Yangelizuka majungu
Yeye wa tangu na tangu, mwanzo
mwisho hana,
Mmoja Mwenyezi Mungu, katu mshirika
hana,
Muumba nchi na mbingu, na vyote
vilojazana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi
kaepukana.
Mfanowe hana Mungu, kiumbe akafanana,
Si watatu kwenye mbingu, baba,
roho wala mwana,
Yangalizuka majungu, sheria
kufarakana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi
kaepukana.
Halali, hachoki Mungu, hasahau
Sub hana,
Mjuzi wa mambo chungu, yote
yalofichikana,
Kwenye ardhi na mbingu, hanaye
wa kushindana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi
kaepukana.
Mlezi Mwenyezi Mungu, atulisha
Maulana,
Mtandazaji mawingu, mvua zanyesha
mwanana,
Minanasi na mikungu, miembe
inashonana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi
kaepukana.
Kaumba Mwenyezi Mungu, sura
kutofuatana,
China, Mwarabu, Mzungu, rangi
zisizofanana,
Kabila za ulimwengu, kilugha
zinapishana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi
kaepukana.
Razaku Mwenyezi Mungu, mgawaji
kwa mapana,
Atupa pweza na changu, bahari
wazaliana,
Michuzi yajaza chungu, samaki
wanoneana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi
kaepukana.
Muweza Mwenyezi Mungu, zake
sifa nyingi sana,
Nemaze kwako na kwangu, tele
zimerundikana,
Kuhesabu kwa mafungu, idadi
yashindikana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi
kaepukana.
Beti nazifunga pingu, mwisho
ninatulizana,
Nawapisha na wenzangu, sitaki
kusema sana,
Waseme sifa za Mungu, wende
wazame kwa kina,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi
kaepukana.
Idd Kikong?ona,
Morogoro.
1+1+1=1 (Sisitizo)
Saa nyingine nacheka, hawa mabwana
wawili,
Viumbe wana mashaka, ya Mungu
vitendawili,
Haja yao wanataka, eti waipinge
Injili!
Ona walivyong?ang?ana, taka
mchunguza Mungu!
Kama huyu S. Luanda, na mwenzake
Kikong?ona,
Kutwa kucha wanawinda, uongo
kuulizana,
Na ukweli wanapinda, viumbe
wamekutana,
Ona walivyong?ang?ana, taka
mchunguza Mungu!
Moja wapo wasema, Mungu mfano
wa mvule!
Mbao tatu akipima, kuwa moja
iwe pale,
Kabisa amesimama, hana hofu
mtu yule,
Ona walivyong?ang?ana, taka
mchunguza Mungu!
Watu hawa ni masikini, mawazo
yao hafifu,
Kabisa tu hawamwoni, Yehova
wa utukufu,
Tena hawako makini, kumwelewa
mtukufu,
Ona walivyong?ang?ana, taka
mchunguza Mungu!
Kwanza hivyo ni kufuru, Yehova
hachunguziki,
Meng?ang?ana kama faru, kuambiwa
hawataki,
Ngoja tuwape uhuru, wapunguze
hamaki,
Ona walivyong?ang?ana, taka
mchunguza Mungu!
Jambo moja sikia, ninyi mnaong?ang?ana,
Yehova akichukia, siku hiyo
mtaona,
Takimbia mkilia, hata pa kwenda
hamna,
Ona walivyong?ang?ana, taka
mchunguza Mungu!
Heri mngesonga mbele, kusema
ya Mwembe chai,
Na mambo ya chama kile, kukichania
uhai,
Kulikoni jambo lile, waungwana
muko hoi,
Ona walivyong?ang?ana, taka
mchunguza Mungu!
Mwinjilisti,
B.E. Dettu,
S.L.P. 60474,
Dar es Salaam.
Kukichagua chafaa? (Jibu)
Sikiliza D tatu, majibu beti napanga,
Hiki si chama cha watu, vyema kukipiga chenga,
Tusikipe kura zetu, kiwe kinatangatanga,
Hiki si cha kuchagua, kina mama sikiliza.
Sasa tusemeni basi, ni mwiko kukichagua,
Tukifatuwe kwa kasi, miguu kukipindua,
Rukwa, Tabora, Masasi, na kote kukiumbua,
Hiki si cha kuchagua, sikiliza kina dada.
Hii ndiyo yake dawa, wanyonge kujikwamua,
Tusiseme sawasawa, vema tukakipatia,
Hali tutaziokowa, machungu yataishia,
Hiki si cha kuchagua, sikilizeni vijana.
Balaa tutazikinga, sasa nawapasulia,
Lindi, Kigoma na Tanga, Pwani Kilwa na Songea,
Mwanza, Arusha na Iringa, ikiwa mnachungua,
Hiki si cha kuchagua, sikilizeni wazee.
Ahadi zote ni hewa, kipi tulichoambuwa?
Yale tuliyoambiwa, mbona hatukutendewa,
Yafaa kikasusiwa, cheupe kukichaguwa,
Hiki si cha kuchagua, sikiliza wananchi.
Mbele sitoendelea, cha siku nyingi sikia,
Ndicho kinachotuua, madhara kinatutia,
Dikupa nawe Luanda, julisha Watanzania,
Hiki si cha kuchagua, sikiliza wananchi!
Mtoto Mtaun (Mtafiti),
S.L.P. 4
Kilwa - Kiwawa.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |