ASASI hizi ni mbali na vyama na vikundi vya wananchi wenyewe, kama vile vyama vya Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA), Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA), Chama cha Wachapishaji wa Vitabu Tanzania (PATA) na kadhalika.
Ili sera ya kutumia Kiswahili itekelezwe vilivyo, lazima vyombo vyote hivi vihusishwe na vifanye kazi yao kwa ufanisi unaotarajiwa. Kwa bahati mbaya uzoefu umeonesha kuwa vyombo hivi havijafanikiwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu, ama kwa sababu ya ukosefu wa fedha na nyenzo, ama kwa sababu nyinginezo. Mathalan, BAKITA, mkuzaji mkuu wa Kiswahili, kwa kipindi kirefu lilikuwa likipewa fedha za kulipia mishahara tu na huduma ndogondogo, na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake halisi. Matokeo ya hali hii ni kwamba "Baraza" kwa hakika halipo, waliopo ni watendaji tu, maana wajumbe wa Baraza hawajakutanishwa kwa zaidi ya miaka 15! Isitoshe, licha ya ukata huo uliokithiri, BAKITA kwa kipindi fulani lilikabiliwa na matatizo ya uongozi na tuhuma za ufujaji wa fedha.
Taasisi ya Elimu nayo halikadhalika haikubadilisha mahtasari wa somo la Kiswahili kwa zaidi ya miaka 20. Hivyo shule zetu zilikuwa zinafundishwa Kiswahili cha miaka ya 60 mwaka 1990!
Mashirika ya uma ya uchapishaji na usambazaji wa vitabu yamekufa au kuuawa kimya kimya. EAPL halipo tena, na haijulikani mali zake zilizozirithi kutoka EALB zinatumikaje na kwa manufaa ya nani, TPH linakaribia kukata roho na maiti yake kuuzwa kwa mchawi atakayehitaji, BAKIZA linaishi kwa kubahatisha, na kadhalika. Kwa ujumla, hali ya mashirika ya Kiswahili, isipokuwa machache yanayojimudu, inasikitisha.
Iwapo kweli tunataka Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia, itabidi TET waandae silabasi za masomo yote na miongozo ya walimu kwa Kiswahili, TUKI waandae vitabu vya sarufi na makamusi, na tafsiri za vitabu vya taaluma mbalimbali, BAKITA waandae istilahi za kutosha na wasimamie mpango mzima wa utekelezaji, na TPH na DUP na mashirika ya ushapishaji ya binafsi yaandae na kuchapisha vitabu vya masomo yote yanayohusika, na kadhalika. Bali hali halisi inaonesha kwamba baadhi ya asasi hizi hazitamudu kazi hiyo. Hivyo hatuna budi kujiuliza: Je, tutaweza kweli kukifanya Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia bila kuimarisha asasi za kutekeleza uamuzi huo?
Shinikizo kutoka nje
Uamuzi wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia, kama uamuzi mwingine wowote wa kujikomboa, haukosi kuwaudhi waliokuwa wakinufaika na hali iliyopo. Kuhusu suala la lugha ya kufundishia, ni wazi kuwa wenye kunufaika tunapoendelea kutumia Kiingereza ni Waingereza na labda Wamarekani. Mwingereza anafahamu fika kuwa Kiingereza ndiyo raslimali yake kuu duniani, na kwa usahihi kabisa anatetea na kukiendeleza dunia nzima, na asingependa kuona matumizi yake yanapunguwa popote pale ulimwenguni. Ripoti ya Baraza la Kiingereza (British Council) ya mwaka 1987/88 inaeleza jambo hili vizuri:
Britain's real black gold is not North oil, but the English language. It has long been the root of our culture and now is fast becoming the global language of business and information. The challenge facing us is to exploit it to the full.
(British Council (1987/88), kama ilivyodondolewa katika Schmied 1991:
Kama hivyo ndivyo, hapana shaka kuwa taifa hili kubwa litafanya kila njia kuzishinikiza nchi ndogo zisikitupilie mbali Kiingereza, na kwa kweli ndivyo lifanyavyo kwa njia za wazi na za kificho. Mataifa mengine makubwa, mathalan Ufaransa, halikadhalika yanazishinikiza nchi zenye kutumia lugha zao ziendelee kufanya hivyo. Mathalan, uhusiano kati ya Ufaransa na Rwanda siku hizi umedorora kwa sababu kadha, ikiwemo ile ya watawala wapya wa Rwanda kupendelea kutumia Kiingereza zaidi katika shughuli zao.
Jibu la tatizo hili ni kusimama imara kutetea uhuru wetu na haki yetu ya kujiamulia mambo yetu wenyewe, na kukubali kuyakabili matokeo ya msimamo huo (ambayo yanaweza kuwa machungu).
Hitimisho
Makala haya yamejadili baadhi ya vikwazo vya
kiutawala vinavyokwamisha utekelezaji wa uamuzi wa kutumia Kiswahili kufundishia
elimu ya sekondari na vyuo. Vikwazo vilivyozungumziwa ni: Migongano ya
sera, ukosefu wa msukumo wa kisiasa na kisheria, kasumba, na ujuaji unaotokana
na kasumba, udhaifu na kutelekezwa kwa vyombo vya kukuza Kiswahili, na
mwisho, shinikizo kutoka nje ya nchi. Ili kuweza kuyakabili na kuyashinda
matatizo haya, ingefaa hatua zifuatazo zichukuliwe haraka:
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |