kariakoo na Ilala pamoja na matengenezo ya machinjioni.

Mwisho akawaomba Madiwani wadumishe uhusiano kati yao na watu waliowachagua.


Makao makuu yahamishiwa Kibaha


Ngurumo, Jumatatu Machi 21, 1966

BAADA ya miaka miwili kutoka sasa, Ofisi Kuu ya Mkoa wa Pwani itahamishiwa huko Kibaha, maili 24 kutoka Dar es Salaam. Haya yalitangazwa na Mkuu wa Mkoa, Bwana Selemani Kitundu alipokuwa akihutubia mkutano wa Halmashauri ya Utendaji ya TANU (TANU Regional Executive Committee).

Bwana Kitundu aliwaeleza wajumbe kazi za ofisi yake. Alisema kwamba wakuu wa Idara zote katika mkoa ni lazima wafanye kazi zao vema wakifuata utaratibu na siasa ya serikali. Pia alisema kwamba ofisi kuu ya TANU ya mkoa itajengwa mjini Dar es Salaam kufuata mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

Aliwataka watu wote wabadilishe tabia zao, na kuwa na moyo wa kujitegemea. Aliwaomba wajumbe watilie mkazo kilimo na ufugaji ili wananchi wapate maisha bora. Alisema katika mkoa wa Pwani kuna mazao mengi ya kudumu, kwa hiyo ulikuwa mkoa tajiri.


Bw. Wilson kapigwa yai viza


Ngurumo, Alhamisi Machi 24, 1966

POLISI wa Uingereza wamemkamata na kumwonya vikali mtoto mmoja mdogo aliyempiga yai viza Waziri Mkuu wa Uingereza, Bwana Wilson. Bwana Wilson mwenyewe aliwataka polisi wasifanye mashitaka kwa mtoto huyo na akasema kuwa mtoto huyo angefaa sana kwa mchezo wa Kriketi.

Daktari aliyempima Bwana Wilson amesema kuwa ameumia kidogo kwenye jicho hilo lililopigwa yai hilo viza.

Itakumbukwa kwamba Rais wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta miaka michache iliyopita aliwahi kufanyiwa dhihaka kama hiyo ya kupigwa yazi viza, lakini aliyempiga yeye hakuwa mtoto mdogo bali alikuwa ni mtu mzima.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook