TOLEO lililopita katika makala haya tuliona kwa msukumo wa silka yake, mwanadamu anawajibika kutambua na kutenda haki zinazogawanyika katika sehemu kuu tatu. Mosi, haki za Muumba wake. Pili, haki za nafsi yake na tatu haki za wanadamu wenziwe ambao hujumuishwa na kuitwa jamii. Ijapokuwa zipo pia haki za viumbe wengine lakini hapa tutazitazama aina hizo kuu tatu za haki. Toleo hili Mwandishi S. HUSSEIN anaelezea zaidi
Kuamini Qur'an
INGAWA wanadamu tumetakiwa kuiamini Qur'an pasina mashaka yoyote, bado tunatakiwa pia kutumia kikamilifu akili zetu kuzitafakari kwa makini aya za kitabu hicho kitukufu.
Kinachovutia zaidi ni kuwa Qur'an yenyewe imetoa changamoto kwa wanaadamu waihoji kama kweli ni kitabu cha Mungu. Na kwa kweli watu mbalimbali wakiwemo wataalamu wa masuala mbalimbali walijikuta wakisilimu na kuwa waumini thabiti baada ya kufanya jitihada za kiutafiti na kuichambua Qur'an kwa shabaha ya kutafuta makosa au mapungufu yoyote ndani ya kitabu hicho.
Wanataaluma walioisoma Qur'an kwa mtazamo huo wameweza kuzipatia majibu aya za Qur'an ambazo awali zilionekana kama mutashabihat (ngumu kueleweka) na maandiko yao juu ya Qur'an yameuzindua ulimwengu kutoa msukumo mpya kwa walimwengu kuukubali ukweli na muongozo wa Qur'an.
Kwa hivyo, kama walivyofanya wataalamu hao, watu wengine ambao hawajauona ukweli wa Qur'an ni vyema wafanye hima kukiangalia kitabu hicho ikiwezekana wakilinganishe na kitabu kingine chochote kinachoitwa kitakatifu.
Tusome tafsiri mbalimbali za Qur'an kwani kila mfasiri amejaaliwa uwezo na maarifa ya aina yake ya kuelewa na kufafanua aya za Qur'an. Hata hivyo, udhaifu wa tafsiri usinasibishwe na Qur'an.
Kwa kufanya hivyo, mwanadamu anakuwa amefikia hatua muhimu ya kiimani baada ya ile ya kumjua Muumba kwa kutumia akili yake. Sio tu atathibitisha imani yake bali pia atapata muongozo unaowafikiana na silika au umbile lake.
Mwenyenzi Mungu amejieleza ipasavyo katika Qur'an. Hivyo, msomaji ataimarisha itikadi yake juu ya kuwepo kwa Muumba mmoja tu. Hapa ndipo inapopatikana tauhiid ambayo sasa ndiyo inayompa Mwenyezi Mungu nafasi yake halisi katika maisha ya viumbe.
Hatua inayofuata baada ya kumjua Mungu na kupata muongozo wake, ni kumtii kwa kutekeleza yale yote aliyoyaamrisha. Na kwa ufupi wa maneno ni kwamba Mwenyezi Mungu ametupa maelekezo juu ya kila kipengele cha maisha yetu.
Haki za nafsi
Kwa kuwa tumekwishaona kuwa nafsi imeumbwa basi haki yake ya awali ni ile ya kumjua na kumtii Allah. Kwa kufanya hivyo nafsi itakuwa imepata haki yake ya kupata pepo ambayo imewekwa kwa ajili yake. Kinyume na hivyo nafsi itakuwa imejidhulumu ikikosa pepo na kuingia motoni. Ili kuyaendesha kwa ufanisi maisha ya kujiandaa kwa maisha ya akhera, nafsi inahitaji elimu likiwa ni jambo la msingi kabisa.
Kwa kupata elimu sahihi nafsi hiyo itakuwa imeweza kufikia hadhi yake ya ukhalifa hapa duniani. Kwa kufikia hadhi hiyo, nafsi itakuwa imepata haki yake ya kimaumbile na kuwa bora kuliko viumbe wengine.
Kwa kuwa msimamizi wa dunia hii, nafsi itakuwa imesimamia haki ya kutodhulumu wala kudhulumiwa. Nafsi itakuwa na sehemu yake ya haki katika rasilimali za dunia hii. Kwa hali hiyo nafsi itapata haki yake ya kula vizuri na vya halali, kunywa vizuri, kuvaa mavazi mazuri na ya halali, kuishi katika makazi mazuri na kadhalika.
Haki za binadamu wenziwe
Haki za binadamu wenziwe zinaambatana na matendo yake ya kila siku. Kwa hiyo la msingi la awali ambalo litamuwezesha mja kuwatendea haki zote wanadamu wenziwe ni kuwalingania na kuwafikishia ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo walivyofanya Mitume.
Lengo la kufanya hivyo ni kuwaita watu katika msingi wa haki zote yaani muongozo wa Mwenyezi Mungu. Mbali na kuwawezesha wenzie kupata haki za kidunia, pia atawasaidia kupata yale malipo mema ya akhera ambayo ndio haki bora ya kila nafsi na kuwaepusha na ule moto wa Jahannamu ambao ndio dhulma mbaya kabisa dhidi ya nafsi.
Hata hivyo, waukubali au wasiukubali mwongozo wa Muumba bado mja muumini ahakikishe kuwa mwenendo wake unabaki kuwa kigezo cha haki daima. Kwa maneno mengine awe mfano mwema wa kuigwa kwa kauli zake na vitendo vyake.
Matendo yake
Muumini ahakikishe hawi kero kwa wenziwe na badala yake awe faraja kwao. Aepuke kuwaudhi watu kwa namna yoyote ile na awe na subira kwa maudhi yanayofanywa dhidi yake. Awe na mazoea ya kuwahi kuwasalimu watu mahali popote pale na ikiwezekana kwa kupeana mikono.
Awe mwenye kutafakari jambo kabla ya kusema. Akitukanwa ajizuie kujibu tusi. Katika maongezi aelemee zaidi katika kumfurahisha Allah kuliko kufurahisha watu. Awe msamehevu pale anapokosewa, lakini asiwe mnyonge pale anapoonewa
Anapomtakiwa lugha mbaya ajibu lugha njema. Atumie saikolojia ya lugha hasa anapotaka kuwasilisha neno dhidi ya mtu au taarifa mbaya kwa mtaarifiwa. Ajitahidi kusema ukweli muda wote. Aepuke michezo na mazungumzo ya kipuuzi (laghwi), aepuke fitna, kibri, usengenyi na kebehi.
Aepuke husuda na badala yake awe na wivu kwa mambo yenye thawabu. Atosheke kwa kidogo cha halali anachokipata na asisononeke kwa kukosa kingi cha haramu. Aepuke majisifu, majigambo na majivuno kwa chochote alichonacho. Atumie afya yake, mali yake, elimu yake na wasaa wake katika mambo mema kabla shetani hajamuhadaa kutumia neema hizo katika maasi.
Asimdharau mtu kwa daraja lake, ufukara wake, ulemavu wake, kiwiliwili chake au umbile lake. Awe pamoja na wanyonge na awe msemaji wa wanaodhulumiwa. Asimuhusudu na kumpa hadhi mtu kwa mali, nguvu, madaraka, rangi au kabila bali amuheshimu sana mtu anayemcha Mungu.
Aishi vyema na majirani pasipo kukejeli dini au imani zao. Ashirikiane nao katika shida za kimaumbile kwa kadri awezavyo na aepukane na maasi yao bila kugombana nao.
Matendo ya ucha Mungu
Muumini awe na kawaida ya kuswali swala za sunna kabla na baada ya swala za faradhi.
Aswali sunna za usiku, afunge hasa Jumatatu na Alhamisi, atoe sadaka kila apatapo wasaa, asaidie wenziwe katika mamb e jema au ovu hata kama ni dogo sana ambalo akilifanya ama asipolifanya halileti athari. Jambo la namna hiyo ni jepesi kwa nje lakini linaathari kubwa kiimani.
Achunge amana, mara zote atekeleze ahadi hata kama ni kwa jambo dogo, atumie mkono wa kulia kwa matendo twahara na mkono wa kushoto kwa najisi na aingie msalani kwa mguu wa kushoto na kutoka kwa mguu wa kulia.
Aingie Msikitini kwa mguu wa kulia na kutoka kwa mguu wa kushoto, ajitahidi kumjengea mapenzi yule anayejitahidi kumjengea uadui au angalau aepuke kumchukiza, amtendee wema yule aliyemtendea yeye uovu na aupukane kuweka kinyongo, donge au mfundo, aepuke kutamka matusi kwa hali yoyote ile.
Aepuke kutenda uovu pale ambapo ana uwezo na wasaa wa kuutenda na atende mema hata pale anapoweza kutenda wema, awe mwepesi kuomba toba pale anapotetereka. Awahurumie viumbe hata wanyama, wadugu na ndege. Awe jasiri pale penye kitisho. Awe na utamaduni wa kuhimiza watu kutenda mema na moyo wake umpende atendae mema na kumchukia atendae maovu kwa makusudi. Aepuke kuwabeza au kuwadharau wengine.
Awapendelee wengine lile ambalo nafsi yake inalipenda na mwili wake kuburudika kwalo madhali liwe jema. Amsaidie na kumuhurumia yule anayelikosa zuri hilo.
Asipendelee zaidi nafsi yake kuliko ya mwenziwe au wenziwe mathalan kama pana sahani yenye sambusa nne, mbili kubwa na mbili ndogo, naye amepewa nafasi ya kuanza kuchukua, au ameanza kula kabla ya wenzie, basi achague sambusa kubwa moja na ndogo moja la sivyo achukue ndogo tupu lakini aepuke kabisa kuchukua kubwa tupu.
Hata akinunua kitu kama vile embe, chungwa, au kingine chochote huku akiwa na mwenzie au wenziwe, japo ana haki zaidi na kitu hicho lakini ajitahidi kugawana sawasawa na mwenzie au wenziwe.
Anapokuwa mahali na wenziwe huku wote wakiwa na njaa, ajitahidi kuepuka kula peke yake au kukubali mwaliko wa chakula bila kuwashirikisha wenzie alioshinda nao njaa. Ama wote wakose au wote wapate chakula hicho.
Penye hafla au mjumuiko na wenzake, muumini aepuke kupendelewa chakula kingi na kizuri zaidi kuliko wenziwe.
Pia muumini asipendelee nafasi ya mbele katika hafla hata kama yeye ni mtu mzima au Sheikh. Hasa hasa katika mikusanyiko ya furaha. Ni heshima kubwa mtu kuitwa mbele na ni fedheha kubwa mtu kuombwa urudi nyuma. Hata hivyo katika vita au mapambano yoyote ya haki, muumini anatakiwa awe mstari wa mbele bila kuombwa. Muumini asipende umaarufu usio wa lazima. Ajitahidi kufanya mambo mena na mazuri pasipo kudhamiria umaarufu au sifa.
Muumini awe mpole na mkarimu kwa kila mtu pasina kujali mtu huyo yukoje. Awe na heshima kwa kila mtu, awe na kauli njema. Awasemehe wanaostahiki msamaha wa madeni. Akiwa na wasaa, basi akiombwa mkopo hasa na fukara, basi ni jambo la taqwa akigeuza mkopo huo kuwa sadaka. Na yeye akikopa basi ajihimu sana kulipa deni kwa wakati uliopangwa.
Ahakikishe analipa deni hata kama aliyemkopesha amefariki. Kama anazidishiwa chenji, arudishe sehemu ya pesa iliyozidi. Anapopimiwa bidhaa, ahakikishe haki inatendeka ila labda mpimaji amuongezee kwa ridhaa yake, lakini yeye asilazimishe kuongezewa kipimo kinyume na thamani ya pesa zake. Anapookota kitu hata kama ni cha thamani kubwa, maadam amemuona aliyekiangusha basi amrudishie.
Kwa ujumla muumini anapaswa kusononeka pale anapolazimika kukiuka amri ya Mwenyezi Mungu. Ajitahidi kuepukana na jambo hilo.
Matendo ya kistaarabu
Muumini akipendelewa kitu na mwenziwe basi na yeye ampendelee kitu hicho huyo huyo mwenziwe. Kwa mfano wapo watu wawili wanaotaka kukaa mahali tuseme kwenye kiti, mmoja wao anapoamua kumpendelea mwenzie akalie kiti hicho, basi yule aliyependelewa asikimbilie kukaa haraka haraka bali naye asite na kumpendelea mwenzie. Awapishe viti walimzidi umri.
Vivyo hivyo, wawili wanapokuwa na kiu, inapoletwa glasi moja ya maji, basi mmoja anapohiwahi kumuachia mwenzie yule anayeachiwa naye amwachie mwenzie. Akumbuke mwenzie kamuachia kwa mapenzi na huruma nae arudishe maji hayo kwa mwenzie ili kuonesha kuwa nae pia ana mapenzi na huruma kama vile alivyo mwenzie.
Muumini anapokwenda nyumbani kwa mtu kisha asimkute baba mwenye nyumba, kama hakuna udhuru, basi ajiepushe kuingia ndani na hata akiingia asikae sana bali afikishe ujumbe wake na kuondoka. Sio anamkuta mama mwenye nyumba anatazama Televisheni na yeye anakaa kuangalia. Kama ana udhuru wa kukaa, basi mama mwenye nyumba ajihifadhi na kuchunga mipaka ya ukaaji na uzungumzaji.
Muumini anapokaribishwa nyumbani kwa mtu asiguse kitu chochote bila idhini ya mwenyewe au wenyewe hata kama kitu hicho ni cha kawaida kama vile gazeti. Huwezi kujua pengine gazeti hilo limetumika kufunikia pesa na pengine mtu mwenye mkono wa birika amekwishazikwapua pesa hizo. Sasa unapolichukua gazeti hilo bila kuwaomba wenyewe kuna hatari ya kutuhumiwa wewe. Lakini ungeomba, wenyewe wangeangalia pesa zao kabla ya kukupa gazeti hilo.
Muumini anapoingia nyumbani kwa watu na kukuta wenyewe wanakula, kama ataona chakula kidogo, aepuke kuitikia mwaliko isipokuwa labda awe na njaa ya kufa. Muumini aepuke vyakula vya kufikia labda kiwe kinaandaliwa kwa ajili yake.
Na muumini anapokaribishwa chakula, hata kama hakipendi bado asithubutu kukikebehi au kutoa neno lolote dhidi ya chakula hicho zaidi ya kusema ameshiba au angalau kula kidogo.
Muumini anapofikiwa na wageni, ajitahidi kuwakirimu kwa kadri ya uwezo wake. Hata kama chakula chake ni kiduchu asikifiche uvunguni na wala asimshauri mkewe asipakue mpaka wageni waondoke. Ila kwa wageni wenye khulka ya ulafi na udowezi kwa kuingia ovyo majumbani mwa watu nyakati za kula, hekima inaweza kutumika.
Muumini anapoamka kitandani ugenini, ahakikishe anatandika kitanda, sio kwa vile mgeni basi ndio atelekeze kitanda na kuwaachia kazi ya kutandika wenye nyumba.
Muumini anapokuta watu wawili au zaidi wanaongea, ajiepushe kuingilia kati maongezi hasa kama yanahusu mambo binafsi ya wahusika. Mazungumzo yasiyomuhusu asikae karibu na wazungumzaji. Ipo kauli ya kistaarabu isemayo mkimya ni Sultani mbele ya waropokaji.
Muumini asiteme mate au makohozi bila kufuikia. Aepuke kurusha mate kama nyoka njiani au mbele za watu. Asipenge kamasi na kukokotoa makohozi kwa sauti mahali wanapokula watu.
Ahakikishe anatumia kitambaa kutemea mate au makohozi katika hadhara iwapo hana namna ya kuchapuka kando iwapo hakuna udongo au mchanga wa kufikilia uchafu huo wa kinywa.
Lakini kuweza kutekeleza yote haya na mengine mengi, muumini hana budi kujielimisha kwa kuhudhuria darsa na kusoma Qur'an, Hadith za Mtume (s.a.w) pamoja na vitabu mbalimbali vya Tauhiid na Akhlaq.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |